Na DIRAMAKINI 24| Dar es Salaam
SEKTA ya Bima nchini imepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, huku mchango wake katika Pato la Taifa ukiongezeka kutoka asilimia 1.68 mwaka 2021 hadi asilimia 2.11 mwaka 2025, sambamba na ongezeko la watumiaji wa bidhaa na huduma za bima kutoka milioni 5.6 hadi milioni 26.8.
Mafanikio hayo yanaashiria kuongezeka kwa mwamko wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima, kuimarika kwa usimamizi wa soko na kupanuka kwa huduma zinazotolewa na kampuni za bima nchini.Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware ameyasema hayo leo Novemba 16, 2026 jijini Dara es Salaam wakati akizungumza katika kikao kazi kati ya mamlaka hiyo, wahariri na waandishi wa habari, chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema, mafanikio hayo yametokana na usimamizi madhubuti wa Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Tanzania (TIRA), pamoja na utekelezaji wa sera na maelekezo ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha.
Dkt. Saqware amesema, katika kipindi hicho, sekta ya bima imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kulinda maisha, mali, afya, biashara na uwekezaji dhidi ya vihatarishi mbalimbali, huku ikiimarisha ustahimilivu wa uchumi na kuwezesha wananchi na taasisi kuendelea na shughuli zao wanapokumbwa na majanga.
Amesema, thamani ya ada za bima zilizoandikishwa (Gross Written Premiums) imeongezeka kutoka Sh bilioni 911 mwaka 2021 hadi Sh trilioni 2.55 mwaka 2025, huku thamani ya madai ya bima yaliyolipwa kwa mwaka ikipanda kutoka Sh bilioni 397.57 hadi Sh trilioni 1.29 katika kipindi hicho.
Aidha, amesema thamani ya mali zilizowekezwa na kampuni za bima imeongezeka kutoka Sh bilioni 939.69 mwaka 2021 hadi Sh trilioni 2.24 mwaka 2025, wakati thamani ya mitaji katika soko hilo ikipanda kutoka Sh bilioni 416 hadi Sh trilioni 1.89.
Ameeleza kuwa, ongezeko hilo linaonesha kuimarika kwa uwezo wa sekta ya bima katika kukusanya rasilimali, kufanya uwekezaji na kutekeleza wajibu wake wa kufidia wateja wanaostahili kulipwa madai.
Katika upande wa manufaa kwa wananchi, amesema kiwango cha matumizi ya bima kimeongezeka kutoka asilimia 8.9 mwaka 2021 hadi asilimia 39.3 mwaka 2025, huku wastani wa fedha zinazotumiwa na mtu mmoja kwa ajili ya bima ukipanda kutoka Sh 15,334 hadi Sh 37,455.
Vilevile, ajira rasmi katika soko la bima zimeongezeka kutoka 3,737 mwaka 2021 hadi kufikia 15,398 mwaka 2025, jambo linaloonesha mchango wa sekta hiyo katika kukuza fursa za ajira na shughuli za kiuchumi.
Dkt. Saqware amesema, watoa huduma za bima wameongezeka kutoka 993 mwaka 2021 hadi 10,940 mwaka 2025, huku uwezo wa sekta ya ndani kubeba vihatarishi ukiimarika na kufikia thamani ya Sh trilioni 193.53, sawa na asilimia 94.5 ya Pato la Taifa.
Ameongeza kuwa uwezo huo umeendelea kuimarishwa katika maeneo ya kilimo, nishati, mafuta na gesi kupitia taasisi za Tanzania Agriculture Insurance Consortium (TAIC) na Tanzania Energy and Capital Insurance Consortium (TECC).
TIRA yajitegemea kwa asilimia 100, gawio kwa Serikali laongezeka
Akizungumzia mafanikio ya taasisi anayoiongoza, Dkt. Saqware amesema, TIRA imeongeza mchango wake kwa Serikali kupitia gawio lililopanda kutoka Sh bilioni 3.56 mwaka 2021 hadi Sh bilioni 5.13 mwaka 2025.
Amesema, taasisi hiyo imeendelea kupata hati safi za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka yote kuanzia 2022 hadi 2025, hatua inayoonesha kuimarika kwa usimamizi wa rasilimali na uwajibikaji wa kifedha.
