Mwinjilisti Temba ashauri Kwala iwe kitovu cha malori kuiokoa Dar es Salaam

DAR ES SALAAM- Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Dkt. Alphonce Boniface Temba ameitaka Serikali kubadili mwelekeo wa mipango ya maendeleo ya miundombinu jijini Dar es Salaam kwa kuimarisha uwekezaji katika maeneo ya pembezoni mwa jiji, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza msongamano wa magari, kuondoa shughuli za malori katikati ya jiji na kuweka msingi wa maendeleo endelevu ya mkoa huo.
Dkt. Temba ametoa rai hiyo leo Novemba 8, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila za kutaka kurejesha hadhi ya jiji hilo.

Dkt. Temba amesisitiza umuhimu wa Serikali kuwashirikisha wadau mbalimbali katika kupanga na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ili kupata mawazo mbadala yatakayosaidia kuzuia changamoto zinazoweza kujitokeza baadaye.

MIPANGO IWE YA MUDA MREFU 

Amesema, pamoja na kutambua juhudi zinazofanywa na Mkuu huyo wa Mkoa katika kuboresha miundombinu na sura ya jiji, ni muhimu mipango inayotekelezwa isiishie katika kutatua changamoto za sasa pekee, bali izingatie pia mahitaji ya miaka 20, 30 na hata 50 ijayo.

Ameeleza kuwa, baadhi ya miradi inayopangwa au kutekelezwa kwa haraka bila majadiliano ya kutosha na wadau inaweza kuleta gharama kubwa za kiuchumi na kijamii, hasa pale inapobainika baadaye kuwa kulikuwa na njia mbadala zenye ufanisi zaidi.

Ni vizuri viongozi wakasikiliza zaidi kabla ya kuanza kupanga na kutekeleza miradi. Kuna Watanzania wenye mawazo na uzoefu unaoweza kusaidia kuboresha mipango ya maendeleo. Hata kama mpango unaonekana mzuri kwa wakati huu, ni muhimu kuangalia athari zake kwa miaka mingi ijayo.
Akifafanua hoja yake, amesema aliwahi kuwasiliana na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ili kuona namna ya  kuhairishwa ujenzi wa Fly Over ya SGR toka Buguruni hadi Posta ili ikaanzie  Pungu Station.

Lakini, Waziri akasema ni mawazo mazuri sana, lakini nimechelewa kwani mkandarasi alikuwa amekwishasaini mkataba na kusitisha wangelipa gharama kubwa ni bora ujenzi uendelee.

Amesema, alipendekeza mfumo huo uhusishe maeneo kama Pugu, Kwala ili wananchi wanaotoka maeneo mbalimbali ya jiji yakiwemo Kimara, Temeke na Mbagala, waweze kupata huduma za usafiri na usafirishaji bila kulazimika kuingia katikati ya jiji kisha kurudi tena katika maeneo ya nje.

Dkt. Temba amesema, Profesa Mbarawa alimweleza kuwa, wazo hilo lingekuwa na nafasi kubwa ya kuzingatiwa iwapo lingewasilishwa mapema, kabla ya Serikali kuingia katika mikataba ya utekelezaji wa mradi husika, akibainisha kuwa kubadili mipango baada ya kuanza kwa kazi kungeongeza gharama.

KUMBUKUMBU MUHIMU 
Aliyekuwa Rais wa Zambia, Hayati Michael Sata (kushoto), akiwa ameshikana mkono na kuombewa na Mwinjilisti wa Kimataifa, Dkt. Alphonce Temba, walipokutana Ikulu ya Lusaka nchini humo kwa ajili ya sala maalumu ya toba na kuliombea taifa hilo mara baada ya kiongozi huyo kuingia madarakani. Rais Sata alimwalika Dkt. Temba kwa ajili ya ushauri maalum ili kustawisha uchumi na kuunganisha Taifa kuwa na hofu ya Mungu. Dkt. Temba mwaka 2012 alimshauri Rais Sata kuhusu maboresho ya Mpaka wa Nakonde kupitia mapambano dhidi ya rushwa, kuimarisha usalama na uboreshaji wa miundombinu ya awali ya forodha na hatua zikachukuliwa, na maombi yake yaliwezesha timu ya Taifa kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka huo.

Aidha, amesema miradi mikubwa ya miundombinu huchukua muda mrefu kukamilika, hivyo ni muhimu maamuzi yake yafanywe kwa kuzingatia mahitaji ya baadaye badala ya kutegemea suluhisho za dharura zinazoweza kushindwa kuondoa chanzo halisi cha tatizo.

CHANGAMOTO SI MAEGESHO DAR

Katika maelezo yake, Dkt. Temba amesisitiza kuwa changamoto kubwa ya usafiri Dar es Salaam si eneo la maegesho ya magari pekee, bali ni ongezeko la magari yanayoingia na kupita katikati ya jiji, hususan malori yanayohudumia shughuli za bandari na biashara.

Amesema, kuendelea kuruhusu malori mengi kuingia jijini bila kuwa na mfumo madhubuti wa kuyapokea, kuyahifadhi na kuyasafirisha nje ya maeneo ya makazi na biashara kutaendelea kuongeza msongamano, hata kama Serikali itaongeza idadi ya barabara.

Pia, ametaja uwepo wa maelfu ya malori jijini kuwa changamoto inayohitaji suluhisho la muda mrefu, akipendekeza shughuli za kupokea, kuhifadhi na kusambaza mizigo zihamishiwe katika maeneo maalumu nje ya jiji.

Katika kutatua changamoto hiyo, amependekeza eneo la Kwala mkoani Pwani, liendelezwe kuwa kitovu kikubwa cha shughuli za usafirishaji na ugavi wa mizigo, kwa kujengwa miundombinu ya kisasa ya kuhifadhi na kusambaza mizigo, pamoja na kuimarisha uhusiano wake na mfumo wa reli.

Amesema, Kwala ina ardhi kubwa inayoweza kutumika kwa shughuli za kiuchumi na viwanda, hivyo kuendelezwa kwake kutasaidia kupunguza utegemezi wa Dar es Salaam kama eneo kuu la kupokea na kuhifadhi malori na mizigo.

Dkt. Temba ameongeza kuwa, maeneo yanayozunguka Kwala yakiwemo Magindu, Mpera Mumbi, Ng'wale, Chaua, Msolwa na Ngerengere , yanaweza kutumiwa kupanua uwekezaji wa viwanda, maghala na huduma nyingine za usafirishaji.

Kwa mtazamo wake, kuhamishia shughuli hizo nje ya Dar es Salaam kutasaidia kupunguza msongamano wa magari makubwa, kuongeza fursa za ajira kwa wananchi wa maeneo hayo na kuchochea ukuaji wa miji mipya ya kiuchumi.

RELI IIMARISHWE ENEO LA KWALA

Dkt. Temba amesisitiza pia umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya reli ya umeme katika eneo la Kwala ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli, hatua ambayo amesema inaweza kupunguza utegemezi wa malori katika kusafirisha mizigo kwenda na kutoka jijini.

Vilevile, amependekeza Serikali kushirikiana na wawekezaji wenye maeneo makubwa ya ardhi, akitolea mfano eneo la Tumbi na mashamba yanayohusishwa na mwekezaji Mohammed Dewji (Mo), ambayo kwa maelezo yake yanaweza kuendelezwa kwa shughuli za viwanda, kilimo na vituo vya usafirishaji.

Amesema, maeneo hayo yana nafasi ya kuwa sehemu muhimu ya upanuzi wa shughuli za kiuchumi kutokana na ukaribu wake na Dar es Salaam pamoja na kupitiwa na miundombinu ya reli, hivyo ni muhimu Serikali kufanya mazungumzo na wamiliki wa ardhi ili kubaini uwezekano wa kuyatumia kwa manufaa mapana ya umma.

Katika hatua nyingine, amependekeza ujenzi wa barabara mpya zinazounganisha maeneo ya Kisarawe, Mzenga, Vihingo, Ruvu, Kwala na Ngerengere, akieleza kuwa maeneo hayo yana ardhi inayoweza kuendelezwa kwa uwekezaji wa viwanda, vituo vya mizigo na makazi mapya.

Amesema, kuimarisha miundombinu katika maeneo hayo kutarahisisha uhamishaji wa baadhi ya shughuli za kiuchumi kutoka katikati ya Dar es Salaam na kutoa fursa kwa wananchi na wawekezaji kuanzisha shughuli mpya nje ya jiji.

Aidha, ameshauri Tanzania kuimarisha udhibiti wa magari chakavu yanayoingizwa nchini, akitolea mfano wa baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika ambazo, kwa maelezo yake, zina masharti makali kuhusu magari yaliyotumika, ubora wake na namna yanavyosafirishwa kuvuka mipaka. 

Dkt. Temba amesema, kwa Afrika Kusini ukiagiza gari lililotumika nje likapita kwao, utalazimika kulibeba bila kulishusha popote hadi huko mipakani, lengo likiwa ni kudumisha ubora wa magari yanayotumika nchini humo, jambo ambalo limefanikiwa kwa mataifa mengi ya Kusini mwa Afrika.

Tofauti na hapa nchini, ambapo magari yanayoingizwa kupitia bandarini na kupata kibali yanaanza kutumika au kupelekwa kwenye yadi bila kuchunguzwa ubora wake, hivyo kusababisha ajali nyingi nchini kutoka na na ubora hafifu.

