Wazo la Rais Shein lawezesha kukabili changamoto ya madawati katika skuli za msingi, sekondari

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein ameipongeza Kamati ya Madawati kwa Skuli za Serikali kwa kusimamia na kuhamasisha wahisani na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi katika kuchangia utatuzi wa uhaba wa madawati,anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Ali Mohamed Shein, akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Madawati Zanzibar, baada ya kukabidhiwa ripoti ya kamati hiyo na (kulia kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt.Abdulhamid Yahya Mzee na kushoto kwa Rais ni Mwenyekiti wa Kamati ya Madawati Zanzibar na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora na Utumishi wa Umma, Haroun Ali Suleiman,hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar Septemba 30,2020. (IKULU).

Ameyasema hayo Septemba 30,2020 Ikulu jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na baadae kukabidhiwa ripoti na Kamati ya Madawati ya Zanzibar ambayo inaongozwa na Mwenyekiti wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman.

Katika pongezi zake hizo, Rais Dkt.Shein ameeleza kuwa, kazi kubwa imefanywa na kamati hiyo na hatimae mafanikio makubwa yameweza kupatikana kwa asilimia 70 ya kupunguza uhaba wamadawati kwa skuli za Unguja na Pemba.

Rais Dkt.Shein ameahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba na ile ijayo itaendelea kuiitafutia ufumbuzi changamoto ya uhaba wa madawati ili kuhakikisha wanafunzi wote wa msingi na sekondari kwa Unguja na Pemba hakuna anayekaa chini.

Aidha, Rais Dkt.Shein amesema kuwa, kamati hiyo aliyoiunda mnamo tarehe 27 Julai mwaka 2016 imeweza kufanya kazi nzuri ya kusimamia na kuhamasisha wahisani na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi katika kuchangia utatuzi wa uhaba wa madawati kwa skuli za Zanzibar.

Ameongeza kuwa, kamati hiyo yenye wajumbe 13 wakiongozwa na Mwenyekiti wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman na Makamu Mwenyekiti wake, Riziki Pembe Juma imefanya kazi kubwa na kuna kila sababu ya kupongezwa.

Amesema kuwa, kila Mjumbe katika kamati hiyo ana sifa zake hali ambayo imepelekea kupatikana kwa mafanikio makubwa hatua ambayo imetokana na nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

‘”Serikali imefanya jitihada kubwa ya kuhakikisha inawapatia wanafunzi wa Skuli za Serikali madawati kwani hapo mwanzo wengi wao walikuwa hawana pa kukaa tumeanza na tumetimiza wajibu wetu,”amesema Rais Dkt.Shein.

Pamoja na hayo, Rais Dkt.Shein amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuendeleza azma ya Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume kutangaza elimu bure hivyo ni vyema na wanafunzi wote wakakaa kwenye madwati ya uhakika ili juhudi hizo ziende sambamba katika kuimarisha sekta ya elimu.

Rais Dkt. Shein amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa elimu bure pamoja na huduma za afya ili kufikia azma ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12,1964 huku akitumia fursa hiyo kuwapongeza wajumbe wa kamati hiyo kwa kuonesha uzalendo wao mkubwa kwa wanafunzi pamoja na nchi yao.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Ali Mohamed Shein akikabidhiwa ripoti ya ukusanyaji wa Madawati Zanzibar na Mwenyekiti wa Kamati ya Madawati Zanzibar na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora na Utumishi wa Umma, Haroun Ali Suleiman, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.(IKULU).

Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Madawati ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesema kuwa kufuatia makusanyo ya fedha za madawati sh.Bilioni 7.6 kamati ilinunua madawati kwa awamu mbili.

Amesema kuwa, Awamu ya kwanza ilifanyika kwa madawati ya wanafunzi wa Sekondari vilivyojumuisha seti 44,620 ya viti na meza na awamu ya pili ni kwa madawati ya wanafunzi wa Skuli za Msingi vilivyojumuisha meza 11,560 za wanafunzi watatu watatu na viti 34,680.

Ameongeza kuwa, jumla ya shilingi bilioni 5.7 zilitumika katika ununuzi wa madawatiya Msingi na Sekondari ambapo kwa awamu ya tatu kwa wanafunzi wa Sekondari zitatumika shilingi bilioni 1.8 na tayari madawati yameshaagizwa na yanatarajia kufika nchini mnamo mwezi wa Disemba, mwaka huu ambapo yote yaitaendelea kusambazwa katika Skuli za Unguja na Pemba.

Kamati hiyo pia, imepongeza ushirikiano mzuri uliofanyika kati yake na Wizara ya Fedha na Mipango na hatimae kupata mafanikio hayo makubwa ndani ya miaka minne ya kamati hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora na Utumishi wa Umma na Mwenyekiti wa Kamati ya Madawati Zanzibar, Haruon Ali Suleiman akizungumza wakati wa kukabidhi ripoti ya ukusanyaji wa madawati Zanzibar,mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar na kushoto ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe.(IKULU).

Nao wajumbe hao walimpongeza Dkt.Shein kwa kuthubutu na kuibua wazo hilo katika uongozi wake jambo ambalo limeweza kuleta faraja kubwa kwa wanafunzi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar huku kamati hiyo ikisifu uimara wa madawati hayo yaliyonunuliwa nchini China.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki pembe Juma kwa niaba ya Wizara yake ametoa pongezi kwa Rais Dkt.Shein kwa jitihada zake hizo za kuhakikisha wanafunzi wanapata madawati, changamoto ambayo waliikabili kwa muda mrefu.

Ameongeza kuwa, uwepo wa viti na meza hizo umepelekea kuimarika kwa sekta ya elimu kutokana na mazingira mazuri waliyowekewa wanafunzi kwa kuweza kupata madawati ya uhakika na kuwasaidia katika kujisomea.Ameeleza kuwa, kwa sasa hakuna mwanafunzi hata mmoja anaeyfanya mitihani katika skuli za Serikali anayekaa chini na badala yake wanafunzi wote wanakaa kwenye viti na madawati ya uhakika ambapo aliongeza kuwa mbali na madawati pia Serikali imejenga majengo mapya na ya ghorofa, imeajiri walimu wengi pamoja na kuongeza huduma nyingine katika sekta hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news