Vijana Tanzania 2026: Mafanikio si njia za mkato, bali maarifa

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesisitiza umuhimu wa kujenga mazingira yatakayowawezesha vijana wote nchini kunufaika na fursa za kiuchumi bila kujali maeneo wanayoishi, kiwango cha elimu au mazingira yao ya kijamii na kiuchumi.
Amesema, kuhakikisha vijana wanapata fursa sawa za elimu, ujuzi, ajira, mitaji, teknolojia na masoko ni hatua muhimu katika kukuza uchumi jumuishi na kufikia malengo ya maendeleo ya Tanzania kuelekea mwaka 2050.

Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo Oktoba 10, 2026 wakati akifungua rasmi Wiki ya Vijana Kitaifa 2026 katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua iliyopo Kata ya Kizwite, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba.

Maadhimisho hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana,” inayolenga kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha vijana kutoka maeneo na makundi mbalimbali wanapata nafasi ya kutumia uwezo wao, kushiriki katika shughuli za uzalishaji na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Mkenda amesema, tofauti za mazingira wanayoishi vijana hazipaswi kuwa kikwazo cha kufikia malengo yao, akieleza kuwa jukumu la Serikali na wadau ni kuhakikisha mifumo ya uwezeshaji inawafikia vijana mahali walipo.

Amesema, kijana anayeishi kijijini, mjini, visiwani au maeneo ya pembezoni, pamoja na vijana wenye ulemavu, wanapaswa kuwa na nafasi ya kupata taarifa, mafunzo, mitaji, teknolojia na masoko kulingana na mahitaji na uwezo wao.
Amesisitiza kuwa, fursa sawa haimaanishi kuwafanya vijana wote wafanye shughuli zinazofanana, bali kujenga mazingira yatakayomwezesha kila mmoja kuanza, kukua na kushindana kwa haki katika eneo analoweza kufanya vizuri.

Vijana ni zaidi ya theluthi moja ya Watanzania

Akifafanua, umuhimu wa uwekezaji katika kundi hilo, Profesa Mkenda amesema, takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonesha kuwa Tanzania ilikuwa na vijana 21,312,411 wenye umri wa miaka 15 hadi 35 sawa na asilimia 34.5 ya watu wote nchini.

Amesema, kati ya vijana hao, 20,612,566 walikuwa Tanzania Bara na 699,845 Zanzibar, hali inayoonesha ukubwa wa mchango ambao kundi hilo linaweza kutoa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, idadi hiyo ni rasilimali muhimu kwa Taifa, lakini manufaa yake yatategemea uwezo wa nchi kuwaandalia vijana mazingira yanayowezesha upatikanaji wa elimu bora, ujuzi, huduma za afya, ajira, mitaji na nafasi za kushiriki katika maamuzi.

Amebainisha kuwa, vijana wanapaswa kupewa nafasi ya kuwa wazalishaji, wabunifu, wajasiriamali na viongozi, badala ya kutazamwa kama kundi linalohitaji msaada pekee.

Ukosefu wa ajira bado ni changamoto

Profesa Mkenda amesema, pamoja na hatua zilizopigwa katika kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana, bado kuna haja ya kuongeza juhudi za kuunda ajira zenye tija na staha.
Amesema, takwimu za Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi zinaonesha kuwa, kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 kilipungua kutoka asilimia 8.3 mwaka 2024 hadi asilimia 7.5 mwaka 2025.

Ameeleza kuwa, kupungua kwa kiwango hicho ni hatua chanya, lakini hakupaswi kutafsiriwa kuwa changamoto ya ajira imetatuliwa, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa ajira, kuboresha ujuzi unaohitajika sokoni na kuweka mazingira rafiki kwa vijana wanaotaka kujiajiri.

Pia, amesema mabadiliko ya teknolojia na mifumo ya uzalishaji yanaendelea kubadilisha mahitaji ya soko la ajira, hali inayolazimisha vijana kujiandaa na fursa mpya zinazotokana na Akili Unde (AI), biashara mtandao, nishati safi, uchumi wa buluu, kilimo cha kisasa, uchakataji wa mazao na huduma za kidijitali.

Amesisitiza kuwa, mifumo ya elimu na mafunzo inapaswa kuandaa vijana kwa mahitaji ya sasa na yajayo, kwa kuwapatia ujuzi wa kutatua matatizo, kutumia teknolojia, kuanzisha biashara na kuongeza thamani katika shughuli za uzalishaji.

Uwezeshaji wa vijana ni uwekezaji wa kimkakati

Akizungumzia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Waziri huyo amesema, kufikiwa kwa malengo ya Tanzania kuwa na uchumi jumuishi, shindani na wenye ustawi kunategemea kwa kiasi kikubwa ushiriki wa vijana katika sekta za uzalishaji, biashara, sayansi, teknolojia, viwanda na huduma.
Amesema, uwekezaji katika maendeleo ya vijana si jambo la hiari, bali ni sharti muhimu la kufikia maendeleo endelevu yanayotarajiwa na Taifa.

Waziri Mkuu kupitia hotuba hiyo amesema, Serikali itaendelea kuhakikisha masuala ya vijana yanaingizwa katika mipango na bajeti za kisekta ikiwemo kilimo, viwanda, biashara, TEHAMA, utalii, madini, mifugo, uvuvi, sanaa, michezo na huduma za fedha.

Amebainisha kuwa, ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni muhimu katika kuimarisha uratibu wa sera na programu za maendeleo ya vijana ili kuhakikisha wanapata fursa bila kujali upande wa Muungano wanakotoka.

Amesema, kuimarishwa kwa Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana na Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji ya Zanzibar ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uratibu wa masuala yanayohusu vijana.

Serikali yaongeza juhudi za upatikanaji wa mitaji

Profesa Mkenda amesema, Serikali inaendelea kuimarisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili kuongeza upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu, sambamba na mafunzo ya biashara, elimu ya fedha na usimamizi wa miradi.

Amesema, lengo ni kuhakikisha mikopo inayotolewa kwa vijana inakuwa nyenzo ya kujenga biashara endelevu zinazokua, kuongeza ajira na kupanua masoko.

Vilevile, ameeleza kuwa, katika mwaka wa fedha 2026/27, Serikali imeongeza kiwango cha fedha zinazotengwa kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya mikopo na uwezeshaji wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15.
Amesema, ongezeko hilo linatarajiwa kupanua wigo wa upatikanaji wa mitaji na kusaidia utekelezaji wa miradi ya pamoja inayolenga kuboresha mazingira ya biashara na ujasiriamali.

Hata hivyo, amewataka vijana kuandaa miradi yenye tija, kusimamia fedha kwa nidhamu na kurejesha mikopo kwa wakati ili kuwezesha fedha hizo kuendelea kuwafikia wanufaika wengine.

Amesisitiza kuwa, uwezeshaji wenye matokeo haupaswi kuishia katika kutoa fedha pekee, bali unapaswa kuhusisha mafunzo, ushauri wa kibiashara, upatikanaji wa masoko na ufuatiliaji wa maendeleo ya miradi.

Vijana wanufaika wa zabuni za Serikali

Akizungumzia fursa zinazopatikana kupitia ununuzi wa umma, Profesa Mkenda amesema, Serikali imeendelea kutenga sehemu ya zabuni kwa makundi maalumu, yakiwemo makundi ya vijana ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kukuza biashara zao.

Amesema, taarifa zilizowasilishwa bungeni mwaka 2026 zinaonesha kuwa, vikundi 299 vya vijana vyenye jumla ya wanachama 2,226 vilikuwa vimepata zabuni zenye thamani ya Shilingi bilioni 13.2 kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).

Amezitaka taasisi zinazohusika kuendelea kutoa elimu na msaada kwa vijana kuhusu taratibu za ununuzi wa umma, maandalizi ya nyaraka na masharti ya kushiriki katika zabuni.
Waziri huyo amesema, hatua hiyo itasaidia vijana wengi zaidi kunufaika na fursa zilizopo, huku akiwahimiza kujenga uwezo wa kutekeleza mikataba kwa wakati na kutoa bidhaa na huduma zenye viwango vinavyotakiwa.

Kilimo, madini na teknolojia vyatajwa kuwa vyanzo vya ajira

Profesa Mkenda amesema, Serikali inaendelea kufungua fursa katika sekta mbalimbali za uchumi, akitaja kilimo, mifugo, uvuvi, madini, viwanda, biashara na teknolojia kuwa miongoni mwa maeneo yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira kwa vijana.

Katika sekta ya kilimo, amesema vijana wanaweza kunufaika kupitia uzalishaji wa kibiashara, uchakataji wa mazao, uongezaji thamani, usambazaji na masoko, huku programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ikiendelea kuwa miongoni mwa mipango inayolenga kuwavutia vijana katika kilimo cha kisasa.