Aidha, TIRA imekamilisha ujenzi wa makao makuu yake jijini Dodoma mwaka 2025 na kufanikiwa kujitegemea kwa asilimia 100 katika kugharamia mishahara, stahiki za watumishi na shughuli zake za maendeleo.
Katika kipindi hicho, thamani ya mali za taasisi imeongezeka kutoka Sh bilioni 11.18 mwaka 2021 hadi Sh bilioni 21.72 mwaka 2025.
Amesema, idadi ya watumishi imeongezeka kutoka 112 mwaka 2021 hadi 151 mwaka 2025, huku asilimia 49 wakiwa na elimu ya uzamili, stashahada za uzamili na uzamivu, asilimia 31 wakiwa na shahada na asilimia 20 wakiwa na stashahada na vyeti.
Ameeleza kuwa, mamlaka hiyo inaendelea kuwekeza katika kuwajengea watumishi uwezo wa kitaaluma kupitia mafunzo, uzoefu na utekelezaji wa majukumu kwa vitendo ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa sekta.
Vilevile, mtandao wa ofisi za TIRA umeongezeka kutoka sita mwaka 2021 hadi 13 mwaka 2025, ukiwemo upanuzi wa huduma katika maeneo ya Unguja na Pemba.
Mifumo ya kidijitali yaimarisha utoaji huduma
Katika hatua nyingine, Dkt. Saqware amesema, TIRA imeimarisha matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa shughuli za bima kwa kuanzisha na kuendeleza mifumo mbalimbali ya kidijitali inayorahisisha utoaji wa huduma kwa wadau.
Amezitaja mifumo hiyo kuwa ni TIRA Management Information System (TIRAMIS), Online Registration System (ORS), TSS Portal, Insurance Regulatory Information System (IRIS) na mfumo wa malalamiko wa kielektroniki (E-Complaint).
Amesema, mifumo hiyo imewezesha kurahisisha maombi ya leseni, uwasilishaji wa taarifa za kampuni za bima, usimamizi wa shughuli za soko na upokeaji pamoja na ushughulikiaji wa malalamiko ya wateja.
Aidha, amesema TIRA imeendelea kuunganisha mifumo yake na ile ya taasisi nyingine za umma na binafsi ili kuongeza ufanisi, uwazi na upatikanaji wa taarifa kwa wakati.
Katika kutambua utendaji wake, amesema TIRA imepata alama za asilimia 86, zilizoiweka katika kundi la utendaji bora zaidi (Excellent) katika tathmini ya utendaji wa Bodi na Menejimenti kwa mwaka wa fedha 2024/2025, iliyofanywa kupitia kampuni huru za ukaguzi kwa niaba ya Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Pia, imepata cheti cha kutambua utii bora wa sheria za kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Vilevile, amesema taasisi hiyo imekuwa mshindi wa pili katika tuzo ya matumizi bora ya fedha kwa taasisi za umma zisizo za kibiashara zilizo chini ya usimamizi wa Msajili wa Hazina, tuzo inayotolewa katika mkutano wa Wakuu wa Taasisi (C-CEO Forum).
TIRA yaweka mikakati ya kulinda fedha na haki za wateja
Akizungumzia jukumu la udhibiti, Dkt. Saqware amesema, TIRA imeweka msimamo wa kuhakikisha soko la bima linaendeshwa kwa misingi ya weledi, uadilifu, ushindani wa haki na uwajibikaji, huku likiwa salama, endelevu na lenye uwezo wa kustahimili vihatarishi.
Amesema, mamlaka hiyo inataka kampuni za bima zikue kutokana na uwezo na ubora wa huduma zake, badala ya kutumia udanganyifu au vitendo vinavyokiuka sheria na kanuni za sekta hiyo.
Amefafanua kuwa, katika kutekeleza wajibu wake, TIRA inahakikisha kampuni zote zinatimiza masharti ya kisheria, yakiwemo kuwa na mtaji wa kutosha wakati wote, kulipa madai halali ya wateja kwa wakati, kuwa na mikataba hai ya bima mtawanyo na kuzingatia misingi ya utawala bora.