Umuhimu wa Jeshi la Polisi kuanzisha kitengo maalum cha kuchunguza magari yanayoingizwa nchini ili kubaini ubora haukwepeki. Ikizingatiwa kuwa, sasa hivi Serikali inakwenda kujenga barabara ya kisasa kwa ajili ya kulipia ambayo magari, ambayo hayana ubora yatasababisha maafa zaidi kwa sababu yatakuwa yanatembea kwa spidi kubwa.

Amesema, ni muhimu kuwepo kwa mifumo madhubuti ya ukaguzi na udhibiti wa ubora wa magari yanayoingia nchini ili kuzuia magari yasiyokidhi viwango kuendelea kutumika barabarani na kuongeza changamoto za usalama na msongamano.
Zaidi ya vijiji 34 vimejumuishwa katika Mradi wa Bandari Kavu ya Kwala.

Dkt. Temba amesisitiza kuwa, mustakabali wa Dar es Salaam haupaswi kutegemea kuongeza barabara na maeneo ya maegesho pekee, bali unahitaji mkakati mpana wa kupunguza shughuli zinazozalisha msongamano, kuendeleza vituo vipya vya kiuchumi nje ya jiji na kuimarisha usafiri wa reli.

MAAMUZI YANAYOFANYWA SASA

Amesema, maamuzi yanayofanywa sasa ndiyo yatakayobainisha namna Dar es Salaam itakavyokuwa katika miongo ijayo, hivyo amewataka viongozi kuzingatia ushauri wa wadau na kufanya maamuzi yanayolinda maslahi ya taifa kwa muda mrefu.

Vilevile, amemuomba Mungu kuwaongoza viongozi kupata ufahamu na busara katika kupanga maendeleo ya jiji hilo, akisisitiza kuwa mafanikio ya mipango ya sasa yatapimwa pia kwa namna yatakavyosaidia vizazi vijavyo.

Wakati huo huo, Mwinjilisti Dkt. Temba alikumbuka alivyoishauri Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambapo mwaka 2008 alimwandikia barua na kumshauri Waziri Mkuu wa kipindi kile, Mheshimiwa Mizengo Pinda kuhusu kuhamisha mzani wa Maili Moja kuhamishiwa Vigwaza na kujengwa kwa Bandari kavu ya Kwala jambo ambalo lilipelekwa bungeni na zaidi ya shilingi bilioni 15 zilitengwa na kutumika kabla ya maboresho yalioongezwa.

Aidha, kwa sasa Bandari kavu ya Kwala imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 90 kujengwa, Dkt. Temba amesema, sababu ya kumshauri kipindi kile ni tatizo la foleni toka Maili moja Kibaha mpaka Ubungo, wakati mwingine kuchukua mpaka saa tano na mpaka kusababisha magari saba Mbezi kulipuka, mpaka sasa eneo hilo linajulikana kama Magari saba.

Vilevile, Mwinjilisti Dkt. Temba alitolea mfano kauli ya RC Chalamila ya kupiga marufuku maeneo ya pembezoni mwa barabara ya Morogoro (Morogoro Road) kuwa na maegesho holela, amesema kuwa haya ni mambo ya muda mfupi.

Mfano ni kwa yeye mwenyewe (RC Chalamila) kusitisha vibali vya mabasi kuwa na vituo Shekilango mpaka Magomeni na kuamuru kurudi Mbezi Luis katika Stendi ya Magufuli, hilo litategemea  Rais ajaye utashi wake na ana mtazamo gani, kwani naye anaweza kuelekeza malori yaishie Kwala na wengi kupata hasara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Shalom Mtumishi....
    Na mimi nina Wazo linaloendana na huo mpango.
    Badala ya kujenga Bypass barabara mpya itakayoanzia Kigamboni kama ilovyopendekezwa na Mkoa wa DSM, wazo hilo ni Zuri lakini linaweza kuboreshwa kama ifuatavyo.
    .Kwanza Mji wa Dar Es Salaam hauhitaji bypass ,bali unahitaji HALF RING ROAD ,Hii inaweza anzia Mkoa wa pwani Maili Moja kuelekea Bagamoyo Baobao hadi Baharini kwa upande mmoja,
    Then Upande wa pili ikaenda Kisarawe,Kuelekea Chanika ,Mkuranga ,Vikindu hadi Buyuni Pembamnazi Kigamboni...hii ina faida nyingi zaidi.
    Sasa pale inapocross SGR inatengenezwa na kuimarishwa zile barabara za Mkandarasi wa SGR ambayo ipo tayari na inapitika hata sasa hiyo inaenda sambamba na Reli mpaka mwisho, hapo unapata hata Lanes 3 kwenda na 3 kurudi.
    Lane moja inakuwa Dedicated kwa malorry na Lanes 2 zinatumika kwa Intercity ,Yaani mkoa hadi mkoa kwa ajiri ya Mabus.
    kisha unajenga fly overr kwenye kila mji inakopita barabara hiyo.

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here