Akizungumzia sekta ya madini, amesema fursa zinapatikana katika uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji thamani wa madini, biashara na utoaji wa huduma zinazohusiana na shughuli za migodi.

Amesema, pia sekta za mifugo na uvuvi zina nafasi katika ufugaji wa kibiashara, uzalishaji wa maziwa na nyama, ufugaji wa kuku na samaki, uchakataji, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa.

Kwa upande wa viwanda na biashara, amesema, vijana wanaweza kuanzisha na kukuza biashara ndogo na za kati, kushiriki katika uzalishaji wa bidhaa na kutumia masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ameongeza kuwa, maendeleo ya teknolojia yanafungua fursa katika uundaji wa programu tumizi, huduma za kidijitali, biashara mtandao, Akili Unde na usalama wa mifumo ya taarifa.
Katika sekta ya elimu, ametaja Samia Scholarship kuwa miongoni mwa fursa zinazolenga kuwaendeleza vijana wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi.

Profesa Mkenda amesema, kwa mwaka wa masomo 2026/27, wanafunzi 1,000 wamepata ufadhili wa masomo ya shahada ya kwanza katika fani za teknolojia, uhandisi, hisabati na tiba.

Halmashauri zatakiwa kuwafikishia vijana taarifa za fursa

Waziri huyo amewaelekeza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na maafisa maendeleo ya vijana kuhakikisha taarifa kuhusu mikopo, mafunzo, ajira, zabuni na fursa nyingine zinawafikia vijana kwa wakati katika kata, vijiji na mitaa.

Amesema, kijana hapaswi kulazimika kusafiri hadi makao makuu ya mkoa ili kupata taarifa za msingi kuhusu namna ya kuomba mkopo, kusajili biashara au kushiriki katika fursa za kiuchumi.

Amezitaka halmashauri kusaidia vijana kubaini miradi inayoweza kutekelezwa kwa kutumia rasilimali na fursa zilizopo katika maeneo yao, huku zikiunganisha uwezeshaji wa kifedha na huduma za ushauri, mafunzo, masoko, viwango vya ubora, usajili wa biashara, kodi, bima na teknolojia.

Akizungumzia Mkoa wa Rukwa amesema, eneo hilo lina fursa katika kilimo, ufugaji, biashara ya mazao, uchakataji, usafirishaji na shughuli zinazohusiana na Ziwa Tanganyika.

Pia, amesema vijana wa mkoa huo wanapaswa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa maeneo yao kwa kuwa wakulima wa kibiashara, wachakataji wa mazao, wafanyabiashara, wasafirishaji na watoa huduma.

Ameonya kuwa, kumpatia kijana mkopo bila kumsaidia katika usimamizi wa biashara na upatikanaji wa masoko kunaweza kupunguza uwezekano wa mradi wake kukua na kuwa endelevu.
Wito kwa vijana kutafuta fursa za kimataifa

Profesa Mkenda amesema, uanachama wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) unafungua fursa za kupanua masoko kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa na vijana.

Amewataka vijana kujifunza kuhusu viwango vya bidhaa, ufungashaji, biashara ya kidijitali, lugha, taratibu za forodha na mahitaji ya masoko ya kikanda ili waweze kushindana katika soko la kimataifa.

Aidha, amesema vijana wanaweza kunufaika na fursa za mafunzo, ubadilishanaji wa uzoefu, ubunifu, ujasiriamali na ajira zinazotolewa na taasisi za kikanda na kimataifa, mashirika ya Umoja wa Mataifa, washirika wa maendeleo na sekta binafsi.

Hata hivyo, amewataka wanaotafuta ajira nje ya nchi kutumia njia rasmi zinazotambuliwa na Serikali, kuelewa mikataba yao na kufahamu haki pamoja na wajibu wao kabla ya kuondoka nchini.

Amesema, hatua hiyo ni muhimu katika kuwalinda vijana dhidi ya unyonyaji na mazingira hatarishi ya ajira.
Vijana wahimizwa kulinda afya na kushiriki katika maendeleo ya Taifa

Katika hotuba hiyo, Profesa Mkenda amesema, maendeleo ya vijana hayawezi kupimwa kwa kipato pekee, bali pia kwa afya njema ya mwili na akili, uwezo wa kufanya maamuzi, stadi za maisha na uwezo wa kukabiliana na changamoto.

