BoT yajivunia ushirikiano na waandishi wa habari kuelimisha umma masuala ya Uchumi na Fedha

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na waandishi wa habari nchini kupitia semina za mafunzo zinazolenga kuongeza uelewa kuhusu masuala ya uchumi na fedha, ili kuwezesha wananchi kupata taarifa sahihi na zenye ufafanuzi wa kutosha kuhusu shughuli za taasisi hiyo.
Meneja Mawasiliano wa benki hiyo, Bi. Victoria Msina ameyasema hayo leo Novemba 4, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akimkaribsha mgeni rasmi Naibu Gavana wa BoT anayeshughulikia Utawala na Udhibiti wa Ndani, Dkt. Rahma Salim Mahfoudh kufungua semina ya siku tatu ya Waandishi wa Habari za Uchumi na Fedha kwa mwaka 2026.

Bi. Msina amesema, mpango huo umekuwa ukitekelezwa kwa takribani miaka 15 ukiwa na lengo la kujenga uhusiano wa karibu kati ya Benki Kuu na wadau wa tasnia ya habari kote nchini.

Amesema, semina hizo zimekuwa zikifanyika katika kanda mbalimbali za nchi, ambapo kwa utaratibu wa kila mwaka, BoT huandaa mafunzo mara mbili ya aina hiyo ili kuwafikia waandishi wengi zaidi, wakiwemo wanaofanya kazi katika vyombo vya habari vya kitaifa na vile vya kijamii.

Vilevile, ameeleza kuwa, semina ya Dar es Salaam imefuatia mafunzo mengine yaliyofanyika mwezi Mei, mwaka huu mkoani Kigoma, hatua inayodhihirisha juhudi za benki hiyo kupanua wigo wa ushirikiano na waandishi wa habari katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Bi. Msina amesema, waandishi wa habari wana nafasi muhimu katika kuunganisha taasisi na wananchi kwa kuwa ndio wanaowezesha taarifa, sera na maelezo ya kitaalamu kuwafikia watu kupitia machapisho, matangazo ya redio, televisheni na majukwaa mengine ya habari.

Amesisitiza kuwa, licha ya BoT kutekeleza majukumu yake na kutoa taarifa mbalimbali, ujumbe huo hauwezi kuwafikia wananchi kwa ufanisi bila mchango wa vyombo vya habari, ambavyo vina jukumu la kuuchambua na kuuwasilisha kwa lugha inayoeleweka kwa jamii.

Meneja Mawasiliano huyo amesema, kujenga ukaribu na waandishi kunawapa nafasi ya kuwasiliana kwa uhuru na wataalamu wa benki hiyo, kuuliza maswali, kutafuta ufafanuzi na kupata taarifa sahihi wanapokutana na masuala yanayohitaji maelezo ya ziada.

Akifafanua kuhusu maudhui ya mafunzo hayo, Bi. Msina amesema, washiriki wanapata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu uchumi na sera za fedha yakiwemo mfumuko wa bei na viwango vya riba vya Benki Kuu, ambayo wakati mwingine hutumia istilahi za kitaalamu zinazoweza kuwa changamoto kwa baadhi ya waandishi.
Pia, amesema mafunzo hayo yanawajengea uwezo wa kuelewa dhana hizo, kuzifafanua kwa usahihi na kuziwasilisha kwa wananchi kwa lugha nyepesi bila kupoteza maana ya kitaalamu.

Aidha, ameeleza kuwa ushirikiano huo unaiwezesha BoT kuwa na mtandao mpana wa waandishi wa habari ambao inaweza kuutumia kufikisha taarifa muhimu kwa umma, kutoa ufafanuzi wa masuala yanayojitokeza na kushirikisha wataalamu wake pale panapohitajika maelezo ya kina.

Amebainisha kuwa, kwa kipindi chote cha miaka 15, benki hiyo imeendelea kupanua kanzidata ya waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali nchini, jambo linalorahisisha mawasiliano na uratibu wa utoaji wa taarifa kwa wakati.

Bi. Msina amesema, juhudi hizo hazilengi vyombo vikubwa vya habari vilivyojikita katika miji kama Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar pekee, bali pia redio za jamii, televisheni na vyombo vingine vinavyohudumia wananchi katika mikoa na maeneo ya vijijini.

Amesema, umuhimu wa kuwafikia waandishi wa habari wa jamii unatokana na ukweli kwamba wananchi katika baadhi ya maeneo hupendelea kupata taarifa kupitia lugha wanazozielewa zaidi, zikiwemo lugha za asili.
Hivyo, kushirikisha vyombo vya habari vilivyo karibu na jamii kunasaidia kuhakikisha ujumbe wa Benki Kuu unawafikia wananchi wengi zaidi.

Ameongeza kuwa, BoT itaendelea kuendesha semina hizo katika maeneo mbalimbali ili kupanua uelewa wa waandishi, kuimarisha mahusiano ya kikazi na kuhakikisha taarifa kuhusu uchumi na fedha zinawasilishwa kwa usahihi, uwazi na kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here