TMA yatoa angalizo la mvua kubwa mikoa 9, huu hapa utabiri kwa Novemba 17, 2026

Na DIRAMAKINI 24 | Dar es Salaam

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo la mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi, kuanzia usiku wa leo Novemba 16, 2026.
Katika utabiri wake wa saa 24 zijazo kwa Novemba 17, 2026 mamlaka hiyo imewataka wakazi wa maeneo yatakayoathirika kuchukua tahadhari, kufuatia uwezekano wa makazi kuzungukwa na maji.

Maeneo yatakayonyesha mvua kubwa

Kwa siku ya leo, angalizo limetolewa kwa maeneo machache ya mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma na kusini mwa Mkoa wa Morogoro.

Hata hivyo, kuanzia kesho Jumanne, tarehe 17 Novemba 2026, mvua hiyo inatarajiwa kuenea zaidi. Maeneo yatakayoathirika ni mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe, Rukwa, Katavi, Tabora, Kigoma na Shinyanga.

TMA imesema, uwezekano wa mvua hiyo kutokea ni wa wastani, huku kiwango cha athari zinazoweza kujitokeza nacho kikiwa cha wastani. Athari kubwa inayohusishwa na mvua hiyo ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji.

Kwa siku za Jumatano hadi Ijumaa, kuanzia tarehe 18 hadi 20 Novemba 2026, Mamlaka hiyo imesema hakuna tahadhari yoyote ya hali mbaya ya hewa.

Hali ya hewa kwa mikoa mingine

Kwa upande wa mikoa ya Morogoro Kusini na Ruvuma, hali inayotarajiwa ni ya mawingu, mvua na ngurumo katika maeneo machache, pamoja na vipindi vifupi vya jua.

Mikoa ya Singida, Kigoma, Tabora na Katavi, pamoja na Rukwa, Iringa, Njombe, Songwe na Mbeya, inatarajiwa kuwa na hali kama hiyo ya mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache, na vipindi vya jua.

Visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na mikoa ya Tanga na Dar es Salaam, inatarajiwa kuwa na mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache, na vipindi vya jua.

Mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro, pamoja na Dodoma na Morogoro Kaskazini, Pwani ikijumuisha Visiwa vya Mafia, pamoja na Kagera, Mara, Simiyu, Shinyanga, Mwanza na Geita, pamoja na Mtwara na Lindi, inatarajiwa kuwa na mawingu kiasi, mvua nyepesi katika maeneo machache na vipindi vya jua.

Viango vya joto kwa miji mikubwa

Mamlaka imeeleza kuwa, joto la juu zaidi linatarajiwa kuwa nyuzi 32 katika miji ya D'Salaam na Dodoma, likifuatiwa na nyuzi 31 Zanzibar, nyuzi 30 Kigoma, nyuzi 29 Mwanza, nyuzi 28 Tabora, nyuzi 27 Arusha, Iringa na Mbeya, nyuzi 25 Tanga na nyuzi 24 Njombe.
Kwa upande wa joto la chini, mji wa Njombe unatarajiwa kuwa na nyuzi 12, Iringa nyuzi 15, Mbeya nyuzi 15, Arusha nyuzi 17, Dodoma nyuzi 17, Tabora nyuzi 20, Kigoma nyuzi 20, Mwanza nyuzi 19, D'Salaam nyuzi 21, Tanga nyuzi 23 na Zanzibar nyuzi 23.

Upepo na hali ya bahari

Kuhusu upepo wa Pwani, unatarajiwa kuvuma kutoka Mashariki kwa kasi ya kilomita 30 kwa saa kwa Pwani yote. Wakati huo huo, hali ya bahari inatarajiwa kuwa na mawimbi makubwa kiasi.

Ushauri kwa Wananchi

TMA imewataka wananchi katika maeneo yaliyotajwa kuzingatia angalizo hilo na kujiandaa ipasavyo, ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here