Waziri wa Fedha akutana na CEO wa Kituo cha Fedha cha Qatar, wajadili mikakati ya kuanzisha kituo Tanzania

DOHA-Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kituo cha Fedha cha Qatar (Qatar Financial Centre-QFC), Bw. Mansoor Rashid Al-Khater, pembezoni mwa Mkutano wa 11 wa Mwaka 2026 wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Miundombinu ya Asia (AIIB) uliofanyika jijini Doha nchini Qatar.
Mkutano huo uliofanyika Makao Makuu ya Kituo hicho, eneo la Lusail ulilenga kumwezesha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Omar na ujumbe wake, kubadilishana maarifa namna kituo hicho kinavyofanyakazi kuelekea mpango wa Serikali wa kuwa na kituo kama hicho jijini Dar es Salaam kwa siku za usoni.

Mtendaji Mkuu wa QFC, Bw. Mansoor Rashid Al-Khater alisema kuwa, kituo hicho ni cha biashara na fedha kilichopo Doha, ambacho kilianzishwa Machi mwaka 2005 ambacho ni "onshore" financial centre yaani si eneo maalum la kigeni (free zone), bali kinatoa huduma za kisheria na udhibiti kwa kampuni za ndani na za kimataifa ndani ya mfumo wa kisheria wa Qatar yenyewe.
Alisema kuwa, lengo lake kuu ni kusaidia sera za kiuchumi za serikali ya Qatar na mipango ya kuondoa utegemezi wa mapato ya mafuta, kwa kuvutia uwekezaji kupitia mazingira rafiki ya kisheria, udhibiti, kodi na biashara.

“Kazi zake ni kuandikisha na kutoa leseni kwa kampuni za fedha, biashara na huduma za kitaalamu,” alisema Bw. Al-Khater.
Aliongeza kuwa, QFC ina mamlaka yake ya udhibiti, Qatar Financial Centre Regulatory Authority (QFCRA) na mfumo wake wa mahakama, Qatar International Court and Dispute Resolution Centre na kwamba QFC ni njia ya watoa huduma za fedha kufikia soko la Qatar, ambalo lina miradi ya miundombinu yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 200, na pia uwekezaji wa karibu dola trilioni 1 katika eneo lote.

Sekta lengwa ni huduma za kidijitali (technology & innovation), vyombo vya habari na burudani, michezo, na huduma za fedha pamoja na utajiri (wealth) na fintech kama sekta ndogo zinazokua.

Takwimu za hivi karibuni (mwishoni mwa Juni 2026), zinaonesha kuwa QFC imesajili Kampuni zaidi ya 4,700.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Omar aliushukuru uongozi wa Kituo hicho na kuahidi kujenga ushirikiano wa Kimkakati na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha ili kutumia uzoefu wake katika kusimamia masuala ya kuendeleza uchumi wa nchi na kuiwezesha Tanzania kimbinu na kiutaalam ili iweze kufikia azma yake ya kuwa na Kituo mahiri kama hicho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here