TAKUKURU: Watanzania wapuuzeni hawa wapotoshaji,wana nia ovu za kujenga chuki dhidi ya wananchi kwa Serikali yao

"Nimewaita hapa ili kupitia vyombo vyenu vya habari, kukanusha taarifa za uongo na upotoshaji, kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Serikali kwa ujumla imekuwa ikiwabambika wananchi kesi za tuhuma za rushwa na utakatishaji wa fedha na baadaye kutaifisha fedha za watuhumiwa hao kutoka katika akaunti zao za benki.

"Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inakanusha taarifa hizi kwamba si za kweli na ni taarifa zenye nia ovu ya kujenga chuki dhidi ya wananchi kwa Serikali yao. Tunapenda umma wa watanzania utambue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanya kazi zake kwa weledi,hivyo suala hili halijawahi kutokea;
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Brigedia Jenerali John Julius Mbungo ameyasema hayo leo Septemba 23, 2020 wakati akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mtazame mubashara Mkurugenzi wa TAKUKURU hapa
KWA UPANDE WA TAKUKURU;

"Ninapenda wananchi wafahamu kuwa, TAKUKURU inapokuwa imepokea tuhuma, inafanya uchunguzi ili kupata ushahidi dhidi ya tuhuma hiyo. Mara baada ya kukamilisha upatikanaji wa ushahidi huo, jalada la uchunguzi linapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP) kwa ajili ya mapitio ya ushahidi tuliokusanya.

"DPP akiridhika na ushaidi ulio kwenye jalada la uchunguzi ndipo kesi inafunguliwa mahakamani. Huu ndiyo mchakato ambao hatuoni ni kwa namna gani suala la kubambikiwa kesi litakavyojitokeza.

"Kwa hiyo basi, tunawasihi wananchi, watambue kwamba watu ambao wamekuwa wakizitoa tuhuma hizi za kwamba TAKUKURU au Serikali kwa ujumla inawabambikia kesi wananchi sio wakweli na wana nia ovu ya kujenga chuki dhidi ya wananchi na Serikali yao,"amesema Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Brigedia Jenerali John Julius Mbungo. Huku akiongeza kuwa,

"Lakini pia ni watu ambao wanataka kurudisha nyuma kasi ya mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini. Ni rai yangu kwa Watanzania kuwa, kamwe wasikubali kudanganywa na maelezo rahisi rahisi ya aina hii na wapuuzie taarifa za aina hii zinazotolewa na baadhi ya watu wasio na uzalendo kwa Taifa letu,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Brigedia Jenerali John Julius Mbungo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news