BoT yadhamini mikopo ya Shilingi trilioni 2.1 kwa wafanyabiashara

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imefanikiwa kutoa dhamana za mikopo zenye thamani ya Shilingi trilioni 1.6 zilizowezesha upatikanaji wa mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni 2.1 kwa wafanyabiashara na wajasiriamali katika sekta mbalimbali za uchumi nchini.
Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Fedha wa BoT, Bi. Gloria Chellunga ameyasema hayo leo Novemba 5, 2026 wakati akiwasilisha mada kuhusu jinsi Mfumo wa Dhamana ya Mikopo unavyofanya kazi na wigo wake wa kisheria, katika semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia mifuko ya dhamana ya mikopo inayosimamiwa na Benki Kuu, kwa lengo la kuwasaidia wajasiriamali na wafanyabiashara wenye miradi yenye tija lakini wanaokabiliwa na changamoto ya kutokuwa na dhamana ya kutosha kukidhi masharti ya taasisi za fedha.

Amesema, Serikali imeanzisha mifuko miwili ya dhamana ya mikopo inayosimamiwa na BoT kwa lengo la kuwasaidia wajasiriamali wenye miradi yenye tija ambao wanakosa mikopo kutokana na upungufu wa dhamana.

Mifuko hiyo ni Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa Mauzo ya Nje (Export Credit Guarantee Scheme - ECGS), ulioanzishwa Julai 2002, na Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (Small and Medium Enterprises Credit Guarantee Scheme - SMECGS), ulioanzishwa Septemba 2005.

Bi. Chellunga amesema, maombi ya dhamana huwasilishwa na benki au taasisi ya fedha inayokusudia kumkopesha mteja, baada ya kubaini kuwa anakidhi vigezo vya mkopo lakini ana upungufu wa dhamana.

Amesema, katika utaratibu huo, taasisi ya fedha huwasilisha barua rasmi Benki Kuu ikieleza taarifa za mteja, kiasi cha mkopo anaohitaji na kiwango cha upungufu wa dhamana, huku ikiomba taasisi hiyo idhamini sehemu ya mkopo husika.

Mtaalamu huyo amefafanua kuwa, baada ya kupokea maombi hayo, Benki Kuu hufanya tathmini ya kina ili kujiridhisha kuwa mradi unaoombewa mkopo una uwezo wa kuzalisha mapato na kurejesha fedha zitakazokopwa.

Aidha, amesema tathmini hiyo huhusisha kuhakiki iwapo mradi unakidhi vigezo na masharti yaliyowekwa, pamoja na kuhakikisha benki husika imefuata miongozo na taratibu zote za ukopeshaji kabla ya kuomba dhamana.
"Baada ya kujiridhisha kuwa mradi unalipika na masharti yote yametimizwa, Benki Kuu hutoa idhini kwa benki husika kuendelea na utoaji wa mkopo kwa mteja wake,” ameeleza.

Bi. Chellunga amesema, baada ya idhini hiyo, benki inayokopesha huingia mkataba na Benki Kuu kuhusu masharti ya dhamana, huku ikiendelea kuwajibika kuhakikisha mkopo unarejeshwa kwa kufuata taratibu za kawaida za ukopeshaji.

Amesema, uwepo wa dhamana ya Benki Kuu haupaswi kumfanya mkopaji au taasisi ya fedha kulegeza masharti ya urejeshaji, kwa kuwa mkopo huo unapaswa kusimamiwa kwa umakini kama mikopo mingine.

Vilevile, ameongeza kuwa, miongoni mwa masharti ya kimkataba kwa benki zinazotumia utaratibu huo ni kulipa ada ya uwezeshaji wa mikopo ya asilimia moja ya kiasi cha fedha kinachodhaminiwa.

Akifafanua falsafa ya uendeshaji wa mifuko hiyo, amesema mfumo huo unazingatia dhana ya kugawana vihatarishi (Risk Sharing), ambapo mkopaji, benki inayotoa mkopo na Benki Kuu inayosimamia dhamana kwa niaba ya Serikali kila mmoja ana wajibu wake katika kuhakikisha mkopo unatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejeshwa kwa wakati.

Sekta mbalimbali zanufaika

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kupitia mifuko hiyo, Bi. Chelunga amesema, dhamana zilizotolewa zimewezesha upatikanaji wa mikopo katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, ujenzi, elimu, mawasiliano, afya, kilimo, utalii, uchimbaji madini na usafirishaji.
Hata hivyo, amesema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto ya ushiriki mdogo wa biashara ndogo na za kati katika kunufaika na mifuko ya dhamana, licha ya kuwa kundi hilo ndilo lililolengwa kwa kiasi kikubwa.

Amesema, moja ya vikwazo vinavyochangia hali hiyo ni uwepo wa biashara nyingi zisizosajiliwa rasmi, jambo linalozifanya zishindwe kutimiza masharti ya kisheria na kiutawala yanayohitajika ili kupata huduma za dhamana kupitia mifuko hiyo.

Ameeleza kuwa, urasimishaji wa biashara ni muhimu kwa kuwawezesha wajasiriamali kupata fursa za mikopo na huduma nyingine za kifedha zinazotolewa na taasisi zilizosajiliwa.

Wanawake na vijana wakabiliwa na upungufu wa dhamana

Katika hatua nyingine, Bi. Chellunga amesema, biashara nyingi ndogo na za kati, hususan zinazomilikiwa na wanawake na vijana, zinakabiliwa na upungufu wa mali zinazokubalika na benki kama dhamana ya mikopo.

Amesema, hali hiyo inakuwa changamoto zaidi pale ambapo mfuko wa dhamana unaweza kugharamia asilimia 50 ya mkopo, lakini mjasiriamali anakosa uwezo wa kutoa sehemu iliyobaki inayotakiwa kukidhi masharti ya taasisi ya fedha.

Amefafanua kuwa, hali hiyo inaonesha kuwa pamoja na uwepo wa mifuko ya dhamana, bado kuna pengo linalohitaji kushughulikiwa ili kuwafikia wafanyabiashara wadogo ambao hawana uwezo wa kumiliki mali zenye thamani kubwa zinazoweza kutumika kama dhamana.
Amesisitiza, umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya uwezeshaji wa biashara ndogo na za kati ili kuhakikisha wajasiriamali wengi zaidi wakiwemo wanawake na vijana, wanapata fursa ya kutumia huduma za kifedha kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here