Simba SC ambao ni mabingwa watetezi wamepoteza mechi ya pili mfululizo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuchapwa moja kwa sufuri na Ruvu Shooting, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Timu hiyo ilimaliza mchezo huo ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja jioni ya leo Oktoba 26,2020 Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Aidha, kwa matokeo hayo yanaifaya Ruvu Shooting ifikishe alama 12 baada ya kucheza mechi nane na kusogea nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ya timu 18, wakati Simba SC iliyofungwa 1-0 pia na Tanzania Prisons kwenye mechi iliyopita mjini Sumbawanga, inaangukia nafasi ya nne ikibaki na alama 13 baada ya mechi saba.
Bao lililoizamisha Simba SC limefungwa na Nahodha wa Ruvu Shooting, Fully Zulu Maganga aliyenufaika na makosa ya beki, Serge Pascal Wawa, hivyo kutumia nafasi hiyo kumfunga kipa Beno Kakolanya 36'.
Ruvu Shooting inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa Tanzania na klabu ya Yanga miaka ya 1980, Charles Boniphace Mkwasa ilimaliza pungufu baada ya mchezaji wake Shaaban Msala kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 75.
Aidha,Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Sven-Ludwig Vandenbroeck ilishindwa kutumia fursa hiyo japo kupata bao la kusawazisha licha ya kupewa hadi penalti, ambayo Nahodha John Raphael Bocco aligongesha mwamba na mpira ukarudi uwanjani 79'.Refa Abdalah Mwinyimkuu wa Singida alitoa penalti hiyo baada ya beki wa Ruvu Shooting, Renatus Ambroce Kisase kuinua mguu kuondosha mpira kwenye boksi lao mbele ya kiungo wa Simba SC kutoka Msumbiji, Luis Miquissone.
Refa Mwinyimkuu aliyekuwa anasaidiwa na Abdulaziz ally wa Arusha na Josephat Kasilirwa wa Iringa, alirefushwa mchezo kwa dakika sita zaidi ili kufidia muda uliopotezwa kwa matukio mbalimbali ingawa hazikuwa na manufaa kwa simba.
Wakati huo huo,Jaffar Salum Kibaya 62' kupitia bao lake pekee limetosha kuipa Mtibwa Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa CCM Gairo mkoani Morogoro.Klabu ya Mtibwa Sugar inafikisha alama 11 baada ya kucheza mechi nane na kusogea nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wakati Azam FC inayobaki na alama zake 21 baada ya kucheza mechi nane na inaendelea kuongoza kwa alama mbili zaidi ya mabingwa wa kihistoria, Yanga SC ambao hata hivyo wana mchezo mmoja mkononi.

