Asasi ya Ushirikiano wa Siasa,Ulinzi na Usalama (TROIKA) ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeridhishwa na mazingira ya hali ya siasa nchini Tanzania ambayo yanaruhusu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28,2020 na kwamba wataendelea kufuatilia mazingira ya uchaguzi huo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi amesema TROIKA imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu tangu awali mchakato wa uchaguzi hapa nchini na kwamba imeridhishwa na mazingira ya amani yaliyopo hali inayoruhusu uchaguzi huo kufanyika.
"Leo katika mkutano wangu na TROKA ulifanyika kwa njia ya mtandao mwenyekiti wa TROIKA ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Botswana, Dkt. Lemogang Kwape ameoneshwa mazingira ya hali ya siasa nchini Tanzania yanaruhusu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 28,2020 na kwamba wataendelea kufuatilia mazingira ya uchaguzi huo,"amesema Prof. Kabudi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akieleza jambo wakati mkutano wa TROIKA ukiendelea. Mkutano huo ulifanyika kwa njia ya mtandao jijini Dar es Salaam.
Prof. Kabudi ameongeza kuwa, ni kwa mara ya kwanza katika historia ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu ipate uhuru uchaguzi huu
unagharamiwa kwa fedha ya walipa kodi, maamuzi ambayo yamefanyika kwa
kutambua kuwa demokrasia ndio jambo kubwa katika uhai,utashi na
kielelezo cha Taifa ambalo ni huru kama ilivyo Tanzania.
Kuhusu
waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, Prof Kabudi
amesema TROIKA imefanya tathimini ya awali ya hali ya usalama na kisiasa
na kwamba Tanzania inategemea kuwapokea waangalizi kutoka Umoja wa
Afrika na wale wa kutoka katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika tukio jingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi amepokea nakala za hati za
utambulisho za Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango
wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson. Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Sarah Gordon-Gibson akimueleza jambo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo
yao Prof. Kabudi amesema WFP imekuwa ni miongoni mwa mashirika ya
Kimataifa ambayo yanaushirikiano mzuri na Tanzania ambapo kwa mwaka 2018
WFP imenunua tani 160,000 za nafaka na 2019 wamenunua tani 36,000 zenye
thamani ya shilingi bilioni 21 fedha ambazo zimesaidia wakulima
wadogowadogo katika kuboresha kilimo.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Sarah Gordon-Gibson
amesema wamejadiliana namna ya kuendeleza ushirikiano baina ya pande
hizo mbili hususani kusaidia wakulima wadogowadogo nchini kuboresha
kilimo,kuboresha mazingira ya lishe na kwamba shirika hilo lina mpango
wa kuongeza msaada wanaoutoa kwa Tanzania.