DC Kinawiro asitisha ubomoaji wa nyumba 374 za wananchi Bukoba

Mgogoro wa viwanja katika mtaa wa Kyebitembe Kata Nshambya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera uliodumu kwa zaidi ya miaka 22 na kusababisha kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani sasa umemalizika baada ya serikali kuingilia kati,anaripoti Allawi Kaboyo, Bukoba.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kata hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Deodatus Kinawiro amesema kuwa Hamashauri ya Manispaa ya Bukoba kupitia kwa viongozi wake waliomaliza muda wao wakiongozwa na mstahiki Meya, walipanga kubomoa nyumba za wananchi 374 pamoja na misingi kwa kosa walilolifanya wao awali.

Kinawiro amesema serikali haipo tayari kuona wananchi wake wakiteseka na kuhangaika kwa makosa ya wataalamu waliokuwa wanahusika na masuala ya ardhi ambao walikuwa wakiuza kiwanja kimoja kwa zaidi ya watu wawili na kusababisha migogoro.

“Mgogoro huu umedumu kwa miaka 22 na kuna watu wamekuwa wakinufaika na mgogoro huu bila kujali wananchi wanaoumia, sasa kuanzia sasa nafuta ramani ya zamani ili ichorwe ramani mpya ambayo itaendana na hali halisi ilivyo ya makazi ya sasa na kuanzia sasa pia hakuna kubomoa wala kugusa nyumba yoyote iliyojengwa hata msingi,” amesema Kinawiro.

Aidha ameiagiza halmashauri kuwatafutia viwanja ndani ya muda mfupi wale wote waliokuwa wakilalamikia viwanja ambavyo tayari viliuzwa na waliouziwa wameshajenga na wale waliokwisha jenga wasibughudhiwe.

Kwa upande wake Kaimu Kamishina wa Ardhi Mkoa wa Kagera Erick Makundi, amewataka wananchii kufuata utaratibu kabla hawajanunua viwanja au kuanza ujenzi, na kuwa endapo watawahi kuchanga pesa za urasimishaji basi watapewa kipaumbele cha kupimiwa na suala la kupewa hati miliki halitazidi wiki mbili.

Mnamo Septemba 16, Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufui akiwa katika mkutano wa kampeni mjini Bukoba aliuagiza uongozi wa Wilaya ya Bukoba kuhakikisha wanamaliza mgogoro wa viwanja Kyebitembe mapema ili kuwawzesha wananchi kuishi kwa uhuru na usalama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news