NA GODFREY NNKO
WAANDISHI wa habari nchini wameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuendelea kuwajengea uwezo na kutoa mafunzo ya kitaaluma kuhusu namna ya kuripoti taarifa za uchumi na sekta ya fedha kwa ufanisi zaidi.
Pongezi hizo zimetolewa leo Novemba 4, 2026 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Semina ya Waandishi wa Habari za Uchumi na Fedha 2026, Bw. Alfred Zackaria wakati wa semina hiyo iliyoandaliwa na BoT.
Ni kwa ajili ya waandishi wa habari, yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kuchambua na kuripoti takwimu, taarifa na ripoti mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na benki hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya waandishi wa habari wanaoshiriki mafunzo hayo, Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa, elimu inayotolewa na BoT itawasaidia kuandaa na kufikisha taarifa sahihi na za kina kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
"Kama ilivyo methali inayosema 'ukimwelimisha mwanamke umeelimisha jamii', katika muktadha wa utendaji wa nchi, ukimwelimisha mwanahabari basi umeelimisha nchi nzima," amesema Bw, Alfred Zakaria.
Ameongeza kuwa, semina hizo zimekuwa fursa nzuri ya kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa karibu kati ya wanahabari na watumishi wa BoT, hususan Kitengo cha Mawasiliano, jambo linalorahisisha upatikanaji wa taarifa na ufafanuzi pale unapohitajika.
Kadhalika, waandishi wa habari wameishukuru BoT kwa kuwa wasikivu na kufanyia kazi mapendekezo waliyoyatoa katika mikutano ya awali, ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wa kuripoti ripoti za kila mwezi, robo mwaka, nusu mwaka na za mwaka mzima (Monthly, Quarterly, Mid-year, na Annual Reports).
Hata hivyo, wanahabari wameiomba Benki Kuu kuendelea kuimarisha ushirikiano huo kupitia fursa za mahojiano maalum (exclusive interviews) na vyombo vya habari vya magazeti, redio, televisheni, vyombo vya habari vya mtandaoni (Online Media), pamoja na redio za kijamii na mikoani (Local Radios).Katika semina hiyo ya siku tatu, wataalamu wabobezi kutoka BoT wanawasilisha mada mbalimbali ikiwemo Utekelezaji wa Sera ya Fedha kwa Kutumia Riba ya Benki Kuu, Kielelezo cha Faida Rejea ya Dhamana za Serikali na Mchango Wake katika Kuimarisha Uwazi wa Masoko ya Fedha, Namna BoT inavyosimamia mifumo ya malipo nchini.
Mada nyingine ni Jinsi Benki Kuu ya Tanzania Inavyosimamia Sekta ya Fedha, Jinsi Mfumo wa Dhamana ya Mikopo Unavyofanya Kazi na Wigo Wake wa Kisheria, Utambuzi wa alama za usalama katika noti na utunzaji bora wa noti.
Pia, kuna mada ya Jinsi Benki Kuu Inavyotumia Mfumo wa SEMA NA BoT katika Kulinda Watumiaji wa Huduma za Fedha, Jinsi ya Kubaini na Kuandaa Habari Zinazotumia Takwimu kutoka katika Ripoti na Taarifa za Benki Kuu ya Tanzania ikiwemo Maoni na ushauri kwa Benki Kuu.
