Majaliwa: Kituo cha Afya Bwisya kimepandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya kuanzia leo

Rais Dkt.John Pombe Magufuli amepandisha hadhi ya Kituo cha Afya cha Bwisya kilichokopo Ukara wilayani Ukerewe, Mwanza kiwe na hadhi ya hospitali ya wilaya kuanzia leo, anaripoti Mwandishi Diramakini.

 

Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Bwisya kwenye mkutano uliofanyika viwanja vya bandarini leo mchana Septemba 23,2020.

 

Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwajulia hali wagonjwa, wanaopata huduma katia kituo cha afya Bwisya, kilichopo katika Kata ya Bwisya, Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, kabla ya kuhutubia mkutano wa kampeni za CCM, katika kata hiyo, Septemba 23, 2020,aidha kituo hicho kuanzia leo kimepandishwa hadhi kuwa hospitali ya wilaya. (Ofisi ya Waziri Mkuu).


Amesema, awali kituo hicho cha afya zamani kilikuwa zahanati lakini ikapandishwa hadhi ili kuwasaidia wakazi wa tarafa ya Ukara. "Tunataka wananchi wasihangaike kwenda hadi Nansio yalipo makao makuu ya wilaya hii. Huduma zitatolewa hapahapa. Hiyo maana yake, majengo ya tiba yataongezwa na vitengo vya huduma vitaongezwa, na madaktari bingwa wataletwa wakae hapa."

 

Amesema, ili kufanikisha hilo kwa haraka hospitali ya wilaya ya Ukerewe ambayo iko Nansio nayo pia itapandishwa na kuwa na hadhi ya hospitali ya mkoa. Kupandishwa hadhi kwa kituo hicho cha afya, kutawasadia wakazi wa Ukara ambao walikuwa wanapaswa kufuata huduma za rufaa Nansio ambako ni umbali km 30 au Mwanza mjini ambako ni umbali wa km. 75.9.

 

“Hapa Bwisya zililetwa sh. bilioni 1.4 za kupandisha hadhi kutoka zahanati na kufikia kuwa kituo cha afya. Hospitali nyingi za wilaya hapa nchini zimepatiwa sh. bilioni 1.8, kwa hiyo na ninyi hapa mtapatiwa fedha ili majengo yanayohitajika yaweze kukamilika,” amesema.

 

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mwanza kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kumwombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi na diwani wa kata ya Bwisya, Bw. Dickson Sute. Madiwani wengine watatu wa tarafa ya Ukara, wamepita bila kupingwa.

 

Akitoa, ufafanuzi kwenye sekta hiyo ya afya, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh. bilioni 2.95 zimetolewa wilaya ya Ukerewe kwa ajili ya ujenzi wa majengo tano ambayo ni maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya wazazi, chumba cha kuhifadhia maiti na nyumba ya mganga  katika vituo vya afya vya Bwisya, Kagunguli na Muriti.

 

“Kituo cha Afya cha Bwisya kilipatiwa shilingi bilioni 1.4 ambapo ujenzi na upanuzi umekamilika. Kituo cha Afya Kagunguli kilipatiwa shilingi milioni 322 ambapo ujenzi chumba cha kisasa cha upasuaji umekamilika na Kituo cha Afya Muriti kilipatiwa shilingi milioni 967 ambapo ujenzi majengo ya RCH, upasuaji na wodi ya wazazi yote yamekamilika,” amesema.

 

Kuhusu ununuzi wa dawa na vifaa tiba, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh. bilioni 3.9 zimetolewa kwa ununuzi wa dawa na vifaa tiba kwa kipindi cha 2015/2016 – 2019/2020 ambapo wastani wa bajeti ya dawa kwa mwezi ulikuwa ni shilingi milioni 63.

 

Kuhusu kuimarisha usafiri wa majini katika maziwa mito na bahari kama ilivyoainishwa kwenue Ilani ya Uchaguzi uk. 69 -70, Mheshimiwa Majaliwa amesema ujenzi wa vivuko vinne ambavyo vitatoa huduma katika maeneo ya Bugolora – Ukara (Mwanza), Kayenze – Bezi (Mwanza), Nyamisati – Mafia (Pwani) na Nkome – Chato -Buharamba (Geita) unaoendelea.

 

Amesema, Serikali imekamilisha ununuzi wa boti tatu za uokozi kwa ajili ya maeneo ya Ilugwa – Ukara (Ukerewe), Nafuba na Gana katika kisiwa cha Ukerewe. “Ili kuimarisha usafiri katika maziwa na mito, Serikali imeanza ujenzi wa vivuko na maegesho muhimu nchini ikiwemo Ujenzi wa maegesho ya Ilugwa (Ukerewe) pamoja na vivuko vya Bwiro–Bukondo (Ukerewe), Irugwa–Murutanga (Ukererwe) na Kakuro–Gana (Ukerewe). Na hii iko kwenye ukurasa wa 83 wa Ilani yetu,” amesema.

 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news