Serikali yatangaza mafanikio makubwa Afya ya Uzazi: Wanaojifungulia vituoni ni asilimia 81, vifo vyashuka

Na GODFREY NNKO| Dar es Salaam

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kuongeza idadi ya wanawake wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya hadi kufikia asilimia 81, kutoka kiwango cha chini kilichokuwepo awali, huku idadi ya wanaojifungulia nyumbani ikipungua kutoka asilimia 47 mwaka 2022 hadi asilimia 18, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za afya ya uzazi na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi nchini.
Fidea Obimbo kutoka Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Wizara ya Afya ameyasema hayo leo Novemba 23, 2026 katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa habari kilichoandaliwa na Wizara ya Afya jijini Dar Es Salaam

Bi. Obimbo amesema, maboresho ya huduma za uzazi salama yamechangia kuimarika kwa upatikanaji wa huduma kwa wajawazito kabla, wakati na baada ya kujifungua.

Amesema, hatua nyingine iliyopigwa ni kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, huku Serikali ikiweka lengo la kufikisha kiwango hicho kwenye vifo 70 ifikapo mwaka 2030.

Pia, amesema mafanikio hayo yametokana na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma, kuwafikia wananchi katika ngazi ya jamii na kuongeza ufanisi wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.

Ameeleza kuwa, idara hiyo ina maeneo makuu mawili, ambayo ni afya ya uzazi na afya ya mtoto.

Upande wa mama unahusisha huduma za uzazi salama, uzazi wa mpango, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti, kuzuia maambukizi ya VVU, kaswende na homa ya ini kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, pamoja na huduma za kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wa mtoto, huduma zinazotolewa zinajumuisha afya ya mtoto mchanga, watoto na vijana, huku kila eneo likiwa na wataalamu wanaosimamia utekelezaji wa majukumu yake kwa lengo la kuongeza ubora na ufanisi wa huduma.

Bi. Odimbo amesema, Serikali imeendelea kuboresha huduma za kliniki kwa wajawazito kwa kuweka utaratibu wa mahudhurio yasiyopungua mara nane katika kipindi cha ujauzito, huku akisisitiza umuhimu wa mama kuanza kliniki kabla ya kufikisha wiki 12 za ujauzito.

Amesema, katika kliniki hizo wajawazito hufanyiwa vipimo mbalimbali, ikiwemo uchunguzi wa upungufu wa damu, VVU, kaswende, kisukari na kundi la damu, pamoja na kupatiwa virutubisho vya madini ya chuma na foliki asidi vinavyosaidia afya ya mama na ukuaji wa mtoto.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa wenza kushiriki katika huduma za kliniki ili kuongeza uelewa kuhusu afya ya mama na mtoto, huku akibainisha kuwa wanawake wanaruhusiwa kuambatana na mtu wanayemwamini ili kuwasaidia kuelewa na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.

Ameongeza kuwa, Serikali imeimarisha huduma zinazozingatia utu, heshima na mahitaji ya wajawazito, pamoja na kupanua huduma rafiki kwa vijana zinazolenga kuwajengea uwezo wa kujitambua, kufanya maamuzi sahihi na kuwajibika katika masuala ya afya.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali imeimarisha huduma za usafiri wa dharura kupitia mfumo wa M-Mama, unaowezesha wajawazito na wanawake wanaokabiliwa na changamoto wakati wa kujifungua au baada ya kujifungua kusafirishwa kutoka maeneo ya jamii kwenda vituo vya afya kwa wakati.

Amesema, pia matumizi ya mifumo ya kidijitali yameboresha uratibu wa huduma kuanzia ngazi ya jamii hadi hospitali, ikiwemo mifumo ya UCS na GoT-HoMIS inayosaidia usimamizi wa taarifa za wagonjwa, utoaji wa rufaa na ufuatiliaji wa huduma wanazopata.

Kuhusu udhibiti wa vifo vya wajawazito na watoto wachanga, Bi. Odimbo amesema, Wizara imeimarisha utaratibu wa kupitia na kuchambua vifo hivyo kupitia mfumo wa MPDSR, unaowezesha wataalamu na viongozi wa Serikali kujadili sababu za vifo na kuweka mikakati ya kuzuia matukio kama hayo kujirudia.

Amewataka wananchi, hususan wanawake wanaopanga kupata ujauzito, kuzingatia maandalizi ya kiafya kabla ya kubeba mimba, kuanza kliniki mapema na kufuata ushauri wa wataalamu ili kulinda afya zao na za watoto wao.

Amesisitiza kuwa, ushirikiano kati ya Serikali, jamii na vyombo vya habari ni muhimu katika kuelimisha wananchi kuhusu uzazi salama na kuhakikisha kila mama anapata huduma bora katika hatua zote za ujauzito na kujifungua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here