NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo la mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha katika maeneo machache ya mikoa 20 kuanzia leo Alhamisi, Novemba 12, 2026 huku ikiwataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza, ikiwemo makazi kuzungukwa na maji.
Kwa mujibu wa utabiri wa saa 24 zijazo kuanzia saa 3:00 usiku wa leo, mikoa ya Dodoma na Singida, Manyara, Arusha na Kilimanjaro, pamoja na Kagera, Simiyu, Shinyanga, Mara, Mwanza na Geita, inatarajiwa kupata hali ya mawingu, mvua na ngurumo katika baadhi ya maeneo, na vipindi vifupi vya jua.
Hali kama hiyo ya mawingu, mvua na ngurumo katika maeneo machache na vipindi vifupi vya jua inatarajiwa pia katika mikoa ya Morogoro, Kigoma, Tabora na Katavi, pamoja na Rukwa, Iringa, Njombe, Songwe na Mbeya.
Kwa upande wa Pwani, mikoa ya Unguja na Pemba, Tanga na Dar es Salaam, Ruvuma, Mtwara na Lindi, pamoja na Mkoa wa Pwani ukiwemo Visiwa vya Mafia, inatarajiwa kuwa na hali ya mawingu kiasi, mvua na ngurumo katika maeneo machache na vipindi vifupi vya jua.
Tahadhari ya siku tatu
Katika matarajio ya hali mbaya ya hewa kwa siku tatu, TMA imetoa angalizo la mvua kubwa leo Alhamisi kwa maeneo machache ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Kigoma, Tabora, Katavi, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa na Njombe.
Uwezekano wa kutokea ni wastani, huku kiwango cha athari zinazoweza kutokea kikiwa wastani. Athari kuu inayotarajiwa ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji.
Ijumaa, Novemba 13, 2026, hali inatarajiwa kuwa kali zaidi. TMA imetoa tahadhari ya mvua kubwa kwa maeneo machache ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa na Njombe.
Uwezekano wa kutokea ni wastani, lakini kiwango cha athari zinazoweza kutokea ni kikubwa.
Jumamosi, Novemba 14, 2026, angalizo la mvua kubwa limetolewa kwa maeneo machache ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Rukwa, Kigoma, Tabora na Katavi.
Uwezekano wa kutokea ni wastani, kiwango cha athari ni wastani, na athari inayotarajiwa ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji.
Jumapili, Novemba 15, 2026, angalizo la mvua kubwa limetolewa kwa maeneo machache ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma, Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma.
Uwezekano wa kutokea ni wastani, kiwango cha athari ni wastani, na athari inayotarajiwa ni baadhi ya makazi kuzungukwa na maji.
Jumatatu, Novemba 16, 2026, hakuna tahadhari iliyotolewa.
Aidha, kwa siku ya leo, TMA imetoa angalizo la vipindi vifupi vya mvua kubwa vinavyotarajiwa katika maeneo machache ya mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma, ambapo athari inayotarajiwa ni mafuriko kuathiri baadhi ya maeneo. Wananchi katika maeneo hayo wametakiwa kuchukua tahadhari.
Joto, mawio na machweo ya jua
Kwa mujibu wa TMA, viwango vya juu vya joto vinatarajiwa kufikia nyuzi joto 32 katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Tabora na Tanga, huku Arusha ikitarajiwa kufikia nyuzi 28, Kigoma nyuzi 30, Mbeya nyuzi 27, Iringa nyuzi 31, Njombe nyuzi 25, Mwanza nyuzi 30 na Zanzibar nyuzi 31.
Viwango vya chini vya joto vinatarajiwa kuwa nyuzi 21 Dar es Salaam, nyuzi 17 Dodoma, nyuzi 15 Arusha, nyuzi 20 Kigoma na Tabora, nyuzi 15 Mbeya, nyuzi 15 Iringa, nyuzi 12 Njombe, nyuzi 19 Mwanza na nyuzi 23 Tanga na Zanzibar.
Hali ya bahari
Upepo wa Pwani unatarajiwa kuvuma kutoka Mashariki kwa kasi ya kilomita 30 kwa saa kwa Pwani ya Kaskazini, na kutoka Kaskazini Mashariki kwa kasi ya kilomita 20 kwa saa kwa Pwani ya Kusini. Hali ya Bahari inatarajiwa kuwa ya mawimbi madogo hadi makubwa kiasi.
Aidha, utabiri huo umetolewa leo Novemba 12, 2026, ambapo TMA imeongeza kuwa, vipindi vya mvua vinaweza kuongezeka katika maeneo mengi ya nchi. Mamlaka hiyo imewataka wananchi kuzingatia taarifa rasmi na kujiandaa ipasavyo.



