Na DIRAMAKINI 24| Dar es Salaam
MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imetangaza mafanikio makubwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwemo kugundulika kwa gesi asilia kiasi cha futi za ujazo bilioni 223 katika kisima cha Kasa-1X kilichopo Kitalu cha Mnazi Bay na kuokoa Dola za Marekani 3,306,678 sawa na Shilingi bilioni 8.86 kupitia kaguzi za gharama na mapato.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Mhandisi Charles Sangweni wakati akitoa tathmini ya utekelezaji wa majukumu yake katika kikao kazi kwa wahariri kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa lengo la kuhabarisha umma kuhusu kazi zinazotekelezwa na Serikali kupitia taasisi zake.
Amesema, PURA ilianzishwa kupitia Kifungu Na. 11 cha Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, ikiwa na majukumu makuu ya kusimamia utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia, kusimamia na kudhibiti shughuli za mkondo wa juu wa petroli, na kusimamia miradi ya kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG).
UZALISHAJI WAONGEZEKA
Amesema, katika mwaka 2025/2026, jumla ya futi za ujazo bilioni 65.4 za gesi asilia zilizalishwa katika vitalu vya Songo Songo na Mnazi Bay, ikilinganishwa na bilioni 62.6 zilizozalishwa mwaka 2024/2025.
Ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa mahitaji na matumizi ya gesi asilia nchini hususan viwandani na matumizi katika magari (CNG).
VISIMA VITATU MNAZI BAY
Ameongeza kuwa, PURA ilisimamia uchorongaji wa visima vitatu katika Kitalu cha Mnazi Bay, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
"Visima hivyo ni Mnazi Bay Five (MB-5) na Msimbati Two (MS-2) ambavyo ni vya uzalishaji, na Kasa One X (Kasa-1X) ambalo ni kisima cha utafutaji," amesema.
Visima vya MB-5 na MS-2 vilikamilishwa na kuanza uzalishaji ambapo vina uwezo wa kuzalisha wastani wa futi za ujazo milioni 40 na milioni 50 kwa siku huku uchorongaji wa Kasa-1X ukikamilika kwa mafanikio na kugundua gesi asilia kiasi cha futi za ujazo bilioni 223.
RUVUMA NA TANGA
Amesema, PURA imeendelea kusimamia uendelezaji wa gesi asilia katika Kitalu cha Ruvuma, ambapo maandalizi ya uchorongaji wa kisima cha Chikumbi-1 (CH-1), ukarabati wa kisima cha Ntorya-1 (NT-1) na majaribio ya uzalishaji wa kisima cha Ntorya-2 (NT-2) yanaendelea.
Katika Kitalu cha Tanga, PURA imesimamia tafsiri mpya ya data za mitetemo za 3D ambapo matokeo yanaonesha maeneo matatu yenye viashiria vya uwepo wa mafuta (Prospect 1, 3 na 5). Maandalizi ya kuchoronga kisima cha utafutaji yanaendelea na uchorongaji unatarajiwa kufanyika mwaka 2027.
TAFITI ZA AWALI
Ameongeza kuwa, katika eneo la Eyasi-Wembere, uchukuaji wa data za mitetemo za 2D umefikia asilimia 99, ambapo jumla ya kilomita za mistari 772 kati ya 779 zimeshakusanywa hadi tarehe 30 Juni 2026.
Katika eneo la Lindi-Mtwara, uchukuaji wa data za mitetemo za 3D umefikia kilomita za mraba 257.96 kati ya 736.3, sawa na asilimia 35.
KAGUZI ZAOKOA BILIONI 8.8
Amesema PURA ilikamilisha kaguzi za gharama na mapato katika vitalu vya Songo Songo kwa mwaka 2023 na 2024, Kitalu Na. 1 na 4 kwa mwaka 2023 na 2024, na Kitalu cha Ruvuma kwa mwaka 2024, na kuanza kaguzi katika Vitalu vya Songo Songo kwa mwaka 2025 na Kitalu Na. 2 kwa mwaka 2023.
"Kupitia kaguzi hizo, jumla ya Dola 3,306,678 sawa na Shilingi 8,861,897,040 ziliokolewa na kurudishwa katika fungu la ugawanaji wa mapato," amesema.
Aidha, PURA ilikamilisha uandaaji wa Mfumo wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Hesabu za Gharama na Mapato (Cost Recovery Management System - CRMS) utakaorahisisha uwasilishwaji na uhifadhi wa taarifa za mapato na gharama.
USHAURI NA KANUNI
PURA ilitoa ushauri kwa Serikali kuhusu mikataba na leseni za Ruvu, Nyuni Area, Nyuni Mashariki ya Songo Songo na Bigwa-Rufiji-Mafia (BRM), na mapendekezo ya maboresho ya Sera ya Nishati 2015, Sheria ya Petroli 2015 na Kanuni mbalimbali.
Pia ilifanya mapitio ya Kanuni za Petroleum (Reconnaissance and Tendering) na Petroleum (Natural Gas Pricing) zilizochapishwa katika Gazeti la Serikali mwezi Agosti 2025, na kuandaa Kanuni za Petroleum (Decommissioning) na Petroleum (Corporate Social Responsibility).WATANZANIA WANANUFAIKA
Thamani ya bidhaa na huduma zilizotolewa na kampuni za ndani imeongezeka hadi zaidi ya Dola za Marekani milioni 30 kwa mwaka 2026, ikilinganishwa na Dola milioni 14 mwaka 2025.
Upande wa CSR, PURA ilisimamia ujenzi wa Shule ya Msingi Likong'o katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, ufungaji wa majiko ya kisasa ya kupikia kwa kutumia nishati ya LPG katika shule nne zilizopo Kata ya Msimbati, Mtwara, na ufadhili wa vijana kusoma ufundi katika Chuo cha VETA mkoani Lindi.
Amesema, PURA itaendelea kuimarisha usimamizi wa mkondo wa juu wa petroli ili kuhakikisha sekta ya nishati inaendelea kuchangia ipasavyo katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Ofisi ya Msajili wa Hazina
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Msajili wa Hazina, Bw. Sabato Kosuri amesema, PURA ina mchango mkubwa sana katika kuhakikisha sekta ya mafuta na gesi inachangia pato la taifa kwa ujumla na kukuza uchumi.
Amesema, katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sekta ya mafuta na gesi ina nafasi muhimu katika kulinda uwekezaji, kukuza uchumi jumuishi na kuongeza upatikanaji wa huduma za mafuta na gesi.
Aidha, ameishauri PURA na kwamba kikao hicho kisiwe mwisho na badala yake waendeleze utaratibu huo ili wananchi waweze kupata uelewa kuhusu masuala yanayohusu mafuta na gesi asilia nchini.



