Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete,MUHAS waanzisha kliniki maalum kwa wagonjwa wa sikoseli wanaokabiliwa na magonjwa ya moyo

SEPTEMBA 16, 2020 Kliniki maalum kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa sikoseli ambao wanaokabiliwa pia na magonjwa ya moyo imeanzishwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Ayoub Kibao akimsikiliza daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) akielezea kuhusu mashine ya kuchunguza jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram) iliyopo katika kliniki maalum ya wagonjwa wenye sikoseli ambao pia wanakabiliwa na magonjwa ya moyo iliyoko katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete jijini Dar ess Salaam. (JKCI).

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, ProF. Mohamed Janabi amesema wameshirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kupitia Programu yake ya Sikoseli.

Prof. Janabi, amesema juhudi za kuianzisha kliniki hiyo zilianza takribani miaka miwili iliyopita na kwamba inalenga kuboresha huduma za matibabu ya wagonjwa hao.

Amesema, "JKCI kila wiki huwa tunawaona kwenye kliniki zet"u na kwamba kabla ya kuanzisha kliniki hiyo ilimlazimu mgonjwa anayehudhuria kliniki ya sikoseli anayegundulika kuwa na shida ya moyo, kuelekezwa JKCI ili kwenda kupangiwa tarehe ya kuanza kliniki ya moyo.

Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) wakimsikiliza mgeni rasmi Dkt. Ayoub Kibao (hayupo pichani) aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kliniki maalum ya wagonjwa wenye sikoseli ambao pia wanakabiliwa na magonjwa ya moyo iliyoko katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam. (JKCI).

“Tukaona ni adha kubwa kwao, maana yake analazimika kuhudhuria kliniki mbili. Sikoseli ni ugonjwa wa damu, mtu mwenye sikoseli yupo kwenye uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo, japo si wote ambao huishia kupata magonjwa ya moyo, lakini mtu akiwa na ugonjwa wa moyo hawezi kupata sikoseli,” amebainisha.

Ameongeza, “Kwa sababu sikoseli wenyewe ni ugonjwa ambao mtu anaupata kwa kurithi vinasaba kutoka kwa wazazi, uhusiano wake na magonjwa ya moyo ni kwamba sikoseli ni tatizo la kwenye damu, wagonjwa wa sikoseli hukabiliwa na upungufu wa damu, hali hii inaweza kuleta athari kwenye moyo na hata viungo vingine vya mwili.

“Kunapokuwa na upungufu wa damu, maana yake mwili unakuwa na damu chache lakini moyo bado hulazimika kupiga zaidi ili kuisukuma.

“Sasa neno ‘circle’ limetokana na vile visu vya kunolea mpunga (mundu), yaani zile chembe chembe za damu huwa hazipo kwenye muundo wa kawaida wa duara, zinapokuwa kwenye umbo la mundu ‘zina-tendency’ (tabia) ya kugandisha damu.

“Damu inapoganda inaweza kuziba kuziba mishipa ya damu na hali hiyo huwa haichagui itokee wapi, ikiganda kwenye mishipa iliyopo kwenye moyo ndipo uhusiano na magonjwa ya moyo unapotokea, wengne hupata pia ugonjwa wa kiharusi,”amebainisha.

Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Ayoub Kibao akizungumza jambo wakati akikagua chumba cha kufanyia kipimo cha kuangalia umeme wa moyo (Electrocardiogram) katika kliniki maalum ya wagonjwa wenye sikoseli ambao pia wanakabiliwa na magonjwa ya moyo iliyoko katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete jijini Dar ess Salaam. (JKCI).

Ameongeza, “Zile changamoto zinazotokea kwenye damu ndiyo zinaleta athari kwenye moyo, kwa hiyo sikoseli ndiyo inasababisha ugonjwa wa moyo, lakini mnoyo wenyewe hauwezi kusababisha sikoseli.

“Hivyo, wataalamu tulishauriana na kukubaliana kuanzisha kliniki hii maalum kwa wagonjwa hawa kwa sababu ni magonjwa yanayoingiliana, mgonjwa atakapokuja ataweza kuonwa na madaktari wa magonjwa yote mawili kwa wakati mmoja,” amesisitiza.

Amebainisha kutokuwa na kliniki ya wagonjwa wa sikoseli kwa upande wa watoto pia watu wazima na kwamba watafanyiwa vipimo vyote vya moyo na damu na kupatiwa dawa kadri itakavyoshauriwa.
Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Ayoub Kibao, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi na Mkuu wa Idara ya Tiba wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) ambaye pia ni Mkuu wa Utafiti katika programu ya sikoseli na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Paschal Ruggajo wakikata utepe kuashiria ufunguzi wa kliniki maalum ya wagonjwa wenye sikoseli ambao pia wanakabiliwa na magonjwa ya moyo iliyoko katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete jijini Dar ess Salaam. (JKCI).

“Tumeanza na sikoseli, siku zijazo dhumuni letu ni kufikia hatua ya kuanzisha kliniki moja kwa magonjwa yanayoingiliana kwa mfano moyo na figo, au moyo na kisukari, kumrahisishia mgonjwa kuhudumiwa na kumuepushia adha ya kukimbizana huku na kule, kufuata huduma,” amesema.

Mkuu wa Idara ya Tiba wa Muhas ambaye pia ni Mkuu wa Utafiti wa Muhas katika programu ya sikoseli na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo, Paschal Ruggajo amesema kliniki hiyo itawasaidia pia wataalamu kujadiliana na kufanya tafiti zaidi ili kuimarisha na kuboresha tiba za wagonjwa wa sikoseli.

Mwenyekiti wa Chama cha Wagonjwa wa Sikoseli Nchini, Arafa Said amepongeza hatua hiyo na kubainisha kwamba gharama za matibabu bado ni changamoto kubwa inayowakabili.

Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufunguliwa kwa kliniki maalum ya wagonjwa wenye sikoseli ambao pia wanakabiliwa na magonjwa ya moyo iliyoko katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete jijini Dar ess Salaam. (JKCI).

“Wengi wetu hawana bima ya afya na wapo wanaokata tamaa na kuacha kuhudhuria kliniki, tunaendelea kujitahidi kutafuta wafadhili, ili kuwasaidia,” amesema.

Akizungumza, Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Ayoub Kibao amewahamasisha watanzania kukata bima ya afya kwani inasaidia kupunguza mzigo wa gharama za matibabu.

“Takwimu zinaonesha nchini kila mwaka watoto 8000 hadi 11,000 huzaliwa na ugonjwa huu, nawashauri hasa vijana wanaotaka kuingia kwenye ndoa, wapime ili kujua iwapo wamebeba vinasaba vya ugonjwa huu ama la,” ameshauri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news