Ofisi ya Msajili wa Hazina: TIRA ni nguzo muhimu ya uchumi imara na ustahimilivu kuelekea Dira 2050

Na DIRAMAKINI 24| Dar es Salaam

OFISI ya Msajili wa Hazina imesema kuwa, Sekta ya Bima nchini ni nyenzo muhimu katika kuimarisha uchumi, kulinda uwekezaji na kuhakikisha wananchi pamoja na taasisi mbalimbali zinakuwa na uwezo wa kukabiliana na hasara zinazoweza kusababishwa na majanga na vihatarishi vya kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo Novemba 16, 2026 jijini Dar es Salaam na Mwakilishi wa Msajili wa Hazina, Bw. Sabato Kosuri katika kikao kazi cha wahariri wa vyombo vya habari na Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Tanzania (TIRA), kilicholenga kuongeza uelewa kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo na mchango wake katika maendeleo ya Taifa.

Kikao kazi hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Msaji wa Hazina huku pia kikiwaleta pamoja waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Bw. Kosuri ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina amesema, TIRA ina wajibu muhimu wa kusimamia na kuendeleza sekta ya bima nchini, kwa kuhakikisha kunakuwa na soko lenye uwazi, ufanisi na ushindani, huku likizingatia ulinzi wa maslahi ya wateja na wadau wengine.

Amesema, bima haipaswi kuonekana kama huduma ya kifedha pekee, bali ni kinga inayowawezesha watu binafsi, wafanyabiashara na taasisi kulinda mali, shughuli zao na uwekezaji dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na matukio yasiyotazamiwa.
Mwakilishi huyo wa Msajili wa Hazina amefafanua kuwa, kupitia huduma za bima, wananchi na taasisi wanaweza kupunguza athari za kifedha zinazotokana na majanga au vihatarishi mbalimbali na hivyo kuendelea na shughuli zao hata baada ya kukumbwa na hasara zinazostahili kulipwa kwa mujibu wa mikataba ya bima.

Akizungumzia mchango wa TIRA katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Bw. Kosuri amesema, mamlaka hiyo ina nafasi ya kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuhakikisha sekta ya bima inakuwa imara, jumuishi na yenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya wananchi na wawekezaji.

Amezitaja njia tano ambazo sekta hiyo inaweza kuchangia kufanikisha azma hiyo kuwa ni kulinda biashara na uwekezaji dhidi ya vihatarishi, kupanua upatikanaji wa huduma za bima, kuimarisha uthabiti wa sekta ya fedha, kuchochea uwekezaji na biashara pamoja na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma na haki zao.
Pia, amesema upatikanaji mpana wa huduma za bima, hususan kwa wafanyabiashara wadogo na wananchi wenye kipato cha chini, ni muhimu katika kujenga uchumi shirikishi unaowapa makundi mbalimbali fursa ya kujilinda dhidi ya changamoto za kifedha.

Aidha, ameeleza kuwa usimamizi imara wa soko la bima unachangia kuimarisha sekta nzima ya fedha, kwani uwepo wa kampuni zinazofanya kazi kwa uwazi na ufanisi huongeza imani ya wananchi na wawekezaji katika huduma zinazotolewa.

Atoa msisitizo kuhusu haki za wateja wa bima

Wakati huo huo, Bw. Kosuri amesema, mafanikio ya sekta ya bima hayapaswi kupimwa kwa kuangalia ongezeko la kampuni zinazoendesha shughuli zake au thamani ya biashara pekee, bali yanapaswa pia kuonekana katika namna wananchi wanavyonufaika na huduma hizo.

Amesema, jambo la msingi ni kuhakikisha wateja wanapata huduma kwa urahisi, wanaelewa masharti na haki zao, pamoja na kulipwa madai halali kwa wakati wanapokumbwa na hasara zinazostahili kufidiwa.
Bw. Sabato ameeleza kuwa, sekta ya bima itakuwa na mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Taifa iwapo itajenga imani kwa wananchi, kupunguza vikwazo vya upatikanaji wa huduma na kuhakikisha kampuni za bima zinatimiza wajibu wake kwa wateja.

Vyombo vya habari vyatajwa kuwa wadau muhimu

Akizungumzia nafasi ya vyombo vya habari, Bw. Kosuri amesema, wahariri na waandishi wa habari wana wajibu mkubwa wa kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa bima, aina mbalimbali za huduma zinazopatikana sokoni, haki za wateja na wajibu wa kampuni zinazotoa huduma hizo.

Amesema, vyombo vya habari vinapaswa kutumia nafasi yake kuwasilisha taarifa sahihi zinazowawezesha wananchi kuelewa manufaa ya bima na kufanya maamuzi sahihi wanapochagua huduma zinazokidhi mahitaji yao.

Vilevile, amevitaka kuibua mijadala yenye tija kuhusu mafanikio na changamoto zinazoikabili sekta hiyo ili kusaidia kuboresha huduma, kuimarisha uwajibikaji na kuongeza uaminifu wa wananchi kwa kampuni za bima.

Amesisitiza kuwa, ushirikiano kati ya TIRA na vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha taarifa kuhusu sekta ya bima zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa lugha inayoeleweka.

Bw. Kosuri amesema, bima ni kinga muhimu ya uchumi dhidi ya vihatarishi na nyenzo ya kujenga mazingira salama kwa shughuli za uzalishaji, biashara na uwekezaji.
Ameeleza kuwa, TIRA ina nafasi ya kimkakati katika safari ya Tanzania kuelekea kuwa na uchumi shindani, jumuishi na ustahimilivu ifikapo mwaka 2050, hivyo usimamizi madhubuti wa sekta hiyo pamoja na elimu kwa umma vinapaswa kupewa kipaumbele.

Kikao hicho kiliongozwa na Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo A. Saqware, menejimenti ya TIRA, wahariri na waandishi wa habari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uelewa na ushirikiano kati ya mamlaka hiyo na vyombo vya habari katika kuendeleza sekta ya bima nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here