Mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) , Vedastus Mathayo amesema andapo atachaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ataiomba Serikali kuongeza eneo la Manispaa ya Musoma kwa kuzirejesha baadhi ya kata zinazopakana na manispaa ikiwemo Kata ya Bisumwa iliyopo Wilaya ya Butiama ili kuwezesha wawekezaji kupata maeneo ya kujenga miradi itakayosaidia kutatua tatizo la ajira na kukuza uchumi,anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.
Ameyasema hayo Septemba 30, 2020 wakati akifanya kampeni ya kunadi sera na kuomba kura katika Kata ya Nyasho ambapo pia, amewaomba wananchi wa Musoma Mjini kukichagua chama hicho kuanzia udiwani, ubunge hadi Rais.
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakifuatilia kampeni za mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Mathayo zilizofanyika Nyasho Stendi Manispaa ya Musoma Septemba 30,2020. (Diramakini).
Aidha amesema, kinamama wenye lengo la kufanya biashara atasimamia waweze kupata elimu ya ujasiriamali bure kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo(SIDO) ambapo baada ya kuhitimu mafunzo hayo watapewa mitaji kwa njia ya mkopo bila riba ili wafanye biashara kwa ufanisi sambamba na kusimamia uongezaji wa fani za ufundi katika Chuo cha VETA cha Musoma kwa ajili ya vijana.
" Eneo letu la Manispaa ni dogo, mkinipa ridhaa nitaiomba Serikali ipanue eneo kwa sababu muda huu ukitaka mwekezaji aje Manispaa ya Musoma lazima alipe fidia kwa wananchi kwa gharama kubwa, lakini eneo likiongezeka watajenga viwanda na kuwekeza miradi yao na hivyo ajira zitaongezeka kwa Vijana. Na pia viwanda vingine vilivyopo nitahakikisha vinafanya kazi na habari njema kwa sasa Serikali imeshapata Mwekezaji wa Kiwanda cha Nguo cha MUTEX wapo kwenye hatua za mazungumzo ya mwisho,"amesema Mathayo.
Mgombea Ubunge Jimbo la Musoma Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Vedastus Mathayo akiwaomba kura wananchi Kata ya Nyasho Septemba 30,2020.(Diramakini).
Aidha Mathayo amesema, atahakikisha anawezesha vijana katika Manispaa ya Musoma kushiriki katika uvuvi bora wa samaki kusudi wazidi kunufaika na rasilimali hiyo kwa maendeleo yao, na hivyo amewaomba wananchi wa Manispaa ya Musoma kuchagua mafiga matatu kuanzia diwani, Mbunge na Rais Dkt.John Magufuli.
Kwa upande wake Mgombea Udiwani Kata ya Nyasho, Khaji Mtete amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuboresha Shule ya Msingi na Sekondari za kata hiyo, na kuwezesha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami pamoja na uimarishaji wa huduma ya maji safi na salama ndani ya kata hiyo.
Mtete ameomba wananchi wa kata hiyo wampe ridhaa kwa kumchagua katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ili akaendeleze utekelezaji wa shughuli zingine za maendeleo ikiwemo kuwezesha ujenzi wa soko la kisasa katika kata hiyo ili wafanyabiashara na wajasiriamali waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi.