Na DIRAMAKINI 24| Dar Es Salaam
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeibuka mshindi wa kwanza katika kundi la Taasisi za Serikali Zinazojitegemea na kutunukiwa Tuzo ya Umahiri wa Uandaaji Bora wa Taarifa za Hesabu kwa mwaka wa fedha 2024/2025.


Tuzo hiyo iliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), inalenga kutambua taasisi zinazofanya vizuri katika uandaaji wa taarifa za hesabu kwa kuzingatia Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (IPSAS).
Ushindi huu ni wa mara ya tisa kwa DCEA kupata tuzo za NBAA tangu mwaka 2017ukiakisi dhamira endelevu ya Mamlaka katika kuzingatia viwango na miongozo ya kitaaluma katika usimamizi wa fedha za umma.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema, ushindi huo ni ishara ya kutambuliwa kwa weledi, uwajibikaji na ubora katika usimamizi wa fedha za umma.
Pia, amesema tuzo hiyo inaonesha dhamira ya mamlaka kuhakikisha rasilimali inazopatiwa zinatumika kwa uadilifu, uwazi na ufanisi ili kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yake, ikiwamo kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini.
Kamishna Jenerali Lyimo ameeleza kuwa, mafanikio hayo yametokana na ushirikiano na kujituma kwa watumishi wa mamlaka, akivitaja Kitengo cha Fedha na Uhasibu pamoja na Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kuwa miongoni mwa vitengo vilivyochangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha ushindi huo.
Aidha, ametoa shukrani kwa NBAA kwa kutambua juhudi za DCEA katika kuimarisha mifumo ya uandaaji wa taarifa za hesabu kwa kuzingatia viwango vya kimataifa, akisisitiza kuwa tuzo hiyo ni chachu ya kuendelea kuboresha utendaji na usimamizi wa rasilimali za umma.
Amesema, mamlaka itaendelea kuzingatia viwango vya kimataifa katika uandaaji wa taarifa za hesabu, kuimarisha uwazi na uwajibikaji, pamoja na kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Vilevile, ameongeza kuwa, DCEA itaendeleza weledi katika maeneo yote ya utendaji wake, hususan usimamizi wa fedha na utekelezaji wa operesheni za kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, ili kuhakikisha inatimiza wajibu wake kwa ufanisi.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema, mafanikio hayo yanaimarisha dhamira ya mamlaka ya kuendelea kutoa huduma kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, matumizi bora ya fedha na viwango vinavyokubalika kimataifa.