BoT yaanza kuwasimamia watoa huduma ndogo za fedha (wasiopokea amana) Zanzibar

Na DIRAMAKINI 24| Dar es Salaam

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeanza rasmi kutekeleza jukumu la kusimamia na kufuatilia watoa huduma ndogo za fedha Zanzibar kwa mujibu wa vifungu vya 15 na 16 vya Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha Zanzibar Na. 9 ya Mwaka 2023.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba.

Sheria hiyo iliyoidhinishwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), ilianza rasmi kutumika mwaka 2025 kufuatia kutangazwa na Waziri wa Fedha Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Huduma Ndogo za Fedha Zanzibar ya Mwaka 2019.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 20, 2026 na Gavana wa BoT, Be. Emmanuel M. Tutuba.

"Ili kutekeleza Sheria hiyo kwa ufanisi, Wizara ya Fedha Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Fedha iliandaa Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha (Wasiopokea Amana - Daraja la Pili) ya Mwaka 2025.

"Kanuni hizi zimeweka utaratibu na vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika utoaji wa leseni, mitaji pamoja na masuala ya utawala wa taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha.

"Hivyo, watoa huduma ndogo za fedha (wasiopokea amana - Daraja la Pili) wanaotoa au wanaotarajia kutoa huduma hizo Zanzibar wanatakiwa kuwasilisha maombi ya leseni Benki Kuu ya Tanzania - Zanzibar kuanzia tarehe ya tangazo hili."

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwa wale ambao wanaendelea kutoa huduma, mwisho wa kuwasilisha maombi hayo ni tarehe 31 Disemba, 2026.

"Umma unakumbushwa kuwa, ni kosa kisheria kwa mtu au taasisi yoyote kufanya biashara ya kutoa huduma ndogo za fedha bila kuwa na leseni ya BoT au Mamlaka iliyokasimiwa, kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha Zanzibar Namba 9 ya Mwaka 2023."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here