Waziri Mkuchika:Waajiri wanakwamisha watumishi

Tatizo la watumishi wa umma kukaimu nafasi za uongozi kwa muda mrefu bila kupata stahili ya vyeo wanavyokaimishwa, linatokana na waajiri kutozingatia taratibu za kiutumishi pindi wanapowakaimisha watumishi hao kama Waraka wa Utumishi Namba 2 wa Mwaka 2018 unavyoelekeza, anaripoti James K.Mwanamyoto (OR-Utumishi) Morogoro.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Morogoro (hawapo pichani) alipoitembelea Ofisi hiyo kwa lengo la kupata taarifa ya utekelezaji wa masuala ya kiutumishi na utawala bora. (Picha na OR-Utumishi).

Hayo yamesemwa leo Desemba 21, 2020 mkoani Morogoro na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika alipoitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo kwa lengo la kupata taarifa ya utekelezaji wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.

Mhe. Mkuchika amesema, kumekuwa na tabia ya Waajiri wengi hususan katika halmashauri kuwakaimisha watumishi ambao hawana sifa za kukaimu wala kibali cha kukaimu ambacho kinatolewa na Katibu Mkuu-Utumishi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Ole Sanare akielezea changamoto za kiutumishi za Mkoa wake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika, alipoitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huyo kwa lengo la kupata taarifa ya utekelezaji wa masuala ya kiutumishi na utawala bora. (Picha na OR-Utumishi).

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, ili mtumishi aweze kukaimu, anapaswa kuwa na cheo cha Afisa Mwandamizi na kuendelea na pia awe amepatiwa kibali cha kukaimu nafasi husika na Katibu Mkuu-Utumishi ambacho atakitumikia kwa miezi isiyozidi 6 kabla ya kithibitishwa rasmi iwapo atakidhi vigezo vya kukitumikia cheo hicho.

Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, kitendo cha Watumishi kukaimishwa bila kufuata taratibu kimekuwa ni chanzo cha malalamiko ya watumishi wengi, hivyo amewataka Waajiri kuzingatia taratibu ili kuepuka malalamiko ambayo yanashusha morali ya utendaji kazi.
Baadhi ya Watendaji wa Mkoa wa Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George Mkuchika (hayupo pichani) alipoitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kupata taarifa ya utekelezaji wa masuala ya kiutumishi na utawala bora. (Picha na OR-Utumishi).

Wakati huo huo, Mhe. Mhe. Mkuchika amewataka Waajiri kuhakikisha wanawawezesha wastaafu kupata mafao yao kwa wakati pindi wanapostaafu ili kuwaondolea usumbufu wa wa kufuatilia mafao yao pindi wanapostaafu ikizingaatiwa kuwa wamelitumikia taifa kwa bidii na uadilifu.

Mhe. Mkuchika amesema, ili Wastaafu wapate mafao kwa wakati, Maafisa Utumishi wanapaswa kufanya maandalizi kwa kukusanya vielelezo vyote vinavyohitajika mapema miezi 6 kabla.

"Kutokana na changamoto hii, nitafanya mkutano na Maafisa Utumishi nchi nzima kama nilivyoahidi hapo awali ili kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu suala hili,” Mhe. Mkuchika amesisitiza

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekekezaji ya Mkoa wa Morogoro, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Mhandisi Emmanuel Kalobelo alimwambia Mhe. Waziri kuwa, pamoja na mafanikio mazuri yaliyopatikana katika Mkoa wa Morogoro, Ofisi yake ina changamoto ya watumishi kukaimu kwa muda mrefu na wastaafu kutokapata mafao yao kwa wakati pindi wanapostaafu.

Post a Comment

0 Comments