ANTALYA, UTURUKI- Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Kampuni ya IC & Holding ya nchini Uturuki kando ya Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) unaofanyika jijini Antalya nchini Uturuki kuanzia tarehe 9 hadi 20 Novemba, 2026, ambapo pamoja na mambo mengine walijadili fursa za uwekezaji wa Kimkakati katika Miundombinu na Viwanda.
Mazungumzo hayo yalilenga kutumia utaalamu wa Kituruki kuchochea ukuaji wa kiuchumi nchini Tanzania kupitia ushirikiano wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public-Private Partnerships-PPP).
Aidha, walijadili maendeleo ya viwanda, ambapo Menejimenti ya IC & Holding ilisisitiza historia ya miaka 50 ya nchi yao ya kusimamia kwa mafanikio maeneo ya viwanda katika kila mji, wakibainisha kwamba mtindo huo unaweza kubadilishwa ili kufaa Tanzania na kutumia viwanda kama kichocheo cha maendeleo ya uchumi.

Suala la miundombinu lilijitokeza kama eneo muhimu la uwekezaji ikiwemo sekta za madini, kilimo, maji, na nishati, ambapo msisitizo maalum uliwekwa kwenye usafiri, huku ikielezwa kuwa barabara sita tayari zimetengwa nchini Tanzania kwa ajili ya miradi ya Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, na Miradi miwili kati ya hiyo tayari imefanyiwa utafiti wa kina, na ziara za kutembelea maeneo zinapangwa ili kuchunguza zaidi fursa hizo.
Mhe. Balozi Omar alisisitiza kuwa Tanzania ni soko imara na salama ndani ya kanda na pande zote zimekubaiana kuendeleza mazungumzo zaidi kwa kuhusisha Wizara za Kisekta na Kampuni hiyo ili kuchambua zaidi namna ya kushirikiana pamoja na kutembelea maeneo ya miradi ili kupata taarifa zaidi.Kampuni ya IC & Holding ilianzishwa mnamo mwaka 1969 na ni kampuni kubwa yenye matawi mbalimbali duniani ikijihusisha zaidi na masuala ya ujenzi wa miundombinu, Nishati, Utalii, na sekta ya ujenzi.



