Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein ameagana na wafanyakazi wake wa Ofisi yake ya Faragha na kuwapongeza kwa kushirikiana nae kwa muda wote wa miaka kumi ya uongozi wake.
Dkt. Shein ameyasema hayo katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar wakati akiwapongeza na kuwaaga wafanyakazi wake wa Ofisi ya Faragha ya Rais pamoja na kula nao chakula maalum cha mchana.
Katika maelezo yake Rais Dkt. Shein amewapongeza wafanyakazi hao kwa kufanya kazi nae vyema katika kipindi chote cha miaka kumi ya uongozi wake akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Aidha, Rais Dkt. Shein amewataka wafanyakazi hao kuendelea kuwa watii, waaminifu na wavumilivu hasa ikizingatiwa kwamba ofisi wanayoifanyia kazi ni ofisi maalum kwa umhimu wake.
Nao wafanyakazi wa Ofisi ya Faragha ya Rais kwa upande wao wamempongeza Rais Dkt. Shein kwa kuwaongoza vyema, kuwalea na kufanya kazi kwa wema na kuavumilia katika kipindi chake chote cha miaka kumi akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Wafanyakazi hao wameeleza kuwa wamefarijika kwa kiasi kikubwa na uongozi wa Rais Dkt. Shein ambao umewafanyia mambo mengi wananchi wote wa Unguja na Pemba ikiwa ni pamoja na kuendeleza na kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo jambo ambalo Rais Dkt. Shein ameacha alama.
Sambamba na hayo, wafanyakazi hao wameeleza Kuwa, mafanikio makubwa yamepatikana katika miaka kumi ya uongozi wa Rais Dkt. Shein na wao wanaona faghari kwamba mafanikio hayo yamepatikana na wao wakiwa ni sehemu ya wasaidizi wa Rais.