Masharti mengine ni kuweka amana ya dhamana inayotakiwa katika Benki Kuu ya Tanzania na kuhakikisha kampuni zina uwezo wa kutekeleza majukumu yake ya kifedha bila kuhatarisha maslahi ya wateja.
Amesema, pale mamlaka inapobaini ukiukwaji wa masharti au changamoto zinazoweza kuathiri uwezo wa kampuni kutekeleza wajibu wake, huchukua hatua stahiki kulingana na uzito wa tatizo na athari zinazoweza kujitokeza.
Amezitaja dalili zinazowekwa katika uangalizi wa karibu kuwa ni upungufu mkubwa wa mtaji na ukwasi, malimbikizo ya madeni na madai ya wateja, pamoja na kushindwa kulipa madeni ya bima mtawanyo au kukosa mikataba hai ya huduma hiyo.
Dalili nyingine ni kuwa na madeni ya muda mrefu kwa taasisi za kisheria kama TRA, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), pamoja na kushindwa kuzingatia misingi ya utawala bora, ikiwemo kutofanyika kwa mikutano mikuu ya wanahisa na vikao vya bodi.
Ameongeza kuwa, idadi kubwa ya kesi mahakamani na kutokuwa na amana ya dhamana inayostahili katika Benki Kuu ya Tanzania ni viashiria vingine vinavyoweza kuashiria kampuni kuwa katika hatari kubwa ya kifedha na kiutendaji.
Kamishna huyo amesema, kampuni zinazobainika kuwa na viashiria hivyo huwekwa katika kundi la uangalizi wa hatari kubwa (Serious Risk Indicators), hatua inayoiwezesha TIRA kuchukua tahadhari mapema ili kuzuia madhara kwa wananchi na soko la bima kwa ujumla.
Amesema, hatua hizo zinalenga kulinda imani ya wananchi katika huduma za bima, kuimarisha uthabiti wa mfumo wa fedha na kuhakikisha ushindani unafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali.
Ameishukuru Wizara ya Fedha, hususan Ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, kwa usimamizi na maelekezo yanayolenga kuhakikisha soko la bima linaendeshwa kwa kuzingatia sheria na kulinda maslahi ya wananchi.
Bima ya Afya kwa Wote: Kaya 625,000 kulengwa katika awamu ya pili
Katika eneo la huduma za afya, Dkt. Saqware amesema, TIRA inaendelea kushiriki katika kusimamia na kuimarisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bila kuzuiwa na changamoto za kifedha.
Ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka msukumo katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora za afya na kuimarisha mfumo wa bima ya afya nchini.
Amesema, baada ya utekelezaji wa awamu ya kwanza, iliyolenga kuwafikia wananchi wasio na uwezo wa kugharamia huduma hizo, Serikali ilizindua awamu ya pili ya mpango huo Oktoba 22, 2026, kupitia Waziri wa Afya, Mohamed O. Mchengerwa.
Kwa mujibu wa Dkt. Saqware, katika awamu ya kwanza, jumla ya kaya 198,709 za wananchi wasio na uwezo zilihakikiwa na kupatiwa kadi za bima ya afya kupitia mpango uliogharamiwa na Serikali.
Amesema, katika awamu ya pili, Serikali inalenga kusajili kaya nyingine 625,000 za wananchi wasio na uwezo, sambamba na kupanua fursa kwa wananchi wenye uwezo wa kuchangia kujiunga na mfumo huo.
Ameeleza kuwa, bima ya afya ni kinga ya kifedha inayomwezesha mwananchi kupata huduma za matibabu anapozihitaji bila gharama zake kuwa mzigo mkubwa unaoweza kuathiri maisha na shughuli zake za kiuchumi.
Amesisitiza kuwa, bima ya afya si huduma inayopaswa kutafutwa baada ya mtu kuugua, bali ni maandalizi muhimu ya kumwezesha mwananchi kukabiliana na gharama za matibabu pale anapokumbwa na changamoto za kiafya.
Kutokana na umuhimu huo, amewahimiza wananchi ambao bado hawajajiunga na bima ya afya kufanya hivyo kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) au kampuni binafsi zilizosajiliwa na kuidhinishwa na TIRA.
