Wananchi wa Manispaa ya Musoma waliojiandikisha kupiga kura wametakiwa kujitokeza kwa wingi hapo kesho kupiga kura na kukichagua Chama Cha Mapinduzi kuanzia madiwani, mbunge na Rais Dkt. John Magufuli ili wawatumikie katika kuwaletea maendeleo kwa miaka mingine mitano, anaripoti Amos Lufungilo (Diramakini) Mara.
Hayo yamesemwa na Mwalimu Makuru Lameck Joseph wakati akizungumza na Diramakini wakati wa kufunga kampeni za chama hicho zilizofanyika Viwanja vya Mukendo Manispaa ya Musoma, ambapo amesema uchaguzi wa kesho ni muhimu kwa wakazi wa Musoma na Watanzania wote kuchagua viongozi wanaofaa na watakaosimamia maslahi ya wananchi.
"Niwaombe wakazi wa Manispaa ya Musoma wajitokeze kwa wingi kuchagua viongozi wa CCM ambao ndio wataweza kutekeleza ilani ya chama hicho kwa ufanisi mkubwa,"amesema huku akiwaasa kudumisha amani na utulivu kwani amani ndio msingi wa mambo yote, hivyo ikitoweka Taifa litashindwa kusimama huku akitolea mfano mataifa ambayo yalichezea amani na kwa sasa uchumi wake umedumaa ikiwemo Somalia na Libya.
Ameongeza kuwa, vyama vyote vinapaswa kufuata sheria taratibu na kanuni za Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuhakikisha wananchi wanarejea nyumbani baada ya kupiga kura na kutokaa mita 200 kuepusha msongamano ambao unaweza kuleta uvunjifu wa amani katika siku hiyo ya uchaguzi.
"Ilani ya CCM inatekelezeka kwa hiyo ninaimani kubwa Chama Cha Mapinduzi kitashinda kata zote 16 kutokana na kazi nzuri za maendeleo zilizofanywa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,"amesema.
Pia amewaasa wananchi wa majimbo mengine kukichagua chama hicho kwa kishindo kwa manufaa yao kwani Rais Magufuli amewapelekea wananchi wa Mkoa wa Mara kwa ujumla miradi mikubwa ya Kimkakati ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Pia kuboresha shule aliyosoma Baba wa Taifa iliyopo Mwisenge, mradi mkubwa wa Maji wa Bukanga, na mradi mkubwa wa maji wa Bunda.
Amesema, kutokana na kasi ya Rais Magufuli kwa kuwaletea maendeleo wakazi wa Mkoa wa Mara,hana shaka kuwa, majimbo yote ya mkoa huo yatachukuliwa na Chama Cha Mapinduzi na hivyo watanzania watarajie mafanikio makubwa kwa miaka mingine mitano ya Rais Magufuli ambayo amesema itakuwa ya neema katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
