Tanzania na Norway zafanya Awamu ya Nne ya Mashauriano ya Kisiasa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia

OSLO, NORWAY- Tanzania na Norway zimethibitisha dhamira yao ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kupanua ushirikiano wa kiuchumi na kuongeza ushirikiano katika masuala ya kikanda na kimataifa wakati wa Awamu ya Nne ya Mashauriano ya Kisiasa kati ya Tanzania na Norway, iliyofanyika jijini Oslo, Norway, tarehe 18 Novemba 2026.
Mashauriano hayo yameongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), kwa kushirikiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Mhe. Espen Barth Eide.

Mazungumzo yao yamejikita katika kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili, ushirikiano wa kiuchumi, biashara na uwekezaji, ushirikiano wa maendeleo, amani na usalama wa kikanda pamoja na ushirikiano katika majukwaa ya kimataifa.
Katika eneo la ushirikiano wa kiuchumi, Mawaziri hao wamejadili fursa zilizopo katika sekta za nishati jadidifu, gesi asilia iliyosindikwa (LNG), kilimo, usalama wa chakula, uchumi wa buluu, teknolojia za kidijitali na ufadhili wa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuelekea kwenye ushirikiano unaojikita zaidi katika uwekezaji badala ya misaada ya maendeleo, kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku ikitambua mchango wa muda mrefu wa Norway katika maendeleo ya nchi.
Aidha, Mawaziri hao wamebadilishana mawazo kuhusu maendeleo ya kisiasa, amani na usalama wa kikanda, umuhimu wa kutumia suluhu za Kiafrika kutatua changamoto za kikanda, pamoja na ushirikiano wa kimataifa kupitia Umoja wa Mataifa.
Tanzania pia imeialika Norway kushiriki Awamu ya Tano ya Mashauriano ya Kisiasa itakayofanyika nchini Tanzania mwaka 2027. 

Awamu ya Tatu ya Mashauriano ya Kisiasa kati ya Tanzania na Norway ilifanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania, Januari 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here