AG Johari ataja manufaa ya kliniki za sheria katika utekelezaji wa Dira 2050

Na Mwandishi Wetu| Arusha

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amesema kuwa, uzinduzi wa Kliniki za Sheria zinazoendeshwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mikoa mbalimbali nchini, ni moja ya nguzo muhimu katika kuipa uhai Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga taifa lenye haki, ustawi na linalojitegemea.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya na Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananachi wa Mkoa wa Arusha leo Novemba 24, 2026 jijini Arusha.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa, kuzinduliwa kwa Kliniki za Sheria ni mwendelezo wa mkakati thabiti wa Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasogezea wananchi huduma za kisheria karibu kabisa na maeneo yao.
"Hadi sasa, Kamati hizi zimekwisha zinduliwa katika mikoa tisa (Dodoma, Kilimanjaro, Mwanza, Singida, Manyara, Simiyu, Dar es Salaam, Tanga, na Katavi) na zimefanikiwa kusikiliza na kutatua kero za wananchi 11,715," amesema Mhe.Johari.

Aidha, Mhe. Johari amesema kuwa Lengo kuu la kuzinduliwa kwa Kamati za Ushauri wa Kisheria ni kupunguza malalamiko na madai yasiyo ya lazima dhidi ya Serikali, sambamba na kurahisisha usimamizi mzuri wa utoaji wa ushauri kwa viongozi na wananchi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewataka, wananchi wa Mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi kuwasilisha changamoto zao mbalimbali za kisheria ili ziweze kutatuliwa katika Kliniki hiyo.

"Nitumie fursa hii kuwasihi wananchi wa Arusha kujitokeza kwa wingi na kuzitumia kamati na kliniki hizi kuwasilisha changamoto zao za kisheria ili zipatiwe suluhisho la kudumu," amesema Mhe. Johari.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Arusha, Bw. Nsajigwa Mwamnyange ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuzindua Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Arusha kwa kuwa itasaidia kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili wananchi.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria Mkoa wa Arusha, Bi. Veritas Mlay amesema kuwa, Kamati za Ushauri wa Kisheria ngazi ya Mkoa na Wilaya zimeanzishwa kwa lengo la kutoa ushauri wa kisheria kwa wananchi, watumishi na viongozi wa Umma kwa ujumla ili kutatua changamoto za kisheria katika Wilaya na Mikoa.

Hafla ya uzinduzi wa Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Taasisi za Kisheria akiwemo, Mwandishi Mkuu wa Sheria, Bw. Onorius Njole, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Bw. George Mandepo, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Dunford Mpelumbe na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mturo.
Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Arusha iliyozinduliwa tarehe 24 Novemba, 2026 itaendelea hadi tarehe 29 Novemba, 2026 kwa wananchi kupata huduma mbalimbali za kisheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here