Kampuni za bima zahimizwa kutoa taarifa sahihi kwa wananchi
Dkt. Saqware amesema, TIRA ina wajibu wa kuhakikisha skimu za bima ya afya zilizosajiliwa zinatoa taarifa sahihi, kamili na zinazoeleweka kuhusu vifurushi vyao kabla ya wananchi kujiunga.
Amesema, ni muhimu kila mwanachama kufahamu huduma zinazolipiwa na bima yake, zile zisizojumuishwa, masharti ya matumizi na utaratibu wa kupata huduma katika vituo vya afya.
Aidha, amesisitiza kuwa wananchi hawapaswi kupotoshwa kupitia matangazo au ahadi zinazoweza kuwafanya kujiunga na vifurushi bila kuelewa masharti na haki zao.
Ameeleza kuwa, usajili unapaswa kufanyika kwa uwazi na kwa urahisi, huku wanachama wakipewa taarifa kuhusu vituo vya kutolea huduma za afya wanavyoweza kutumia pamoja na taratibu za rufaa.
Vilevile, amezitaka skimu za bima kuhakikisha malalamiko ya wanachama yanapokelewa, kuchunguzwa na kutatuliwa kwa wakati ili kujenga imani ya wananchi katika mfumo huo.
Amesema, TIRA imeendelea kuimarisha usimamizi wa Bima ya Afya kwa Wote kupitia mpango wa kuwa na maafisa uhusiano wa TIRA katika halmashauri, kwa kushirikiana na maafisa maendeleo ya jamii katika ngazi za wilaya, halmashauri na kata.
Hatua hiyo inatekelezwa kwa ushirikiano kupitia makubaliano ya pamoja (MoU) kati ya TIRA, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara inayohusika na maendeleo ya jamii.
Elimu ya bima na ulinzi wa wateja kupewa kipaumbele
Katika kuendeleza sekta hiyo, Kamishna huyo amesema, TIRA imeimarisha utoaji wa elimu kwa umma, utatuzi wa migogoro na ulinzi wa haki za watumiaji wa huduma za bima.
Amesema, mamlaka hiyo pia imeanzisha kitengo maalumu cha kupambana na udanganyifu katika sekta ya bima ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na imani ya wananchi.
Aidha, imeanzisha mikakati ya kuvutia ubunifu kupitia mpango wa Regulatory Innovation and Development Ecosystem Strategy (RIDES), pamoja na mkakati wa kuchochea ujumuishaji wa huduma za bima nchini (National Insurance Inclusion Strategy – NIIS).
Dkt. Saqware amewashukuru wahariri na waandishi wa habari kwa mchango wao katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa bima, akisema ushirikiano wao umekuwa sehemu muhimu ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo.
Amesema, TIRA itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu huduma za bima, haki zao na wajibu wa kampuni zinazotoa huduma hizo.
Amesisitiza kuwa, lengo kuu la mamlaka hiyo ni kujenga soko la bima linaloaminika, lenye uwezo wa kulinda wananchi na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Msajili wa Hazina
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Msajili wa Hazina ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msaji wa Hazina, Bw. Sabato Kosuri amesema, TIRA ina mchango muhimu katika kulinda wananchi, biashara na uwekezaji dhidi ya vihatarishi na hasara zinazoweza kujitokeza, huku ikiimarisha uthabiti wa sekta ya fedha na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Amesema, katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sekta ya bima ina nafasi muhimu katika kulinda uwekezaji, kukuza uchumi jumuishi na kuongeza upatikanaji wa huduma za bima kwa wananchi na wafanyabiashara wadogo, akisisitiza kuwa mafanikio ya sekta hiyo hayapaswi kupimwa kwa ongezeko la kampuni au thamani ya biashara pekee, bali pia uwezo wa wananchi kupata huduma na kulipwa madai yao kwa wakati.
TIRA ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bima, Sura ya 394, ikiwa na jukumu la kusimamia na kuendeleza sekta ya bima nchini. Majukumu yake yanajumuisha kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma, kuandaa kanuni na miongozo, kutoa elimu kwa umma, kulinda haki za watumiaji na kuishauri Serikali kuhusu sera na masuala yanayohusu sekta hiyo.






























