Watuhumiwa 165 wakamatwa kwa makosa mbalimbali Mkoa wa Kipolisi Rufiji

PWANI- Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji limeendelea na operesheni na misako katika kuimarisha ulinzi na usalama kwa kushirikiana na jamii katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu.
Katika kipindi cha Oktoba 1, 2026 hadi Oktoba 31, 2026 wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 165 wa makosa mbalimbali yakiwemo unyang'anyi, wizi, uvunjaji kupatikana na nyara za Serikali.

Vilevile, kupatikana na mali zidhaniwazo za wizi, kupatikana na dawa za kulevya, wizi pamoja na pombe ya moshi (gongo).

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Protas Mutayoba.

Oktoba 11, 2026 tuliwakamata watuhumiwa watano ambao ni Salim Rashid Mofack (27) mkazi wa Mbezi Msufini 2. Salum Athuman Puga (55) mkazi wa Mbezi Msufini 3. Majaliwa Hassan James (22) mkazi wa Kurungu 4. Hussein Juma Hamidu (26) mkazi wa Bungizi wa 5.

"Hawa Rashid Msangi (49) mkazi wa Mkuranga "A" kwa tuhuma za wizi wa viti vya plastic 275 vyenye thamani ya TShs. 12,300,000/= mali ya ukumbi wa mafunzo Beacon Conference & Social Hall uliopo Mkwalia wilayani Mkuranga, huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria. Watuhumiwa wamefikishwa mahakamani kwa hatua zaidi."

Pia, amesema Polisi Wilaya ya Mkuranga walimkamata Justine Fred Kalikawe (27) mkazi wa Kisemvule akiwa na kifaa kinachotumika kuzuia radi na tetemeko la ardhi kwenye nyumba ambazo zimeunganishwa na huduma ya gesi asilia.

Mtuhumiwa alifanya kitendo hicho Oktoba 27, 2026 saa 8:00 mchana huko Kisemvule Kata ya Vikindu baada ya Christian Paul Mkoba (42) kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu kuibiwa kwa kifaa hicho, msako ulianzia mara moja na majira ya saa 2:30 usiku tarehe hiyo, mtuhumiwa alikamatwa na kifaa hicho. Upelelezi wa shauri hilo unaendelea.

Vilevile, Oktoba 27, 2026 ya saa 09:00 asubuhi huko Kijiji cha Kimanzichana Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Salum Mussa Mpili aligundua kuharibiwa miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kukatwa nyaya za umeme kutoka kwenye transformer na watu wasiofahamika.

Amesema, Jeshi la Polisi lilifanya upelelezi na kufanikisha kukamata watuhumiwa wawili ambao ni Samwel Stansleus (22) mkazi wa Kigamboni- Kibugumo na 2. Samson Marwa (28) mkazi wa Kigamboni – Kibugumo, wakiwa wanatuhumiwa kwa kosa hilo la kuharibu miundo mbinu ya Serikali. Watuhumiwa wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Katika opresheni hiyo tumefanikiwa kukamata lita 35 za pombe haramu ya moshi (gongo) pamoja na mtambo mmoja wa kutengenezea pombe hiyo ambapo jumla ya watuhumiwa 26 wamekamwatwa na kesi zao zipo katika hatua mbalimbali mahakamani.

Kwa upande wa dawa za kulevya jumla ya Kilo 60 na gramu 965.5 za bangi pamoja na watuhumiwa 81 walikamatwa, kati yao wanawake 3 na wanaume 78, kesi hizo zikiwa katika hatua za upelelezi na zingine zipo katika hatua mbalimbali mahakamani.

Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Kamanda huyo amesema, wamezikamata pikipiki 33, aina tofauti tofauti zingine zikiwa hazina namba za usajili ambazo zinadhaniwa ni mali ya wizi huku zingine zikitumika katika matukio ya uhalifu.

Watuhumiwa waliokutwa nazo walishindwa kutoa vithibitisho juu ya umiliki wa pikipiki hizo. Upelelezi unaendelea kubaini wamiliki halali wa vyombo hivyo.

Kwa upande wa mafanikio mahakamani kesi za ukatili wa jinsia na unyanyasaji, kubaka na kulawiti mahakama imemtia hatiani Edward Mahona (45) mkazi wa Chamgoi wilayani Mkuranga kwa kosa la kumbaka mhanga mwenye matatizo ya akili mwenye umri wa miaka 17.

Mtuhumiwa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kumlipa muhanga fidia ya TShs. 3,000,000/=.

Katika tuko jingine Mahakama imemhukumu Godwin Salum Mzeru (39) kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili ambayo ni kubaka na kumlawiti mtoto wa miaka (10).

Aidha, kutokana na kuporomoka kwa maadili katika jamii Mahakama ilimuhukumu Daud Paschal Lushaga (36) mkazi wa Mlaleni wilaya Mkuranga kifungo cha miaka 20 jela na kulipa fidia ya TShs. 2,000,000/= baada ya kupatikana na hatia ya unyanyasaji wa kingono kwa mototo mwenye umri wa miaka (3).

Kwa upande wa usalama barabarani tumefanikiwa kukamata jumla ya makosa ya usalama barabarani 6846 ambapo makosa ya magari ni 3909 na makosa ya bajaji na pikipiki ni 2937 zilizotozwa faini, hata hivyo tumewafungia leseni za madereva watatu kutokana na kutofuata sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuendesha mwendo kasi ambapo tuliwakama kwa mfumo wa (VTS) kwenye magari ya kubeba abiria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Protas Mutayoba amesema, elimu inaendelea kutolewa na Polisi Kata kwa kushirikiana na viongozi wa vitongoji/mitaa, vijiji na kata juu ya ushirikishwaji wa jamii katika kubaini na kuzuia uhalifu. Operesheni za kupambana na uhalifu na wahalifu zinaendelea.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji limetoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu pale wanapobaini au kutilia mashaka mtu/watu kuwa ni wahalifu.

Pia, limewataka wananchi kuacha matukio ya unyanyasaji kwa watoto na kuacha kujichukulia sheria mkononi. 

Jeshi la Polisi halitamuonea muhali yeyote atakayefanya vitendo hivyo katika jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here