Mama mkwe wa Freeman Mbowe wa CHADEMA afariki

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mke wa aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Tanzania (BoT) na baadaye mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei,Johara Mtei amefariki.
Taarifa hizo zimethibitishwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, John Mnyika leo Agosti 20,2021.

Marehemu Johara alikuwa mke wa Edwin Mtei, mwasisi wa CHADEMA ambaye pia amewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kati ya Juni 1966 hadi Januari 1974 katika utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

"Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Johara Mtei. Mke wa Mzee Edwin Mtei Mwenyekiti muasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

"Poleni sana familia na ukoo kwa msiba. tumuweke Mzee Mtei kwenye maombi katika kipindi kigumu ambacho yeye na familia wanapitia,"ameeleza Mheshimiwa Mnyika.
Kwa nyakati tofauti wananchi mkoani Kilimanjaro wameieleza DIRAMAKINI Blog kuwa, huo ni msiba mkubwa si kwa familia tu. Bali hata kwa chama na Taifa kwa ujumla.

"Maono ya mama na baba yetu.Mzee Mtei ndiyo yaliyozaa tija hii kubwa na kufungua ukurasa imara wa Demokrasia nchini Tanzania. Mungu amlaze mahali pema mama yetu na aendelee kutupa uvunilivu katika kipindi hiki kigumu,"ameeleza Seba mkazi wa Moshi.
Aidha, huu ni msiba mzito kwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Mbowe ambaye huyu alikuwa ni mama wa mke wake.

Mama mkwe wake Freeman Mbowe, Johara Mtei alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Aghakan mkoani Dar es Salaam.

Mashinda Mtei ambaye ni Mtoto wa Edwin mtei amesema, ni kweli mama yao amefariki na kwa sasa wanaelekea mkoani Arusha kutoka Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi ya maziko.

Msiba huu umetokea ikiwa ni siku 28 zimepita tangu mbowe alipompoteza baba yake mdogo, Manase Alphayo Mbowe. Manase alifikwa na umauti Julai 23 mwaka huu katika Hospitali ya Machame Mkoani Kilimanjaro alikokuwa anapatiwa matibabu baada ya kusikia taarifa za mwanae mbowe kufunguliwa kesi ya ugaidi.

Mbowe ambaye ni mume wa Dkt. Lilian, binti wa Edwin Mtei na marehemu Johara amepokea taarifa ya vifo hivyo wakati akiwa mahabusu kwenye Gereza Kuu la Ukonga mkoani Dar es Salaam kwa tuhuma za uhujumu uchumi na kupanga njama za ugaidi.

Huu ni msiba wa tatu kumkuta Mbowe ndani ya wiki chache, baada ya kaka yake, Charles Mbowe, kufariki Dunia Julai 8 mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news