NEC yawatoa hofu wapiga kura wenye mahitaji maalum

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC ) imewatoa hofu wapiga kura wenye mahitaji maalum katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa wadau wa uchaguzi Mkoa wa Dar es Saalam, Afisa Tume ya Uchaguzi, Duttu Kasanda, amesema watu wenye mahitaji maalum wakiwemo walemavu, wajawazito,
mama wanaonyonyesha watakapofika vituoni watapewa kipaumbele katika kupiga kura.
Amesema kuwa, watu wasiojua kusoma na kuandika wanaruhusiwa kwenda na watu wanaowaamini ili wakawapigie kura na kwa upande wa watu wenye ulemavu wa kuona kila kituo cha kupiga kura kitakuwa na kifaa cha maandishi ya nukta nundu kwa wale wanaofahamu kutumia maandishi hayo ili kila Mtanzania asipoteze haki yake ya msingi na kikatiba.

Aidha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi pia itaweka vifaa maalum (Vituturi) kila kituo kwa watu wenye ulemavu wa viungo lengo likiwa ni kuhakikisha hakuna mwananchi anapoteza haki ya kuchagua kiongozi anayemfaa,huku ikivipa onyo vyama vya siasa na wagombea kuzingatia maadili ya uchaguzi katika kampeni zao,ikiwemo kuepuka lugha za kashfa na maneno ya uchochezi yanayotishia usalama wa nchi.

Aidha, amevisistiza vyama vya siasa na wagombea wao pindi wanapokuwa na malalamiko yoyote ya kimaadili kuwasilisha 
malalamiko kwenye kamati za maadili ndani ya muda uliowekwa.

Ameongeza kuwa, wakati tume ikiendelea kuratibu kusimamia na kuendesha uchaguzi kwa kutumia sheria za uchaguzi vyama vya siasa, wagombea na wananchi wanakumbushwa kuwa katika kipindi hiki sheria nyingine za nchi hazijasimama hivyo wajihadhari na vitendo ama matamshi ambayo yanaweza kusababisha vurugu kwa kisingizio cha uchaguzi.

Kwa upande wake, Mkurungezi Msaidizi wa Elimu ya Mpiga Kura, Monica Mnanka, amesema mpaka sasa maadalizi ya vifaa vya uchaguzi yamekamilika ikiwa ni pamoja na vifaa kusambazwa katika maeneo mbalimbali ya nchi ambapo wiki iliyopita NEC ilipeleka vifaa aina ya masanduku katika mikoa 12.

"Tumejipanga vizuri kwa kuhakikisha kuwa hakuna ucheleweshwaji wa vifaa, tutatumia njia mbalimbali ikiwemo za majini na ardhini ili vifaa vifike kwa wakati,"amesema Mnanka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news