NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeeleza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa waandishi wa habari katika kuandika na kuchambua masuala ya uchumi na fedha ili kuongeza usahihi wa taarifa zinazowafikia wananchi na kuwajengea uelewa kuhusu shughuli za taasisi za kifedha nchini.
Hatua hiyo inalenga pia kuimarisha ushirikiano kati ya benki hiyo na vyombo vya habari, kwa kutambua nafasi ya wanahabari katika kuunganisha taasisi na wananchi kupitia utoaji wa taarifa sahihi, zenye ubora na zinazozingatia weledi wa kitaaluma.
Naibu Gavana wa BoT anayeshughulikia Utawala na Udhibiti wa Ndani, Dkt. Rahma Salim Mahfoudh amesema hayo leo Novemba 4, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina ya siku tatu ya Waandishi wa Habari za Uchumi na Fedha kwa mwaka 2026.
Amesema, BoT imekuwa na utaratibu wa kuandaa mafunzo hayo kwa takribani miaka 15 ili kuongeza uelewa wa wanahabari kuhusu majukumu yake na mwenendo wa sekta ya uchumi na fedha.
Pia, amesema semina hiyo imewakutanisha waandishi kutoka Dar es Salaam, Zanzibar, Dodoma, Pwani na Morogoro ikiwa ni sehemu ya mpango wa kitaifa unaotekelezwa sambamba na mafunzo mengine yanayoandaliwa katika kanda mbalimbali nchini.
Naibu Gavana Dkt. Mahfoudh amesema, mafunzo hayo yana malengo kadhaa, yakiwemo kuwawezesha waandishi kuelewa kwa kina majukumu na shughuli za Benki Kuu, kufuatilia mabadiliko na ubunifu unaojitokeza katika sekta ya fedha.
Sambamba na kuongeza uwezo wa kuandaa habari na makala zinazohusu masuala ya kiuchumi kwa usahihi.
Amesema, pia mpango huo unalenga kujenga mtandao wa waandishi waliobobea katika masuala ya uchumi na fedha, hatua itakayosaidia kukuza utaalamu katika tasnia ya habari na kuongeza ubora wa taarifa zinazotolewa kwa umma.
Naibu Gavana huyo ameeleza kuwa, mafunzo hayo yanawawezesha wanahabari kupata ujuzi wa kuchambua na kutumia takwimu kutoka katika ripoti na machapisho mbalimbali ya BoT, zikiwemo taarifa za kila wiki, robo mwaka na mwaka ili kubaini habari zenye umuhimu kwa jamii.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana kutokana na semina zilizotangulia, Dkt. Mahfoudh amesema, kumekuwa na ongezeko la uelewa na usahihi katika uandishi wa habari zinazohusu Benki Kuu, hususan katika maeneo yanayohitaji ufafanuzi wa kitaalamu kuhusu uchumi na huduma za kifedha.
Vilevile ameongeza kuwa, mafunzo hayo yameimarisha mawasiliano kati ya waandishi na wataalamu wa benki hiyo, ambapo wanahabari wamekuwa wakipata nafasi ya kuwasilisha maswali na kuthibitisha taarifa kabla ya kuzichapisha au kuzitangaza.
Amesema, ushirikiano huo umechangia pia kukuza uwezo wa kuandika makala za uchambuzi wa kiuchumi na kuwasaidia wananchi kupata taarifa zinazotegemewa, badala ya kutegemea maelezo yasiyo na uthibitisho wa kitaalamu.
Dkt. Mahfoudh amesisitiza kuwa, BoT inathamini mchango wa vyombo vya habari kwa kuwa ni daraja muhimu la kuwasilisha taarifa za taasisi hiyo kwa wananchi, wakiwemo wakazi wa maeneo ya vijijini ambao wanahitaji elimu kuhusu masuala ya fedha, uchumi na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.
Katika semina hiyo ya siku tatu, BoT imeandaa wataalamu wabobezi ili kutoa mada mbalimbali zinazohusiana na usimamizi wa uchumi na sekta ya fedha nchini.
Miongoni mwa mada zinazojadiliwa ni utekelezaji wa Sera ya Fedha kwa Kutumia Riba ya Benki Kuu, Kielelezo cha Faida Rejea ya Dhamana za Serikali na Mchango Wake katika Kuimarisha Uwazi wa Masoko ya Fedha, na Namna BoT inavyosimamia mifumo ya malipo nchini.
Mada nyingine ni Jinsi Benki Kuu ya Tanzania Inavyosimamia Sekta ya Fedha, Jinsi Mfumo wa Dhamana ya Mikopo Unavyofanya Kazi na Wigo Wake wa Kisheria, na Utambuzi wa alama za usalama katika noti na utunzaji bora wa noti.
Pia, kuna mada ya Jinsi Benki Kuu Inavyotumia Mfumo wa SEMA NA BoT katika Kulinda Watumiaji wa Huduma za Fedha, na Jinsi ya Kubaini na Kuandaa Habari Zinazotumia Takwimu kutoka katika Ripoti na Taarifa za Benki Kuu ya Tanzania ikiwemo Maoni na ushauri kwa Benki Kuu.
Naibu Gavana huyo amewataka waandishi kutumia fursa hiyo kushiriki kikamilifu, kufuatilia mada zinazowasilishwa na kuuliza maswali pale wanapohitaji ufafanuzi, akieleza kuwa uelewa wa kina ndio msingi wa kuwasilisha taarifa sahihi kwa jamii.
Amesema, BoT inatarajia kuona maboresho zaidi kuhusu namna waandishi wanavyochambua na kuwasilisha taarifa za uchumi na fedha baada ya mafunzo hayo, huku ikiahidi BoT kuendelea kuandaa semina kama hizo katika maeneo mbalimbali nchini.
Mbali na kuwajengea uwezo wa kitaaluma, semina hiyo inatoa fursa kwa waandishi hao kupata taarifa na maarifa yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Sambamba na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu nafasi, majukumu na mchango wa Benki Kuu katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
Tags
Benki Juu ya Tanzania
BoT
Dar es Salaam
Dkt. Rahma Salim Mahfoudh
Habari
Semina ya BoT
Uchumi na Fedha
Waandishi wa Habari


