NA MARY GWERA,
Mahakama Arusha
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Arusha, Mhe. Frank Mahimbali leo tarehe 12 Novemba, 2026 amemwakilisha Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju katika hafla ya Maadhimisho ya miaka 25 (Silver Jubilee) tangu kuanzishwa kwa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) iliyofanyika jijini Arusha.
Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda, Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji na Viongozi wengine waliohudhuria katika hafla ya maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) leo tarehe 12 Novemba, 2026 jijini Arusha. Wa tatu kulia ni Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe. Nestor Kayobera, wa kwanza kushoto ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, wa pili kushoto ni Jaji Mkuu wa Malawi na Mwenyekiti wa Jukwaa la Majaji Wakuu wa Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF), Mhe. Rizine Mzikamanda. Waliosimama (wa kwanza kulia) ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Arusha, Mhe. Frank Mahimbali pamoja na Viongozi wengine walioshiriki katika maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama hiyo.
Akifungua hafla ya maadhimisho hayo kwa niaba ya Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda, Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga ameipongeza Mahakama hiyo kwa mafanikio makubwa tangu ilipoanza kufanya kazi mwaka 2001 ikiwa na nchi tatu pekee Tanzania, Uganda na Kenya hadi kufikia nchi wanachama nane zenye zaidi ya watu milioni 350, zikijumuisha ukanda wote kuanzia Bahari ya Hindi (Somalia na Tanzania) hadi Bahari ya Atlantiki (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo).
Katika hotuba yake, mgeni rasmi ameeleza umuhimu wa mtangamano wa kikanda akirejea mazungumzo yake ya mwisho na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, jijini Arusha kuhusu mustakabali wa Bara la Afrika. Amefafanua kuwa, Afrika ilichelewa kuendelea na kujikuta ikitawaliwa na wakoloni kutokana na mgawanyiko na ubinafsi wa kiutawala, hali aliyoiita kwa lugha ya asili ‘okukonesa’ au ‘ukusia’ kwa Kiswahili yaani kupika chakula kwa moto usio na uwiano na kukifanya kiive nusu, hivyo kupoteza rasilimali.

Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda, Mhe. Rebecca Alitwala Kadaga akitoa hotuba kwa niaba ya Rais wa Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni leo tarehe 12 Novemba, 2026 wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ).
Amebainisha kuwa, kizazi chao kiliweka malengo makuu manne ya kihistoria kwa Afrika: ukombozi dhidi ya ukoloni (ambao umekamilika), kwenda na wakati kupitia sayansi na teknolojia, kuleta ustawi wa kiuchumi kwa wananchi, pamoja na ulinzi na usalama wa kimkakati.
Alisisitiza kuwa ustawi wa kiuchumi hauwezi kuja kwa maombi pekee wala kwa kesi zisizoisha mahakamani, bali kwa kuzalisha bidhaa na huduma na kuwa na soko kubwa la ndani la watu milioni 350, kama ilivyo kwa mataifa tajiri duniani kama Marekani, China na India.
Katika hotuba yake iliyosomwa na Mhe. Kadaga, Rais Museven amezungumzia wajibu wa Mahakama ya Afrika Mashariki ya Haki, kuwa, Mahakama hiyo haikuundwa ili watu waje Arusha kubishana kuhusu vifungu vya kisheria na kukwamisha maendeleo, bali ili kuwa mlinzi wa Mkataba wa Jumuiya na kiunganishi cha biashara.
Amesema kuwa, wawekezaji wanapokuja Afrika Mashariki, swali lao la kwanza ni iwapo kuna mwamuzi huru na wa haki endapo malori yao yatakwamishwa mipakani kama vile Namanga au Malaba. Alionya kuwa, bila mfumo wa haki wa kibiashara ulio wa haraka na unaotabirika, wawekezaji watakata tamaa, mitaji itaisha, na vijana wataendelea kupoteza maisha wakivuka Bahari ya Mediterania kwenda Ulaya kutafuta ajira.
Washiriki kutoka Mahakama ya Tanzania wakiwemo baadhi ya Majaji, Mtendaji Mkuu, Msajili Mkuu Naibu Wasajili pamoja na Mahakimu walioshiriki katika hafla ya Maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) wakiwa katika picha ya pamoja.
Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe. Nestor Kayobera akitoa neno wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama hiyo leo tarehe 12 Novemba, 2026 jijini Arusha.
Aidha, ametoa wito kwa Majaji wa Mahakama za Kitaifa na Kikanda kuondokana na kile alichokiita "mchanganyiko wa kiitikadi" (ideological disorientation), ambapo baadhi ya Majaji hunakili maamuzi ya kisheria kutoka Ulaya bila kuzingatia mazingira halisi ya kiuchumi na kijamii ya nchi zinazoendelea.
Amekemea tabia ya kutoa zuio la Mahakama (injunctions) linalosimamisha miradi mikubwa ya kimkakati kama ujenzi wa barabara, reli, au mabwawa ya umeme kwa miaka mingi kutokana na kasoro ndogo za kiutaratibu, huku akisisitiza kuwa, sheria inapaswa kuwa chombo cha mabadiliko ya kijamii na ukombozi wa kiuchumi, na si kikwazo cha maendeleo.
Kuhusu changamoto ya utekelezaji wa hukumu za Mahakama iliyotajwa awali na Rais wa Mahakama hiyo, Mhe. Nestor Kayobera (Jaji), mgeni rasmi alikubaliana na kauli yake kuwa, Mahakama ambayo maamuzi yake hayatekelezwi ni sawa na simba asiye na meno.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa suluhisho la kudumu la vikwazo vyote vya kibiashara, kiusalama, na kimahakama ni kufikia Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki (East African Political Federation), ambalo litakuwa na mfumo mmoja wa Mahakama, Jeshi moja la ulinzi, na sauti moja duniani.
Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Kadaga amewahimiza Majaji na Watumishi wa Mahakama hiyo kuongeza kasi ya utatuzi wa migogoro ya kibiashara, kuachana na urasimu wa kisheria unaokwamisha maendeleo, na kuliongoza eneo la Afrika Mashariki kuelekea kwenye uchumi wa kisasa, wenye ustawi na usalama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Arusha, Mhe. Frank Mahimbali (wa kwanza kulia) pamoja na wageni wengine wakifuatilia kinachojiri wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) leo tarehe 12 Novemba, 2026.
Awali akitoa neno kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki ya Haki (EACJ), Mhe. Nestor Kayobera amesema Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) imeadhimisha Jubilei ya Fedha (miaka 25) tangu kuanzishwa kwake, ikiwa na wito mahsusi kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuheshimu na kutekeleza hukumu zinazotolewa na Mahakama hiyo ili kuimarisha utawala wa sheria na mtangamano wa kikanda.
Katika hotuba yake, Mhe. Kayobera amesema ili kuendana na kasi ya ukuaji wa mtangamano wa Jumuiya ikiwemo Soko la pamoja na Umoja wa Fedha, ameainisha vipaumbele vitano vikuu kwa miaka 25 ijayo ambavyo ni pamoja na Kupanua mamlaka ya Mahakama chini ya Kifungu cha 27(2) ili kujumuisha masuala ya biashara, uwekezaji, na fedha, Kukamilisha suala la Makao makuu ya kudumu ya Mahakama hiyo.
Masuala mengine aliyosisitiza ni pamoja na Kuongeza uelewa kwa umma kuhusu majukumu na taratibu za mahakama kupitia elimu ya sheria na mifumo ya kidijitali, Kukuza njia mbadala za utatuzi wa migogoro (ADR) kama vile usuluhishi na upatanishi pamoja na Kuimarisha ushirikiano na Mahakama za kitaifa, Vyama vya Mawakili, Vyuo Vikuu na Vyombo vya Habari.
Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia alikuwa kuwa Msajili wa kwanza wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe. Prof. John Ruhangisa akitoa uzoefu wake wa utumishi katika Mahakama hiyo na namna ya kuendelea kuiboresha zaidi.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla pamoja na wajumbe wengine wakifuatilia kinachojiri katika hafla ya ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) leo tarehe 12 Novemba, 2026 jijini Arusha.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Arusha, Mhe. Nyigulila Mwaseba (aliyeketi nyuma) wakiwa katika hafla ya maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki leo tarehe 12 Novemba, 2026.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akitoa neno wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) leo tarehe 12 Novemba, 2026 jijini Arusha.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi amesema, uwezo wa Mahakama ya Afrika Mashariki unapaswa kuimarishwa kuhudumia Nchi nane Wanachama huku akisisitiza juu ya hatua za makusudi za kuongeza uwezo wa rasilimali watu, fedha na miundombinu ya kidijitali ili kukidhi mahitaji ya nchi wanachama zilizofika nane.
