DAR ES SALAAM- Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wafanyabiashara wa Kariakoo kutumia mifumo ya malipo ya kidijitali katika shughuli zao za biashara ili kuongeza usalama wa miamala, kurahisisha upokeaji wa malipo na kuongeza ufanisi wa biashara zao.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo ya Taifa wa Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Lucy Shaidi, wakati akifungua mkutano wa uelimishaji kuhusu mifumo ya malipo uliohusisha viongozi na wafanyabiashara wa Kariakoo, uliofanyika katika Ofisi za Benki Kuu, Makao Makuu Ndogo ya Dar es Salaam, Novemba 11, 2026.
Amesema mkutano huo umeandaliwa kwa lengo la kuwajengea wafanyabiashara uelewa kuhusu mifumo mbalimbali ya malipo, matumizi yake salama na faida zake katika shughuli za kila siku za biashara.
Aidha, mkutano huo umeiwezesha Benki Kuu kupata fursa ya kusikiliza maoni na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara katika matumizi ya mifumo hiyo inayojumuisha malipo kwa kutumia kadi za benki na mashine za POS, simu za kiganjani, benki mtandao, Lipa Namba, msimbomilia (TANQR), hundi pamoja na uhamishaji wa fedha kutoka benki moja kwenda nyingine.
Akitoa wasilisho kuhusu faida za mifumo ya malipo ya kidijitali, Meneja Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya Benki Kuu, Bw. Fabian Kasole amesema, mifumo hiyo inawezesha kuongeza usalama wa fedha kwa kupunguza hatari ya wizi na matumizi ya noti bandia.
Vilevile, kutunza kumbukumbu za miamala, kurahisisha upatikanaji wa mikopo kupitia kumbukumbu za biashara, pamoja na kuongeza kasi na urahisi wa kupokea malipo.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa Kariakoo, Kaimu Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Bw. Donald Kibuna, amesema matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali yamewasaidia kuokoa muda na kurahisisha miamala ya fedha kwa kuwawezesha kufanya malipo papo hapo bila kulazimika kwenda benki.

Amesema, hali hiyo imewawezesha kuendelea na shughuli zao za biashara kwa ufanisi zaidi.
Aidha, wafanyabiashara hao wameishukuru Benki Kuu kwa kuandaa mkutano huo na kupongeza juhudi zake katika kuimarisha huduma za malipo nchini.
Uhamasishaji wa matumizi ya malipo ya kidijitali ni sehemu ya juhudi za Benki Kuu katika kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi imara, wa kisasa na wa kipato cha juu, ambapo teknolojia na uchumi wa kidijitali ni miongoni mwa nguzo muhimu za maendeleo.
Benki Kuu itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo wafanyabiashara, kusikiliza maoni yao na kufanyia kazi changamoto zinazojitokeza katika matumizi ya mifumo ya malipo ili kuimarisha mazingira ya kufanya biashara kwa usalama, urahisi na ufanisi zaidi.


