NA DIRAMAKINI
WIZARA ya Fedha imetangaza kuanza kwa Awamu ya Tatu ya zoezi la uhakiki binafsi kwa wastaafu wanaolipwa pensheni ya kila mwezi na Hazina, zoezi lililoanza Oktoba 25 hadi Novemba 30, 2026.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, zoezi hilo linawahusu wanufaika wote waliomo kwenye Daftari la Pensheni la Hazina ambao hawakujihakiki katika Awamu ya Kwanza na ya Pili, iliyofanyika kuanzia Januari 15 hadi Septemba 19, 2026.
Wanufaika hao ni pamoja na wastaafu, wanaolipwa pensheni ya kustaafu, maafisa na askari wanaolipwa pensheni ya ulemavu, pamoja na wajane wanaolipwa pensheni ya kifo, wanaoishi ndani na nje ya Tanzania.
Wizara imewataka wanufaika hao kujihakiki kupitia programu tumizi (applications) za benki za biashara kwenye simu zao za mkononi, au kupitia matawi ya benki wanakopokelea pensheni zao za kila mwezi.
Kwa wastaafu watakaokumbana na changamoto ya alama za vidole, Wizara imewaelekeza kufika katika Ofisi za Hazina Ndogo zilizo karibu nao, Makao Makuu ya Wizara ya Fedha, au Wizara ya Fedha Zanzibar, wakiwa na Kitambulisho cha Taifa, nakala ya kadi ya benki na kitambulisho cha mstaafu, ili waweze kuhakikiwa.
Wizara imeonya kuwa, wastaafu ambao hawatajihakiki hadi kufikia Novemba 30, 2026, watasitishiwa malipo ya pensheni zao.
Aidha, Wizara imesisitiza kuwa huduma zote kwa wastaafu zinatolewa bure, na kuwataka wanufaika kuepuka matapeli.
