BoT yahimiza matumizi sahihi ya Noti za fedha kuepusha gharama za ziada

NA GODFREY NNKO

WANANCHI wameonywa dhidi ya tabia ya kuharibu kwa makusudi sarafu (noti) za Tanzania huku wakikumbushwa umuhimu wa kuzitunza kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa ili kupunguza gharama za uchapishaji na uingizwaji wa fedha mpya.
Afisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoka Kurugenzi ya Sarafu, Bw. Shadrack Mapunda.

Onyo hilo limetolewa na Afisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoka Kurugenzi ya Sarafu, Bw. Shadrack Mapunda leo Novemba 6, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada kuhusu utambuzi wa alama za usalama katika noti na utunzaji bora wa fedha katika semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari za uchumi na masoko ya fedha.

Bw. Mapunda amesema kuwa, utunzaji usiofaa wa noti unaofanywa na baadhi ya wananchi unasababisha fedha hizo kuharibika kabla ya kufikia muda wake wa kawaida wa matumizi, hali inayolazimisha Benki Kuu kuzibadilisha mapema na kuongeza gharama za uchapishaji.

Ameeleza kuwa, tabia ya kukunja noti, kuzibana kwa pini, kuziweka katika mazingira yasiyofaa na kutozihifadhi kwa uangalifu inachangia kuharibika kwa fedha hizo, ambazo zinatarajiwa kudumu kwa takribani mwaka mmoja na nusu.

Pia, amesema gharama zinazotumika kuchapisha noti mpya kutokana na uharibifu unaosababishwa na utunzaji mbaya zingeweza kuelekezwa katika shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara na miundombinu.
Akizungumzia taratibu za kubadilisha noti zilizochakaa au kuharibika, Bw. Mapunda amesema, si kila noti iliyoharibika inastahili kubadilishwa, kwani kuna vigezo maalumu vinavyopaswa kuzingatiwa.

Amesema, miongoni mwa vigezo hivyo ni noti husika kuwa halali na kubaki na angalau asilimia 75 ya ukubwa wake wa awali, huku pande zote mbili za noti yaani mbele na nyuma, zikionekana na kuwezesha kutambulika kwa taarifa na alama zake muhimu.

Bw. Mapunda ameongeza kuwa, noti zilizoharibika kwa kiwango kikubwa, zikiwemo zilizoliwa, kuungua au kufutika kwa alama muhimu za utambuzi zinaweza kushindwa kukidhi vigezo vya kubadilishwa na hivyo kusababisha hasara kwa mmiliki wake.

Katika hatua nyingine, Bw. Mapunda amewataka wananchi kuongeza umakini wanapopokea fedha ili kujiepusha na noti bandia, akieleza kuwa ukosefu wa elimu ya msingi kuhusu namna ya kuthibitisha uhalali wa fedha ni miongoni mwa sababu zinazochangia baadhi ya watu kupokea noti bandia bila kugundua.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kujifunza alama za usalama zilizowekwa kwenye noti, ikiwemo alama ya taswira fiche (watermark) na vipengele vingine vya kiusalama vinavyosaidia kutofautisha fedha halali na bandia.

Akitoa mfano wa tukio lililotokea mkoani Njombe mwaka jana, Bw. Mapunda ameeleza kuwa, mfanyabiashara wa parachichi alipokea kiasi kikubwa cha fedha bandia katika malipo ya biashara yake, hali inayoonesha umuhimu wa kukagua fedha kabla ya kukamilisha miamala, hususan ile yenye thamani kubwa.

Kuhusu hatua za kisheria dhidi ya watu wanaojihusisha na kughushi fedha, Mapunda amesema Kifungu cha 338 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16, kinaweka adhabu ya kifungo cha maisha kwa mtu anayepatikana na hatia ya kughushi nyaraka mbalimbali, zikiwemo noti za benki na noti za fedha.
Ameongeza kuwa, kifungu hicho kinaipa mahakama mamlaka ya kuamuru nyaraka zilizoghushiwa kutaifishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Bw. Mapunda amesisitiza kuwa, utunzaji bora wa fedha na uelewa wa alama za usalama ni wajibu wa kila mwananchi, akieleza kuwa hatua hizo zitasaidia kupunguza uharibifu wa noti, gharama za uchapishaji wa fedha mpya na hatari ya kuingia katika miamala inayohusisha fedha bandia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here