Wizara zenye hoja za Muungano zatakiwa kukaa mapema

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu, amezitaka wizara ambazo zina hoja 11 za Muungano ambazo hazijapatiwa ufumbuzi kukaa mara moja ili kuzipatia ufumbuzi wa pamoja, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Waziri Ummy ameyasema hayo leo katika kikao cha pamoja baina yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Zanzibar Dkt. Khalid Mohammed mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Ofisi ya Makamu wa Rais Mtumba Dodoma kwa lengo la kujitambulisha.

Amesema, wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha wanaimarisha Muungano na kuhakikisha una kuwa imara kwa sababu Muungano ndio umoja wetu, usalama wetu na amani yetu.

“Hatutamvumilia mtu yoyote anayeleta chokochoko na kutaka kuvuruga umoja na mshikamano wa Watanzania,”amesema Waziri Ummy.

Kwa upande wake Waziri Dkt. Khalid Mohammed amesema, Serikali zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimefanya kazi kubwa katika kuondoa changamoto kumi ndani ya kipindi cha miaka mitano.

“Kupitia vikao vya Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ ndani ya kipindi cha miaka mitano jumla ya changamoto 21 ziliwasilishwa na kati ya hizo changamoto 10 zimepatiwa ufumbuzi, ni imani yangu kuwa hata zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi kwa kuwa viongozi wetu wana dhamira ya dhati,”amesisitiza Dkt. Khalid.

Amesema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar imeanza matayarisho ya ujenzi katika kiwanja chenye ukubwa wa ekari 33 katika eneo la Mahoma Makulu ili kurahisha kazi ya uratibu.

Waziri Ummy amemuhakikishia Waziri Khalid kufanya kazi kwa pamoja katika kuimarisha misingi ya amani, umoja na mshikamano kwa maslahi ya pande zote mbili za Muungano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news