Aliwataka vijana kujiepusha na dawa za kulevya, ukatili, uhalifu, matumizi yasiyo na tija ya kamari na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Badala yake, aliwahimiza kutumia teknolojia kwa ajili ya kujifunza, kutafuta masoko, kutangaza bidhaa na huduma zao na kujenga mitandao ya kitaaluma.

Pia alisisitiza umuhimu wa vijana kushiriki katika maamuzi na shughuli za maendeleo kwa kutoa mawazo, kupendekeza suluhisho na kujenga mijadala yenye heshima, huku wakilinda umoja, amani na mshikamano wa Taifa.

Alisema uzalendo unapaswa kuonekana katika kufanya kazi kwa bidii, kulipa kodi, kuheshimu sheria, kupinga rushwa, kulinda mali za umma na kutunza mazingira.
Maazimio ya Wiki ya Vijana yafuatiliwe

Akitoa maelekezo kwa taasisi zinazohusika na maendeleo ya vijana, Profesa Mkenda alitaka Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana kwa kushirikiana na Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji ya Zanzibar kuimarisha uratibu wa taarifa na programu za vijana katika pande zote za Muungano.

Pia alizitaka wizara, taasisi za Serikali na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha mipango na bajeti zao zinaonesha kwa uwazi namna vijana watakavyonufaika na huduma na fursa zinazotolewa.

Amesema, ni muhimu kupima idadi ya vijana wanaofikiwa, aina ya fursa wanazopata na matokeo yanayopatikana badala ya kuishia kutangaza kuwa vijana ni kipaumbele cha Serikali.

Aidha, amezitaka taasisi za fedha na sekta binafsi kubuni huduma zinazokidhi mahitaji ya vijana, ikiwemo mitaji kwa biashara changa, ushauri wa kibiashara, teknolojia na upatikanaji wa masoko.
Waziri huyo amesisitiza kuwa hoja, mapendekezo na maazimio yatakayokusanywa wakati wa Wiki ya Vijana yanapaswa kuwekwa katika mfumo wa ufuatiliaji utakaowezesha utekelezaji na utoaji wa mrejesho baada ya maadhimisho.

Amesema, Wiki ya Vijana haipaswi kuwa tukio linaloishia Oktoba 14, bali iwe mwanzo wa utekelezaji wa hatua zinazopimika kwa ajili ya kuboresha maisha na fursa za vijana.
Vijana wahimizwa kutumia fursa zilizopo

Profesa Mkenda amewataka vijana kujenga ujuzi, kujifunza kusimamia fedha, kutumia taarifa rasmi na kuimarisha ushirikiano katika kuanzisha na kukuza biashara.

Amesema, vijana wanapaswa kuanza kutumia rasilimali walizonazo, bila kudharau kazi halali, huku wakizingatia ubora, nidhamu na uadilifu katika shughuli zao.

Amesisitiza kuwa, mafanikio endelevu hayawezi kupatikana kwa kutafuta njia za mkato, bali kwa kufanya kazi kwa maarifa, uvumilivu na kujituma.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kila kijana anapaswa kutambua tatizo analoweza kutatua katika jamii yake, thamani anayeweza kuongeza katika shughuli za uzalishaji na ujuzi anaopaswa kujifunza ili kuunda ajira kwa ajili yake na watu wengine.

Wakati huo huo, amewapongeza viongozi na wananchi wa Mkoa wa Rukwa kwa kuwa wenyeji wa Wiki ya Vijana Kitaifa 2026, huku akiwashukuru wadau wote walioshiriki katika maandalizi ya maadhimisho hayo.

Amesema, Serikali ina imani na uwezo wa vijana wa Tanzania katika kubuni, kuzalisha, kuongoza na kulinda tunu za Taifa, na itaendelea kushirikiana nao kujenga mazingira yatakayohakikisha tofauti za kijiografia na kijamii hazizuii upatikanaji wa fursa.

Wiki ya Vijana Kitaifa huadhimishwa kila mwaka kuanzia Oktoba 8 hadi 14, ikiwa ni jukwaa la kuhamasisha uzalendo, kujitolea, uwajibikaji na ushiriki wa vijana katika maendeleo ya Taifa.
Maadhimisho ya mwaka huu yanatarajiwa kutoa nafasi kwa vijana kushiriki katika maonesho, kongamano, huduma za afya, shughuli za kujitolea, mafunzo na majadiliano yatakayowaunganisha na taarifa, ujuzi na fursa mbalimbali za maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here