EAC yahitimisha Mkutano wa 49 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji

ARUSHA- Mkutano wa 49 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (SCTIFI) umehitimishwa jijini Arusha tarehe 13 Novemba 2026, katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), baada ya kukamilika kwa majadiliano katika ngazi ya Mawaziri.
Ujumbe wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika ngazi ya Mawaziri umeongozwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Munde, akiambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Millya. 

Vilevile, mkutano huo ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Bw. Charles Kadonya, pamoja na Katibu Mkuu wa Uwekezaji kutoka Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa, wakiongozana na wakurugenzi na maafisa kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali.
Katika mkutano huo, Mawaziri walipitia taarifa na mapendekezo yaliyowasilishwa katika majadiliano ya ngazi ya Makatibu Wakuu, kwa lengo la kujadili na kufikia makubaliano kuhusu sera na mifumo mbalimbali inayohusu maswala kadhaa hususan hali ya vikwazo visivyo vya ushuru wa forodha (NTBs) ili kuboresha mazingira ya biashara, viwanda, fedha na uwekezaji. 

Baada ya majadiliano, sera na mapendekezo mbalimbali yalipitishwa kwa ajili ya kuendeleza ushirikiano na kuboresha mazingira ya kiuchumi katika Jumuiya.

Aidha, Nchi Wanachama zilikubaliana kuendeleza mashauriano na kuharakisha hatua za kushughulikia NTBs zilizobainika, ambazo zinaweza kuchelewesha utekelezaji wa maamuzi ya wakuu wa Nchi wanachama wa EAC katika Mkutano wao wa 25.

Msisitizo uliwekwa katika kuhakikisha mifumo iliyokubaliwa inafanyiwa kazi kwa wakati ili kurahisisha biashara na shughuli za kiuchumi, kuongeza ufanisi katika taratibu za mipakani na kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara, wananchi na wawekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kupitishwa kwa mapendekezo hayo kunatarajiwa kuchangia katika kukuza uzalishaji wa viwandani, kuongeza shughuli za kiuchumi na kupanua fursa za biashara na uwekezaji miongoni mwa Nchi Wanachama.

Mkutano huo umehitimisha mchakato wa siku tano wa majadiliano katika ngazi za Wataalamu, Makatibu Wakuu na Mawaziri, ukiweka msingi wa hatua zaidi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here