MWANANCHI TAMBUA UMUHIMU WA KURA YAKO - MAJALIWA

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amewataka Watanzania watambue umuhimu wa kura zao watakapoenda kuchagua viongozi tarehe 28 Oktoba, 2020.

“Tambua umuhimu wa kura yako. Uongozi wa nchi hautaki majaribio, unaweza kufanya majaribio kwa viongozi wa vikao vya harusi au send-off lakini siyo uongozi wa nchi,” amesema.

Ametoa wito huo leo Oktoba 6, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa Kata ya Kilindoni wilayani Mafia, mkoani Pwani kwenye mkutano wa kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt John Pombe Magufuli pamoja na mgombea ubunge wa jimbo la Mafia, Bw. Omari Kipanga na mgombea wa udiwani wa kata ya Kilindoni, Bw. Salum Ally.

“Nawaletea viongozi kutoka chama ambacho ni taasisi madhubuti yenye kuweka mipango yake kwenye Ilani yake ya uchaguzi. Watakuja wagombea mbalimbali hapa, wasikilizeni, wapimeni lakini tambueni umuhimu wa kura zenu,” amesisitiza.

“Viongozi wa CCM ninaowaleta kwenu wana mambo ya kueleza. Wanaeleza ni nini wamefanya katika miaka mitano iliyopita na nini watafanya katika miaka mitano ijayo. Tunatafuta kiongozi wa nchi, ambaye ametulia, anayekwenda kuongoza watu zaidi ya milioni 60 wenye dini tofauti, makabila na itikadi tofauti, tunatafuta kiongozi ambaye anaweza kuzitunza tunu za Taifa ikiwemo amani,” amesema.

Amesema Watanzania wanapaswa kumchagua Rais ambaye anaweza kuzifanya rasilimali za nchi ni mali za Watanzania na siyo za hao anaowajua yeye na akawaacha Watanzania wakihangaika.
“Lazima tumpe urais mtu ambaye tunamjua kwa historia, ambaye amewahi kuongoza kikundi cha watu na akapata mafanikio. Tunataka tumchague Rais ambaye anayeweza kutuletea maendeleo na siyo maneno tu. Tumebakiza siku 21 tu, tunataka kiongozi ambaye kwa dhamira yake mwenyewe anamtanguliza Mungu mbele.”

Akielezea kuhusu uboreshaji wa barabara, Mheshimiwa Majaliwa amesema sh. bilioni mbili zimetolewa kupitia TARURA kwa ajili ya matengenezo ya kawaida, matengenezo ya sehemu korofi, ya muda maalum na madaraja kadhaa katika Halmashauri ya Mafia.

“Matengenezo ya kawaida yamefanyika katika barabara za Kilimahewa – Mdundani (km. 2), Jimbo – Jojo (km. 10), Baleni – Kipingwi (km 6.4) na matengenezo ya maeneo korofi yamefanyika katika barabara za Ndogoni - Kimtondo; Baleni - Kipingwi, na Mwambae – Tumbuja. Pia matengenezo ya muda maalum yamefanywa katika barabara za Marimbani – Utende (km 4.2) na Baleni – Kilombero (km 8.3),” amesema.

Akielezea kuhusu uboreshaji wa sekta ya maji, Mheshimiwa Majaliwa amesema Mafia kuna miradi mikubwa ya maji ambayo imepatiwa sh. bilioni 5 ili kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama.

“Shilingi bilioni 5 zimetumika kwa ajili ya miradi ya mikubwa ya maji ikiwemo ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Bweni; ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Kanga; uchimbaji visima vitatu vya Kigamboni, Vunjanazi na Dawe. Na pia ujenzi wa mradi wa maji ya bomba vijiji vya Jibondo, Juani na Chole umetumia fedha hizo.”

Amesema kiasi kingine cha sh. milioni 66 kimetumika kwenye miradi ya ukarabati wa miundombinu na kuboresha mtandao wa maji ya bomba katika kijiji cha Kilindoni. Amesema zilitolewa pia sh. bilioni 2 ili kutandika mabomba chini ya maji kwenda Jibondo.

Kuhusu sekta ya elimu, Mheshimiwa Majaliwa amesema kiasi cha sh. bilioni 1.5 kimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha VETA ambacho ujenzi wake hadi sasa umefikia asilimia 40. “Ujenzi wa chuo hiki unaendelea; ukikamilika, tunataka vijana wa Mafia waende pale wakajifunze ufundi uashi, ujenzi au utaalamu wa kompyuta,” amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news