MSIMAMIZI wa Uchaguzi katika Jimbo la Musoma Mjini,Fidelica Myovera amesema kuwa jumla ya wagombea 10 kati ya 14 waliochukuwa fomu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoka vyama mbalimbali vya siasa wamerejesha na kuteuliwa kuwania nafasi hiyo katika Jimbo la Musoma Mjini.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Musoma Mjini,Vedastus Mathayo (CCM) akipokea barua ya uteuzi kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi Jjmbo hilo,Fidelica Myovera mjini hapa leo. Picha na Amos Lufungulo/www.diramakini.co.tzNi baada ya kukidhi vigezo, huku wengine kutoka vyama vitatu wakishindwa kurejesha na mmoja akirejesha,lakini hajakidhi vigezo, anaripoti Amos Lufungulo-Musoma www.diramakini.co.tz
Myovera ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari Mjini Musoma, ambapo pamoja na mambo mengine amesema zoezi la uchukuaji fomu na urejeshaji limefanyika vizuri na kwamba changamoto iliyojitokeza ni Mgombea mmoja kutoka Chama Cha 'AAFP' ambaye alichukua fomu leo na kurejesha leo, muda mfupi kabla ya zoezi hilo kufungwa, huku akiwa hajakidhi baadhi ya vigezo na hivyo kushindwa kuteuliwa.
Amevitaja vyama 10 ambavyo wagombea wake wameteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa ni pamoja na ACT Wazalendo, CUF, CHADEMA, NCCR Mageuzi, CCM, CCK, DP, NRA,UDP, ADC.
Kwa upande wake Mgombea Ubunge wa Jimbo la Musoma Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi,Vedastus Mathayo akizungumza mara baada ya kurejesha fomu amesema kuwa, iwapo atashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu atahakikisha anashirikiana na wananchi wa Jimbo la Musoma Mjini kutatua changamoto zilizopo ili maendeleo yaweze kuendelea kufanyika kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Mathayo ameongeza kuwa, wananchi wanapaswa kuendelea kumuamini pamoja na chama chake na hivyo wakipe ushindi wa kishindo kwa kuchagua viongozi kuanzia diwani, mbunge pamoja na Rais Magufuli kwa ajili ya kuendelea kuwaletea maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo uchumi, na kuimarisha huduma za kijamii.
"Wananachi wa Musoma Mjini nipo nao pamoja wakati wote, kwa hiyo nasisitiza kuwatumikia kwa moyo wa dhati baada ya kunichagua ili changamoto zilizopo tuweze kuzitatua kwa pamoja tukitekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa kushirikiana na Rais Magufuli kwa miaka mingine mitano ijayo,"amesema.
Nao wgombea walioteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutoka vyama mbalimbali Jimbo la Musoma Mjini wakizungumza na www.diramakini.co.tz kwa nyakati tofauti baada ya majina yao kubandikwa wamesema zoezi la uchukuaji fomu na urejeshaji limefanyika vizuri na kwamba, hakuna changamoto zilizojitokeza tangu mchakato huo ulipoanza na kuhitimishwa.
"Zoezi la uchukuaji fomu na urejeshaji limefanyika vizuri upande wangu sijaona changamoto kama zipo basi ni ndogondogo na ambazo ni za kibinadamu,lakini kwa ufupi limeenda vizuri,"amesema Julius Mwita mgombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo.