Serikali yaongeza wodi za watoto wachanga hadi 438 kutoka 14

Na GODFREY NNKO| Dar Es Salaam

SERIKALI imeongeza idadi ya wodi maalumu za kuhudumia watoto wachanga kutoka 14 mwaka 2018 hadi kufikia 438 mwaka 2026, hatua inayolenga kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kuhakikisha wanapata matibabu stahiki karibu na maeneo wanayoishi badala ya kusafirishwa umbali mrefu kutafuta huduma.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Wizara ya Afya wa kuimarisha huduma za afya ya mtoto na mtoto mchanga nchini, hususan kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na wale wanaopata changamoto za kiafya mara baada ya kuzaliwa.

Akizungumza leo Novemba 23, 2026 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa habari kilichoandaliwa na Wizara ya Afya, Mratibu wa Huduma za Afya ya Mtoto katika wizara hiyo, Bi. Naomi Chamhene amesema, ongezeko hilo limewezesha hospitali nyingi za halmashauri kuwa na uwezo wa kuhudumia watoto wachanga wenye mahitaji maalumu.

Amesema, awali huduma hizo zilikuwa zinapatikana katika hospitali chache kubwa nchini, hali iliyosababisha watoto wenye changamoto za kiafya kuhamishwa kutoka vituo walikozaliwa kwenda hospitali nyingine, jambo lililoongeza hatari ya kupoteza maisha wakiwa safarini au muda mfupi baada ya kufikishwa kwenye vituo vya rufaa.

Ameeleza kuwa, kutokana na changamoto hiyo, Serikali iliamua kuanzisha wodi za watoto wachanga katika hospitali za halmashauri ili kuhakikisha huduma zinapatikana karibu na wananchi na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.

Bi. Chamhene amesema, uanzishaji wa wodi hizo umehusisha matumizi ya majengo yaliyokuwepo, ununuzi wa vifaa tiba na dawa, pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya ili kuongeza uwezo wao wa kuwahudumia watoto wachanga wenye changamoto mbalimbali.

Amesema, Serikali sasa inaendelea kuachana na utaratibu wa kutumia baadhi ya majengo yaliyoboreshwa kwa muda na kuanza kujenga wodi maalumu zinazokidhi mahitaji ya huduma za watoto wachanga kutokana na ongezeko la wagonjwa wanaohitaji matibabu.

Katika hatua nyingine, amesema Wizara ya Afya imeimarisha mafunzo ya vitendo kwa watoa huduma kupitia utaratibu wa ushauri na uelekezaji wa kitaalamu wakiwa kazini (on-site clinical mentorship), huku baadhi ya wataalamu wakipelekwa katika hospitali kubwa kujifunza zaidi kuhusu namna ya kuwahudumia watoto wenye changamoto za kiafya.

Ameongeza kuwa, wataalamu hao wameunganishwa kupitia mifumo ya mawasiliano inayowawezesha kupata ushauri wa haraka kutoka kwa madaktari bingwa katika hospitali za rufaa, pale wanapokutana na changamoto zinazohitaji utaalamu wa ziada.

Akizungumzia hali ya vifo vya watoto nchini, Bi. Chamhene amesema, takwimu za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto pamoja na Viashiria vya Malaria Tanzania zinaonesha kuwa vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano vilipungua kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000 kati ya mwaka 2015/16 na 2022.
Amesema, kwa upande wa watoto wachanga, yaani waliozaliwa hadi kufikisha siku 28, vifo vilipungua kutoka 25 hadi 24 kwa kila vizazi hai 1,000 katika kipindi hicho, kiwango ambacho bado kinahitaji juhudi zaidi ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Ameeleza kuwa, Tanzania imejiwekea lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka 24 hadi 12 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2030, huku vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano vikilenga kushuka kutoka 43 hadi 25 kwa kila vizazi hai 1,000.

Amesema, kufikia malengo hayo kunahitaji ushirikiano kati ya wataalamu wa afya, Serikali, jamii na vyombo vya habari katika kuelimisha wananchi kuhusu huduma muhimu za afya ya mtoto.

Huduma maalumu zaimarishwa kwa watoto wachanga

Bi. Chamhene amesema, wizara imeendelea kuimarisha huduma muhimu kwa watoto wachanga zinazojumuisha kuwakausha mara baada ya kuzaliwa, kuwafunika ili kuhifadhi joto la mwili, kuwanyonyesha maziwa ya mama mapema, kuwapa kinga ya macho na chanjo zinazostahili.

Amesema, huduma hizo zinapaswa kutolewa kwa kila mtoto anayezaliwa, bila kujali amezaliwa katika hospitali kubwa, kituo cha afya au zahanati, pamoja na wale wanaozaliwa kabla ya wakati.

Ameeleza kuwa, watoto wanaozaliwa kabla ya kufikisha wiki 37 za ujauzito wanahitaji uangalizi maalumu, ikiwemo kudhibiti joto la mwili, kusaidiwa kupumua na kupatiwa matibabu kulingana na changamoto wanazokabiliana nazo.

Katika msisitizo wa matumizi sahihi ya lugha katika uandishi wa habari, amewataka waandishi kuacha kutumia neno njiti wanapozungumzia watoto waliozaliwa kabla ya wakati, akisema ni muhimu kutumia lugha inayoheshimu utu na kuepuka maneno yanayoweza kuwanyanyapaa watoto hao.

Aidha, amesema Serikali inatekeleza huduma za matibabu jumuishi kwa watoto wenye magonjwa mbalimbali, zinazojulikana kitaalamu kama Integrated Management of Childhood Illness (IMCI), pamoja na ufuatiliaji wa ukuaji na maendeleo ya mtoto ili kubaini mapema changamoto za kiafya na ukuaji.

Amesema, ufuatiliaji huo unahusisha kupima uzito, kuangalia ukuaji wa mwili na maendeleo ya mtoto kulingana na umri wake, hatua inayosaidia wataalamu kubaini mapema matatizo ya lishe na ukuaji.
Serikali yaimarisha uchunguzi wa vifo vya watoto

Katika kuhakikisha vifo vya watoto vinapungua zaidi, Bi. Chamhene amesema, Wizara imeimarisha mfumo wa kupitia na kuchambua vifo vya wajawazito na watoto wachanga unaojulikana kama Maternal and Perinatal Death Surveillance and Response (MPDSR).

Amesema, mfumo huo unasaidia kubaini sababu zilizochangia vifo, kuchunguza mapungufu katika utoaji wa huduma na kuweka hatua za kurekebisha changamoto zilizobainika ili kuzuia matukio kama hayo kujirudia.

Amefafanua kuwa, uchunguzi huo hauishii kuangalia sababu za vifo katika jamii pekee, bali pia huchunguza ubora wa huduma zilizotolewa na wataalamu wa afya, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba pamoja na changamoto zinazoweza kujitokeza katika vituo vya kutolea huduma.

Amesema, hatua hizo zimeambatana na uwekezaji katika vifaa tiba maalumu vinavyohitajika kwa watoto wachanga, wakiwemo wanaohitaji msaada wa kupumua, kudhibiti joto la mwili na matibabu ya manjano kwa kutumia mwanga maalumu.
Chamhene amesisitiza kuwa, ushirikiano kati ya wataalamu wa afya na vyombo vya habari ni muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu huduma za mtoto na mtoto mchanga, akieleza kuwa uelewa sahihi wa masuala hayo utasaidia wazazi kutambua mahitaji ya watoto na kuwapeleka mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here