Mkurugenzi wa JamiiForums aachiwa kwa masharti

Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media inayoratibu JamiiForums, Maxence Memo amehukumiwa kifungo cha nje na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Hukumu hiyo imetolewa leo Novemba 17, 2020 baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kuzuia askari kutekeleza majukumu yao. Aidha, Mahakama hiyo, imemuhukumu kifungo hicho wa masharti ya kutokurudia kosa hilo ndani ya mwaka mmoja.

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wa Mahakama hiyo ndiye aliyesoma hukumu hiyo huku upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Faraji Ngukah.

Hakimu Shaidi amesema, mshtakiwa alionekana kuwa na makosa katika kesi ambazo zilifunguliwa awali ambazo zote zilikuwa na makosa yanayofanana. Amesema, Jeshi la Polisi liko kwa ajili ya wote, ambapo kazi yake ni kupeleleza na ni wajibu wa kila mmoja kushirikiana nalo katika kazi zake.

Hata hivyo, mahakama hiyo ilimwachia huru mshtakiwa namba mbili katika kesi hiyo, Mike Mushi baada ya kutopatikana na hatia katika makosa yote, ambapo yeye alikuwa ni kama msindikizaji katika kesi hiyo.

Aidha, katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi sita ambao walikuwemo askari wapelelezi, ambapo upande wa utetezi Melo alijitetea mwenyewe bila kuwa na shahidi mwingine.

Pia kabla ya kusomwa hukumu hiyo, Wakili Ngukah aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa kwani kitendo alichokifanya cha kuzuia askari kutekeleza majukumu yao ni hatari kwa Taifa.

Kwa upande wa utetezi, Wakili wa Melo,Bernedict Ishabakaki aliomba kama sheria inatoa mbadala wa faini, Mahakama imuhukumu kutoa faini kwani ana vijana ambao amewaajiri na wanamtegemea hivyo faini itakuwa fundisho.

Hata hivyo, katika hati ya mashtaka, Melo na Mushi walidaiwa kuendesha mtandao ambao haujasajiwa kwa kikoa cha .tz na katika shitaka jingine walidaiwa kuzuia askari polisi kutekeleza majukumu yao, makosa wanayodaiwa kuyatenda kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13, 2016 katika eneo la Mikocheni wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments