Mchungaji Msigwa kupitia CHADEMA aahidi neema Iringa Mjini, awataka wananchi wasidanganyike

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Mchungaji Peter  Msigwa amewaomba wananchi wa jimbo hilo kumpa miaka mitano mingine ili aendelee kuleta maendeleo kama alivyofanya kwenye miaka kumi ya ubunge wake na wasikubali kurubuniwa.

Akizungumza kwenye mkutano wa kuomba kura kwa wananchi wa Kata ya Igumbilo,Mchungaji Msigwa amesema kuwa, Iringa ya sasa imepiga hatua kimaendeleo baada ya kufanya kazi kubwa ya kimaendeleo kama kuboresha sekta ya afya na miundombinu.

Amesema kuwa barabara nyingi za jimbo la Iringa Mjini zimejengwa kwa kiwango cha lami kutokana na juhudi za kujenga hoja bungeni na kwa wadau mbalimbali ambao walisaidia kujenga barabara hizo.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA,Mchungaji Peter Msigwa akiomba kura kuelekea Oktoba 28,2020.(MPW).

"Mnakumbuka nilipoingia madarakani asilimia kubwa ya barabara zetu zilikuwa za vumbi, hivyo nilijitahidi kupambana kuhakikisha kuwa Iringa Mjini inakuwa na miundombinu bora ya barabara,"amesema Msigwa.

Msigwa ameongeza kwa kusema kuwa wamefanikiwa kuboresha sekta ya afya tofauti na ilivyokuwa awali na ameahidi kuboresha sekta ya afya kwa kutoa bima za afya kwa wananchi wote kwa kuwa ndio Sera ya CHADEMA katika uchaguzi wa mwaka huu.

Lakini Msigwa amesema kuwa ni aibu kwa wananchi wa jimbo la Iringa Mjini kushindanisha na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jesca Msambatavangu kwa kuwa hata uwezo wa kuliongoza jimbo la Iringa Mjini hana.

Msigwa alimalizia kwa kuwaomba wananchi wa jimbo la Iringa Mjini kumpigia kura mgombea urais wa CHADEMA,Tundu Lisu na diwani wa CHADEMA Kata ya Igumbilo na kata zote kwa maendeleo ya nchi,jimbo na kata hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news