Kilio cha maji safi na salama Mhanhuzi chatua kwa RC Kafulila

Na Derick Milton, Meatu

Shida ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa mji wa Mhanhuzi, makao makuu ya Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu imeendelea kuwateseka kila mwaka hasa inapofika kipindi cha kiangazi huku wakidai maji yanayopatikana kwa sasa yamejaa tope.

Changamoto hiyo ambayo uwakumba kila mwaka wananchi wa mji huo, inasababishwa na kupungua maji kwenye bwawa la Mwanyahina ambalo ndicho chanzo kikuu cha huduma hiyo.

Mbali na hilo mamlaka ya maji katika mji huo (Mhanhuzi WSSA) inaeleza kuwa, kuwepo maji yenye tope katika kipindi cha kiangazi inasababishwa na mtambo wa kuchuja maji kuchakaa vifaa vyake ambavyo vimedumu kwa muda wa miaka 12.
Mbele ya mkuu wa mkoa, David Kafulila kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini hapo, wananchi hao walimemuomba kiongozi huo awasaidie waondokane na kero hiyo ambayo inawatesa kila mwaka.

Bulolelo Daudi mmoja wa wananchi amesema kuwa, changamoto kubwa kwa wananchi wa mji huo ni tatizo la maji hasa kipindi cha kiangazi kwani wamekuwa wakipata maji yenye tope ikifika kipindi hiki.

“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa, tunaomba tukuletee maji ambayo tunatumia wananchi wako wa mji huu wa Mhanhuzi, sisi hapa shida yetu ni maji, maji, maji…kwani serikali imeshindwa nini kutuletea maji kutoka ziwa Victoria?.

“Maji tunayopata kwa sasa yamejaa tope, hata wewe huwezi kuyatumia, tusaidieni mtuletee maji, ziwa lipo karibu tunaomba maji,” alieleza Bulolelo huku akishangiliwa na umati wa wananchi.

Kabla ya kuongea Mkuu wa Mkoa, alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji, Mhanhuzi Makongo Stephano kutoa maelezo juu ya changamoto hiyo ambapo alikiri uwepo wa changamoto kubwa katika mji wa Mhanhuzi.

“Ni kweli bila ya kuficha, kumungunya maneno, tunalo tatizo kubwa la maji, na tatizo hili limekuwa likitokea kipindi cha kiangazi, na mwaka jana hali ilikuwa mbaya zaidi, baada ya chanzo chetu kukauka,”amesema Stephano.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa, mtambo wa kuchuja maji unazidiwa uwezo na vifaa vyake vimechakaa, kutokana na kutumika kwa zaidi ya miaka 12 bila ya kufanyiwa ukarabati upya kama ambavyo inatakiwa.

Stephano ameeleza kuwa, mtambo huo ulijengwa mwaka 2009 huku ukilenga kuwahudumia wananchi 24,000 tu, ambapo matumizi yake yalitakiwa kukoma mwaka 2015 ili ufanyiwe matengenezo upya.

“Licha ya kuzidisha muda wake, lakini watu wameongezeka na kufikia 38,624 hivyo umezidiwa uwezo wake ndiyo maana kipindi hiki huduma inapatikana kidogo kidogo, lakini maji kweli yana tope,”alieleza Stephano.

Hata hivyo Mkurugezi huyo amesema kuwa ofisi yake imekuwa ikifanya jitihada za kutatuliwa kwa changamoto hiyo kutoa taarifa hadi wizarani, lakini bado hawajapata fedha.

Mkuu wa mkoa amesema kuwa, changamoto hiyo ameipokea na atakwenda kuifanyia kazi haraka iwezekanavyo huku akihaidi kufanyika jitihada za haraka ambazo zitaweza kutatua shida hiyo katika kipindi hiki.

“Juzi tumepokea pampu mbili kutoka wizarani ili kuweza kutatua changamoto hii kwa muda, na zitafungwa wiki hii ili ziongeze upatikanaji wa maji, lakini serikali imetupatia milioni 300 ili kujenga mradi wa maji kutoka Mto Semi, lengo ni kuongeza upatikanaji wa huduma,”amesema Kafulila.

Post a Comment

0 Comments