Uwezo wa uzalishaji umeme Tanzania wafikia MW 4,646

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Juma Homera amesema, uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini Tanzania umeongezeka hadi kufikia Megawati 4,646 kutokana na kukamilika kwa baadhi ya miradi ya nishati, huku Serikali ikiendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza uzalishaji hadi kufikia Megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.
Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Homera akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam leo Oktoba 18, 2026.

Dkt. Homera ameyasema hayo leo Oktoba 18, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme nchini, utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu, ujenzi wa njia za kusafirisha umeme na shughuli za utafutaji wa gesi asilia.

Amesema, ongezeko hilo limetokana na uwekezaji katika vyanzo mbalimbali vya nishati ikiwemo maji, gesi asilia na jua, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa matumizi ya wananchi, viwanda na wawekezaji.

Uzalishaji Umeme Megawati 8,000 nchini Tanzania 

Waziri huyo amesema, Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kuongeza uzalishaji wa umeme ili kufikia Megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030, lengo linaloendana na mwelekeo wa maendeleo uliowekwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Amesisitiza kuwa, kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme kunapaswa kwenda sambamba na kuboresha miundombinu ya usafirishaji ili kuhakikisha nishati inayozalishwa inawafikia watumiaji kwa uhakika na kwa wakati.

Miradi ya Nishati Jadidifu

Akizungumzia matumizi ya nishati jadidifu, Dkt. Homera amesema, mradi wa umeme wa jua wa Kishapu I, wenye uwezo wa kuzalisha megawati 50 umekamilika na unaendelea kufanya kazi.

Ameongeza kuwa, Serikali inaendelea na maandalizi na utekelezaji wa mradi wa Kishapu II, unaotarajiwa kuongeza megawati 100, huku miradi mingine yenye jumla ya megawati 600 ikiwa katika hatua mbalimbali za majadiliano na utekelezaji.

Pia, amesema miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za kupanua vyanzo vya uzalishaji wa umeme na kuongeza uwezo wa nchi kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nishati.

Njia za Kusafirisha Umeme Zaimarishwa

Dkt. Homera amesema, Serikali inaendelea kuboresha njia za kusafirisha umeme ili kuongeza ufanisi wa usambazaji na kuimarisha upatikanaji wake katika maeneo mbalimbali nchini.

Ametaja njia ya kusafirisha umeme ya Chalinze– Dodoma kuwa imekamilika tangu Septemba, mwaka huu ambapo imechangia kuimarisha upatikanaji wa umeme na kuongeza uwezo wa kusambaza nishati kuelekea mikoa ya Magharibi na Kaskazini.

Kuhusu mradi wa Iringa- Tunduma- Sumbawanga, Dkt. Homera amesema, ujenzi wake umefikia hatua za kukamilishwa, huku Serikali ikitarajia kuanza kuingiza umeme huo kwenye gridi ya taifa mwezi Novemba, 2026.

Pia, ameeleza kuwa, kuunganishwa kwa mradi huo na gridi ya taifa kutaimarisha upatikanaji wa umeme katika Nyanda za Juu Kusini, kuchochea shughuli za viwanda na uwekezaji pamoja na kuongeza fursa za biashara ya umeme na nchi jirani ya Zambia.

Aidha, amesema mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya Chalinze–Kinyerezi hadi Mkuranga unatarajiwa kuwashwa Februari, 2027.
Mradi huo, amesema unalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme jijini Dar es Salaam na maeneo ya viwanda vya Mkuranga, ambayo yanaendelea kuwa muhimu katika shughuli za uzalishaji na uwekezaji.

Vilevile, ametaja mradi wa Songea–Tunduru hadi Maumbika kuwa unaendelea kutekelezwa, huku mkandarasi akiwa eneo la kazi.

Amesema, mradi huo ni miongoni mwa hatua zinazolenga kuimarisha miundombinu ya umeme na kupanua huduma ya gridi ya taifa katika maeneo ya kusini mwa nchi yakiwemo mikoa ya Lindi na Mtwara.

Utafutaji wa gesi asilia waendelea

Akizungumzia sekta ya gesi asilia, Dkt. Homera amesema, shughuli za uchimbaji zimeendelea katika maeneo mbalimbali zikiwemo vitalu vya Songo Songo Magharibi, Mnazi Bay Kaskazini na Ntorya.

Waziri huyo amesema, visima vitatu, viwili vya uendelezaji na kimoja cha utafiti, vimekamilishwa huku shughuli nyingine za uchimbaji zikiendelea kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa gesi asilia nchini.

Amesema, matokeo ya shughuli zinazoendelea yanaashiria uwezekano wa kuongeza upatikanaji wa gesi, jambo litakalosaidia kuimarisha uzalishaji wa umeme na upatikanaji wa nishati kwa matumizi mbalimbali ya kiuchumi.
Dkt. Homera amesema, Serikali inatarajia kukamilisha hatua zilizopangwa katika baadhi ya shughuli hizo ifikapo Desemba 2026, huku ikiendelea kufuatilia maendeleo ya miradi husika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here