MARRAKECH, MOROCCO NOVEMBA 23, 2026- Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Crispin Francis Chalamila, ameshiriki na kutoa hotuba ya ufunguzi katika Mkutano wa Afrika kuhusu Uwazi katika Taasisi za Uadilifu na Kupambana na Rushwa (African Meeting on Open Integrity and Anti-Corruption Institutions), unaofanyika jijini Marrakech, nchini Morocco.
Mkutano huo unalenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa taasisi za uadilifu na kupambana na rushwa barani Afrika, pamoja na kuanzisha Muungano wa Afrika wa Taasisi za Uadilifu na Kupambana na Rushwa zilizo wazi (African Alliance of Open Integrity and Anti-Corruption Institutions).
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Bw. Chalamila ameipongeza Serikali ya Morocco na Mamlaka ya Kitaifa ya Uadilifu, Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Morocco (NAPPFC) kwa kuanzisha mpango huo muhimu unaolenga kuimarisha ushirikiano wa taasisi za Afrika katika mapambano dhidi ya rushwa.
Amesisitiza kuwa, rushwa bado ni moja ya changamoto kubwa zinazokwamisha maendeleo endelevu, utawala bora na imani ya wananchi kwa taasisi za umma barani Afrika, hivyo, ameeleza umuhimu wa taasisi za kupambana na rushwa kuimarisha mifumo ya kuzuia, kubaini na kushughulikia vitendo vya rushwa kwa kutumia mbinu za kisasa na shirikishi.
Akizungumzia umuhimu wa kuanzishwa kwa Muungano wa Afrika wa Taasisi za Uadilifu na Kupambana na Rushwa zilizo wazi, Bw. Chalamila amesema kuwa, muungano huo unapaswa kuwa jukwaa la ushirikiano wa vitendo, kujifunza kutoka kwa kila mmoja, kusaidiana kitaalamu na kuandaa mipango madhubuti inayozingatia mazingira na vipaumbele vya nchi za Afrika.
Ameongeza kuwa, kupitia muungano huo, nchi za Afrika zitapata fursa ya kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu badala ya kila taasisi kutekeleza juhudi zake peke yake.
Bw. Chalamila ametoa wito kwa washiriki wa mkutano huo kuwa na mshikamano na dhamira ya pamoja katika kuhakikisha majadiliano yanazaa hatua na matokeo yanayoonekana katika kuimarisha taasisi za uadilifu na mapambano dhidi ya rushwa barani Afrika.
Pia ametumia fursa hiyo kueleza kaulimbiu ya TAKUKURU isemayo “PREVENTING CORRUPTION IS OUR RESPONSIBILITY; LET'S PLAY OUR PART” (Kuzuia Rushwa ni Jukumu Letu; Kila Mmoja Atimize Wajibu Wake), akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji umiliki wa pamoja, uwajibikaji wa kila mmoja na ushiriki hai wa wananchi.
Mkutano huo unatoa fursa muhimu kwa taasisi za Afrika kuimarisha ushirikiano katika kujenga mifumo ya uwazi, uwajibikaji na uadilifu, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi za umma.
...Kuzuia Rushwa ni Jukumu Letu; Kila Mmoja Atimize Wajibu Wake...

