Dkt.Mwinyi kuja na Zanzibar mpya iliyosheheni amani, mshikamano; wavuvi,wakulima,wafugaji,wafanyabiashara,wafanyakazi, elimu, afya itakuwa zaidi ya raha

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt.Ali Mohamed Shein amewataka wana CCM pamoja na wananchi kiswani Pemba kumchagua Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi kuwa Rais wa Zanzibar, kwani ndie pekee anayeweza kuyalinda Mapinduzi ya Januari 12, 1964 pamoja na kuutunza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, inaripoti DIRAMAKINI.
Sehemu ya maelfu ya wanachi na WanaCCM wa mikoa wa Pemba wakiwa katika uzinduzi wa kampeni za CCM kwa kuwatambulisha na kuwaombea kura wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwemo Urais wa Zanzibar,Ubunge,Uwakilishi na Udiwani katika Uwanja wa Gombani ya Kale Wilaya ya Chakechake Pemba leo Septemba 16, 2020.(IKULU).

Dkt.Shein ameyasema hayo leo katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisiwani Pemba, uliofanyika katika viwanja vya Gomnani ya Kale, Chake Chake Pemba katika Mkoa wa Kusini Pemba ambao ulihudhuriwa na maelfu ya wanaCCM na wananchi.

Katika maelezo yake, Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar amesema kuwa, Dkt. Hussein Mwinyi ndiye pekee anayeweza kuyalinda na kuyatunza Mapindzi ya Januari 12.1964 pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na hakuna kiongozi mwingine anayeweza kutekeleza hayo miongoni mwa wale wanaogombea nafasi hiyo.

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM ameeleza kuwa, Zanzibar imepata uhuru wake kupitia Mapinduzi Matukufu yaliyofanyika mwaka 1964 ambapo kipindi chote hicho hadi leo CCM ndio inayoongoza dola hivyo, chama hicho kinatambua mahitaji na maisha ya wananchi hasa wanyonge.

Rais Dkt.Shein amesema kuwa, Dkt.Hussein Mwinyi anaiweza kazi ya kuyalida Mapinduzi na kuuimarisha Muungano, kwani ameshaifanya kwa kipindi kirefu kupitia nafasi za uongozi alizoitumikia ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kipindi kirefu sambamba na kuwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano.

Aidha, Makamu huyo Mwenyekiti wa CCM amesema kuwa, siku zote chama hicho hakibahatishi kuwachagua viongozi wake katika nafasi za Urais na ndio maana katika chaguzi zote wamekuwa wakipata ushindi mkubwa, hivyo kuchaguliwa kwa Dkt.Hussein Mwinyi kunaonesha wazi ushindi wa kishindo kwa CCM unakuja.

Rais Dkt. Shein amesema kuwa, CCM imemchagua Dkt.Hussein Mwinyi kuwa mgombea nafasi ya urais kutokana na sifa zote za kuwa Rais hasa ikizingatiwa kuwa yeye anapenda haki na anaichukia rushwa kwani ni mtu safi

Pia, Rais Dkt.Shein amesema kuwa, Dkt.Hussein Mwinyi ni mtu mwenye maadili na kiongozi mchapa kazi mahiri na mwenye elimu kubwa na mwenye utaalamu wa afya na aliyebobea katika fani hiyo kwani ni mtu anayejituma sana.

Rais Dkt.Shein amesema kuwa, yeye mwenyewe binafsi anamfahamu sana Dkt.Hussein Mwinyi kutokana na kuwa ameshawahi kufanya nae kazi wakati Rais Dkt.Shein akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Hussein Miwnyi akiwa Waziri katika ofisi hiyo anayeshughulikia Muungano.

Ameongeza kuwa, Dkt.Hussein Mwinyi ni kiongozi mwenye maadili, heshima na nidhamu ya hali ya juu na hawezi kufananishwa na wagombea wengine wa nafasi hiyo ya Urais wa Zanzibar.

"Dkt.Hussein ataongoza ushindi wa CCM kwani aliyepewa kapewa na wala hapokonyeki, kwani uwezo wake ni mkubwa sana,"amesisitiza Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar.

Hivyo, Rais Dkt.Shein amewataka wananchi wa kisiwa cha Pemba kutokubali kubabaishwa wala kulazimishwa kumchagua mtu asiye kuwa na sifa za kuiongoza Zanzibar na badala yake wamchague kiongozi kutoka CCM.

Aidha, Rais Dkt. Shein ameeleza matumaini yake makubwa aliyonayo kwa Dkt.Hussein Mwinyi katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi mpya ya mwaka 2020-2025 kama alivyosimamia yeye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010-2015 na ile ya 2015-2020.
Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi (kushoto) akipokea Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020-2025 kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dkt.Ali Mohamed Shein mara baada ya kumtambulisha kwa wanaCCM  wa Mikoa ya Pemba katika uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu Mwezi Oktoba, zilizofanyika leo uwanja wa Gombanio ya Kale Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba.(IKULU).

Makamu Mwenyekiti huyo ametumia fursa hiyo kumuombea kura Dkt.Hussein Mwinyi pamoja na wagombea wengine wote wa CCM wa kisiwani Pemba huku akitumia fursa hiyo kuwanadi wagombea Ubunge, Uwakilishi na Udiwani wa CCM wa mikoa miwili ya Pemba pamoja na kuwakabidhi Ilani ya chama hicho ili waende wakainadi kwa wananchi.

Nae mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi amempongeza Rais Dkt.Shein kwa kuimarisha uchumi wa Zanzibar na kupelekea kukua kwa asilimia 6.8 kwa kila mwaka.

Aidha, ameeleza mafanikio yaliopatikana katika utekeleza wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020 chini ya uongozi wa Rais Dkt.Shein na kuahaidi atayaendeleza katika Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 aliyokabidhiwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni MakamouMwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dkt.Ali Mohamed Shein akiteta jambo na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt.Abdalla Juma Saadala katika uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba zilizofanyika leo uwanja wa Gombani ya Kale Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba.(IKULU).

Dkt.Hussein ameeleza haja kwa wanaCCM na wananchi kukichagua chama hicho ili kuendeleza mafanikio hayo yaliyopatikana huku akieleza azma yake ya kuyaendeleza Mapinduzi pamoja na kuutunza na kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Aidha, ametumia fursa hiyo kueleza vipaumbele vyake iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuiimarisha sekta ya uchumi wa bahari (blue economy), hasa uvuvi wa bahari kuu kwa lengo la kuinua ajira kwa vijana sambamba na kuimarisha pato la Taifa.

Dkt. Mwinyi amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Saba hatua zilizofikiwa katika kukuza uchumi sambamba na kuongeza pato la taifa kutoka thamani ya shilingi trilioni 2.4 mwaka 2015 hadi kufikia thamani ya shilingi trilioni 3.1 mwaka 2019.

Amepongeza hatua za kuongeza makusanyo ya ndani, kutoka shilingi bilioni 428.511 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 748.9 mwaka 2019 pamoja na kupunguza utegemezi wa bajeti na kufikia asilimia 5.7 na kuvuuka lengo linaloanishwa na kufikia asilimia 7.

Aidha mgombea huyo wa urais wa Zanzibar amewaahidi wananchi hao, kama akipata ridhaa ya kuwa Rais wa Zanzibar atajenga barabara kwa kiwango cha lami, zenye urefu wa kilomita 198 kwa Unguja na Pemba.

"Tunaposema tunaimarisha uchumi, lazima tuangalie pia na ujenzi wa barabara, ndio ambao utarahisisha kila kitu,"ameeleza Dkt. Mwinyi.

Pia, Dkt. Hussein Mwinyi ameyaeleza mambo mengine atakayoyapa kipaumbele ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya utalii, sekta ya uvuvi, viwanda ufugaji wa samaki, kuwasaidia wavuvi, elimu, umeme, miundombinu, kuimarisha sekta ya kilimo na sekta nyinginezo.

Dkt.Hussein Mwinyi ameeleza kuwa, atahakikisha katika kuendeleza mradi wa upatikanaji wa mafuta na gesi mikataba itakayofungwa inawanufaisha wananchi wa Zanzibar sambamba na kuhakikisha wanapata fursa kubwa ya ajira katika sekta hiyo.

Ameeleza kuwa, katika kuhakikisha uchumi unaimarika ni lazima miundombinu ya barabara, bandari na viwanja vya ndege vyote vinaimarishwa pamoja na kuhakikisha vinapatikana vyanzo vipya vya umeme kazi ambayo ataiendeleza kwa lengo la kukuza uchumi na maendeleo ya Zanzibar.

Sambamba na hayo ameeleza azma yake ya kuimarisha huduma za jamii zikiwemo elimu bora bila ya malipo hadi sekondari, kuongeza ufaulu kwa wanafunzi na kupitia upya mitaala ya elimu ikiwemo elimu ya ufundi ili vijana waweze kujiajiri wenyewe, kuongeza udahili, fedha kwa wanafunzi vyuoni huduma za afya kuanzia msingi hadi rufaa, kukuza bajeti ya afya, maji safi na salama.

Aidha, ameeleza azma yake ya kuimarisha sekta ya kilimo, viwanda, sambamba na uimarishaji wa miundombinu ya barabara Unguja na Pemba , viwanja vya ndege na bandari.

Pia, ametoa pongezi kwa Rais Dkt.Shein kwa kusimamia amani na utulivu huku akiahidi na yeye kwa upande wake iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ataiendeleza kwani anatambua umuhimu wake kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa jumla.

Dkt.Hussein Mwinyi amegusia suala zima la utawala bora katika kukuza uchumi na kusisitiza suala zima la uwajibikaji na kueleza kuwa, hatawavumilia wale wote waliokuwa hawawajibiki na pia atahakikisha kwamba watu hawafanyi kazi kwa mazoea.

Sambamba na hayo, Dkt. Hussein Mwinyi ameeleza dhamira yake katika kuyasaidia makundi maalum ikiwa ni pamoja na kuwalinda na kuwatunza wazee, walemavu, wanawake, wasanii na wana michezo huku akieleza mikakati itakayowekwa katika kupambana na dawa za kulevya na unyanyasaji wa kijinsia.

Amesema, suala la udhalilishaji linaendelea kumuumiza kichwa, hivyo akiingia madarakani, tatizo hilo atalipa kipaumbele, ili kuona kundi la wanawake na watoto linaishi kwenye mazingira bora na imara.

"Kila ninapopita wananchi wa Zanzibar wanalilia suala la udhalilishaji kuwa limekuwa kubwa mno, sasa hili lazima nilifanye kuwa miongoni mwa vipaumbe vyangu,"ameeleza.

Aidha, ameeleza kuwa, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma, uzembe kazini vyote hivyo atavisimamia ipasavyo na kuahidi kuweka utaratibu maalum pamoja na wale atakaowachagua katika kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.

Mapema Naibu Katibu wa CCM Zanzibar, Abdalla Juma Mabodi alieleza kuwa, mara zote Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa kikibishana kwa sera na sio vituko huku akieleza kuwa Dkt.Hussein Mwinyi ana uwezo mkubwa wa kuiongoza Zanzibar.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuielezea kwa ufupi Ilani ya Uchaguzi mpya ya mwaka 2020-2025 na kusisitiza kuwa CCM haina ubaguzi na chama hicho kitaendelea kuwahudumikia wananchi wote.

Mkutano huo ulikwenda sambamba na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wa ndani ya nje ya Zanzibar wakiongozwa na msanii mwanadada machachari katika anga za Bongo Flava Nandi, Profesa Gogo na kikundi chake pamoja na wasanii wengine mbalimbali wakiwemo wale wa kizazi kipya.

Katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM aliwaomba viongozi na wanaCCM wote kusimama kwa dakika moja kwa ajili ya kumkumbuka Marehemu Salim Hassan Turky aliyekuwa mgombea nafasi ya Ubunge Jimbo la Mpendae ambaye alifariki dunia usiku wa kumkia jana na kuzikwa jioni yake Kijitoupele, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Viongozi mbalimbali wa CCM walihudhuria akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd pamoja na viongozi wengine wastaafu akiwemo Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Waziri Kiongozi Mstaafu Shamsi Vuai Nahodha pamoja na viongozi wengine wa CCM kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news