Wizara: Kuchepusha maji faini Shilingi milioni 50, jela miaka 5

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI wa Huduma za Sheria katika Wizara ya Maji, Wakili Simon Nkanyemka amewatahadharisha wananchi dhidi ya kuchepusha maji au kujiunganishia huduma ya maji kinyemela, akieleza kuwa vitendo hivyo ni makosa ya jinai yanayoweza kusababisha adhabu ya faini ya hadi Shilingi milioni 50 au kifungo cha hadi miaka mitano jela.
Kuchepusha maji kwa manufaa yako kutakugharimu kiuchumi na kustawi. (Picha na DIRAMAKINI).

Wakili Nkanyemka amesema, Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya mwaka 2019 imeweka masharti yanayolenga kulinda miundombinu ya maji na kuhakikisha huduma hiyo inatolewa na kutumika kwa kuzingatia sheria.

Ameeleza kuwa, kifungu cha 62 cha sheria hiyo kinahusu makosa ya kuchukua au kuchepusha maji kutoka katika miundombinu ya maji bila kufuata taratibu za kisheria, ikiwemo kujiunganishia huduma ya maji bila idhini ya mamlaka husika.

Kwa mujibu wa Nkanyemka, mtu atakayepatikana na hatia ya kutenda kosa hilo anakabiliwa na faini isiyopungua Shilingi 500,000 na isiyozidi Shilingi milioni 50, au kifungo cha muda usiopungua miezi 12 na kisichozidi miaka mitano, au adhabu zote mbili kwa pamoja.

Aidha, amesema pamoja na adhabu hizo, mtu atakayetiwa hatiani anawajibika kulipa gharama za kurekebisha uharibifu na kufidia hasara iliyosababishwa na kitendo hicho cha ukiukaji wa sheria.

Wakili huyo amesisitiza kuwa, wananchi wanapaswa kuzingatia taratibu zinazowekwa na mamlaka za huduma za maji wanapohitaji kuunganishiwa huduma hiyo, badala ya kujichukulia hatua za kujiunganishia au kuchepusha maji bila kufuata utaratibu unaotakiwa.

Vitendo vya kuchepusha maji na kujiunganishia huduma kinyume cha sheria vinaweza kuathiri miundombinu ya usambazaji, kuongeza gharama za matengenezo na kuathiri upatikanaji wa huduma kwa watumiaji wengine.

Hivyo, wananchi wanahimizwa kutumia njia halali kupata huduma za maji na kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini vitendo vinavyoweza kuhatarisha miundombinu hiyo.

Vilevile, uzingatiaji wa sheria na ushirikiano kati ya wananchi na mamlaka za maji ni muhimu katika kulinda miundombinu iliyopo, kupunguza upotevu wa maji na kuimarisha upatikanaji wa huduma endelevu kwa jamii.
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria katika Wizara ya Maji, Wakili Simon Nkanyemka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here