Dkt. Mwigulu aagiza ujenzi wa kituo kipya cha afya Ngerengere uanze

✓Aelekeza ujenzi wa daraja la Tununguo uingizwe kwenye bajeti ijayo

Na Mwandishi Wetu| Morogoro

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza ujenzi wa kituo kipya cha afya katika Kata ya Ngerengere, mkoani Morogoro, uanze na ameahidi kutafuta Sh. milioni 100 za kugharamia hatua za awali za mradi huo.
Dkt. Mwigulu alitoa agizo hilo Novemba 22, 2026 wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Taletale, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Ngerengere, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.

Alisema amepokea taarifa kuwa wananchi, kwa kushirikiana na Mbunge wao, wametenga eneo la ekari 15 kwa ajili ya ujenzi huo na kuelekeza kituo hicho kijengwe kwa hadhi ya hospitali ya wilaya.

“Sasa mimi niwaambie, Katibu Tawala wa Mkoa, wekeni makadirio yenu kwenye bajeti inayokuja ili kituo hicho kiweze kujengwa kikiwa ni chenye hadhi ya hospitali ya wilaya,” alisema.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa ujenzi huo uanze sasa wakati taratibu za kuuingiza mradi kwenye bajeti ijayo zikiendelea.

“Wakati ninyi mnajipanga kuweka kwenye bajeti, ujenzi huu uanze, mimi nitawatafutia milioni 100 ili muanze. Tafuteni fundi muanze kujenga,” alisema.

Alieleza kuwa, Serikali itaendelea kutafuta fedha nyingine kwa ajili ya kuendeleza mradi huo, huku akiwataka viongozi na wataalamu wa mkoa wahakikishe fedha za kukamilisha ujenzi zinajumuishwa katika bajeti ijayo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alielekeza gharama za ujenzi wa daraja katika kijiji cha Tununguo ziingizwe kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha baada ya kupokea taarifa kuwa usanifu wake umekamilika.
Wananchi wa Tununguo wanahitaji daraja hilo ili kuvuka Mto Ruvu kuelekea upande wa Ngerengere na makao makuu ya tarafa kupata huduma za kijamii na kibiashara.

Alisema mamlaka zinazohusika zinapaswa kuanza taratibu za kumpata mkandarasi ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huo katika mwaka ujao wa fedha.

“Kwa kuwa mmeshakamilisha usanifu, anzeni taratibu zinazotakiwa ili liwepo kwenye bajeti inayokuja. Lakini pia mpate mkandarasi ili tuweke kwenye mwaka wa fedha unaokuja tulijenge hili daraja,” alisisitiza.
Awali, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Taletale, alimweleza Waziri Mkuu kuwa wananchi wa Ngerengere wanahitaji kituo kipya cha afya kutokana na uchakavu wa kituo kilichopo, pamoja na daraja la Tununguo ili kupunguza hatari wanazokabiliana nazo wakati wa kuvuka mto.

Aidha, Mbunge huyo aliwasilisha ombi la kubadili jina la Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki na kupendekeza liitwe Ngerengere ili kuondoa mkanganyiko wa majina kati ya jimbo hilo na Jimbo la Morogoro Kusini.
Akijibu ombi hilo, Waziri Mkuu alisema pendekezo hilo linapaswa kupitia taratibu zinazohusika katika ngazi mbalimbali, huku akimtaka Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, asimamie mchakato huo ili uweze kuzingatiwa wakati wa kushughulikia majina ya majimbo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here