Aidha, Katibu Mkuu huyo amebainisha kuwa, tangu kuzinduliwa kwa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) tarehe 30 Novemba, 2001, na kuanzishwa kwa Divisheni ya Kwanza na ya Rufaa mwaka 2006 Mahakama imesajili jumla ya mashauri 1,032 kufikia Agosti 2026 ambapo ameeleza kuwa, idadi hiyo inaonesha jinsi wananchi na wadau wanavyoendelea kuamini Mahakama hiyo katika kutatua migogoro na kutafsiri Mkataba wa EAC.
Katika kujiandaa na miaka 25 ijayo, Katibu Mkuu huyo ameeleza vipaumbele viwili vikuu vya kuzingatiwa ambavyo ni Kuimarisha Uwezo wa Mahakama kwa kuongeza rasilimali ili kukabiliana na ukuaji wa Jumuiya tangu ilipoanza na Nchi Wanachama 3 hadi kufikia 8 kwa sasa, pamoja na kuweka mifumo ya kisasa ya kidijitali ili kuharakisha usimamizi wa mashauri.
Amekumbusha kuwa, EACJ ilikuwa miongoni mwa Mahakama za kwanza duniani kubadilisha kanuni zake kuwezesha vikao vya mtandao wakati wa janga la UVIKO-19 mwaka 2020.
Jambo lingine amezungumzia kuhusu Matumizi ya Utatuzi wa Migogoro kwa njia ya Usuluhishi (Arbitration), ambapo ameeleza kuwa eneo la usuluhishi kupitia Mahakama halijatumika kikamilifu, licha ya ukuaji wa biashara na uwekezaji kikanda. Ameagiza taasisi zote za EAC zihakikishe usuluhishi ndani ya EACJ unakuwa njia kuu ya utatuzi wa migogoro katika mikataba yote endapo suluhu ya amani itashindikana.
Aidha, ameahidi kuwa, Sekretarieti ya EAC itaendelea kushirikiana na Uongozi wa Mahakama hiyo katika kuhamasisha rasilimali, kuratibu masuala ya kiutawala, na kufanyia kazi mapendekezo yatakayotolewa katika kongamano hilo kupitia vyombo vya maamuzi vya Jumuiya.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu (kulia) akiwa pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) leo tarehe 12 Novemba, 2026.
Meza kuu katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Tanzania walioshiriki.
Meza za pamoja na washiriki mbalimbali waliohudhuria hafla ya maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) leo tarehe 12 Novemba, 2026.

Wimbo wa Afrika Mashariki ukiimbwa kabla ya kuanza kwa hafla ya Maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ).
Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), Mhe. Yohane Masara akitoa hotuba ya kufunga hafla maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama hiyo leo tarehe 12 Novemba, 2026.
Viongozi wakiwa wameshika Vitabu vya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ).(Picha na MARY GWERA & JEREMIA LUBANGO, Mahakama-Arusha).
Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu isemayo; Miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, kutoka msingi hadi mustakabali yamepambwa na matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na mijadala ya kubadilishana uzoefu na kutathmini mchango wa Mahakama hiyo katika kutatua migogoro, kulinda haki na kuhakikisha utekelezaji wa Mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Majaji,Wasajili, Mahakimu wa Mahakama na Wadau mbalimbali wa Mahakama. Na kwa upande wa Mahakama ya Tanzania baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani akiwemo Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, Mhe. Yohane Masara na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu Arusha, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Dkt. John Antony Jingu, Msajili Mkuu, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Naibu Msajili na Rais wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), Mhe. Elimo Massawe na wengine kadhaa wameshiriki katika Maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama hiyo.
Matukio katika picha Hafla ya Maadhimisho ya miaka 25 ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) leo tarehe 12 Novemba, 2026 katika Ofisi za Makao Makuu ya Afrika Mashariki jijini Arusha.



















