Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameshuhudia uzinduzi wa Msikiti wa Sheikh Abubakar Zubeir Ally uliojengwa Chamwino mkoani Dodoma kwa gharama ya shilingi milioni 319.3 zilizotokana na michango ya viongozi, taasisi na watu mbalimbali, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Ujenzi wa msikiti huo ulianza tarehe 28 Agosti, 2020 ikiwa ni siku tatu baada ya Rais Magufuli kuitisha harambee ya kuchangisha fedha za kujenga Msikiti mpya kwa ajili ya Waislamu wa Chamwino, akiwa katika Ibada ya uzinduzi wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Imakulata Ikulu-Chamwino ambalo pia limejengwa kwa harambee iliyoendeshwa na Mhe. Rais Magufuli.
Uzinduzi wa Msikiti huo umefanywa leo Oktoba 26,2020 na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Ally ambapo pamoja na Rais Magufuli, sherehe za uzinduzi huo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge, viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini, viongozi wa taasisi, na watu mbalimbali waliochangia ujenzi huo.
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Charles Mbuge amemshukuru Rais Magufuli kwa kuiamini JKT kujenga miradi mbalimbali na amesema kutokana na Msikiti huo kujengwa na JKT gharama za ujenzi zimekuwa shilingi Milioni 319.3 ikilinganishwa na shilingi Milioni 439.4 kama ujenzi ungefanywa na kampuni za ukandarasi.
Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Ally amemshukuru, Rais Magufuli kwa moyo wake wa upendo na ucha Mungu wake uliomuongoza kuchangisha fedha zilizofanikisha kujengwa kwa Msikiti huo, pamoja na Msikiti mkubwa wa kimataifa uliojengwa Kinondoni Jijini Dar es Salaam ambapo Mhe. Rais Magufuli alimuomba Mfalme Mohammed VI wa Morocco kufadhili ujenzi huo.
Sheikh Abubakar Zubeir Ally pia amezishukuru taasisi na watu wote waliojitokeza kuchangia ujenzi huo na ameongoza Dua ya kuuombea Msikiti, Taifa la Tanzania na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020.
Mhe. Rais Magufuli amesema anaamini kuwa kujengwa kwa Msikiti huo sio tu kutawafaa Waislamu watakaoutumia kuswali bali pia utadumisha amani, upendo na umoja wa Watanzania.
Amesisitiza kuwa baada ya kukamilisha ujenzi huo anadhamiria kufanya harambee nyingine ya kuchangisha fedha kwa ajili Dhehebu la Dini linalofanya Ibada ya Juma siku ya Jumamosi na ameeleza kuwa atafurahi kuona Ikulu ya Chamwino ikiwa imezungukwa na Makanisa na Misikiti.
